JENGO
la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNIA-TBIII) linalotarajiwa kukamilika Desemba 2018, litafungwa mfumo
wa huduma ya viza kwa njia ya mtandao (e-visa), ambao utarahisha na
kuharakisha upatikanaji wake.
Kaimu
Mkuu wa Kitengo cha Uhamiaji cha JNIA, Bw. Kaanankira Mbise amemwambia
jana Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi
na Mawasiliano), Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye alipotembelea eneo la
uombeaji viza kwa abiria wa kimataifa wanaowasili, kuwa wanatarajia
kutumia huduma hiyo ambayo ni rahisi na haraka.
“Tayari
mkakati umeanza wa kuanzisha huduma hii ya e-visa hivyo tukifanikiwa
utafungwa katika jengo hili jipya, ambapo itasaidia kwa abiria kuipata
huduma hiyo kwa haraka kwani itatumia mtandao,” amesema Bw. Mbise.Hata
hivyo, Bw. Mbise amesema kwa sasa wameboresha huduma hiyo kwa wasafiri
wanaowasili katika jengo la pili la abiria (JNIA-TBII) , ambapo tayari
wamepatiwa mashine nne za kisasa zinazosaidia kupunguza msongamano wa
abiria wenye kuhitaji huduma hiyo, hususan kipindi cha mchana chenye
ujio wa ndege nyingi za nje ya nchi.
“Hizi
mashine zimeharakisha upatikanaji wa huduma kwani tumeweza kuhudumia
abiria wengi kwa wakati mmoja, na msongamano umepungua kiasi tofauti na
awali mashine zilikuwa chache.” amesema Mbise.Naye Mhe. Mhandisi Nditiye
amesema baada ya ziara yake amegundua mashine za viza ni za muda mrefu
na zinahudumia abiria mmoja kwa mrefu, na tayari ameuagiza uongozi wa
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuwasilisha kwa maandishi
mapendekezo yao ya namna ya kuharakisha huduma hiyo, ili serikali
iyafanyie kazi kwa kusaidia kuondoa kero hiyo.
“Nimegundua
kuna baadhi ya mashine za viza zimeongezwa lakini pia zilizopo
zimechoka kwani ni za muda mrefu na zinahudumia abiria mmoja kwa muda
mrefu na hii inaharibu sifa ya kiwanja chetu kwa wageni wanaokuja hapa
nchini,” amesema Mhandisi Nditiye.Hata hivyo, amesema wanampango wa
kuongeza madirisha ya benki yanayolipia viza hizo ili kuharakisha huduma
hiyo, ambapo sasa ni machache kulinganisha na idadi kubwa ya abiria
wanaowasili kwa ndege kubwa. Ndege hizo ni Emirates, Etihad, Oman Air,
Qatar, South Africa Air na Ethiopia, ambazo zimekuwa zikipishana kwa
muda mfupi.
Naye
Kaimu Mkurugenzi wa TAA, Richard Mayongela amesema tayari wanampango wa
kuongeza upana wa eneo hilo la wasafiri wanaowasili wa kimataifa, ambapo
sasa kumekuwa na msongamano kutokana na ufinyu wake.“Hili jengo
linazaidi ya miaka 30 na ukiangalia abiria waliokuwa wamekadiriwa wakati
ule lilikuwa likikidhi mahitaji, lakini sasa abiria wameongezeka na
eneo limekuwa dogo, hivyo tayari tumeanza kwa kuondoa baadhi ya ofisi
ili kuongeza upana wake, ninaimani litapunguza msongamano uliopo sasa,”
amesema Bw. Mayongela.
Lakini
pia Bw. Mayongela amesema sasa wapo katika mazungumzo na Mamlaka ya
Usafiri wa Anga (TCAA), ili kuangalia namna bora ya kuzipangia muda
ndege zinazopishana muda mdogo kwa wakati wa mchana ili ziachiane muda
mrefu, ambapo kutasaidia kupunguza msongamano.Awali eneo hilo linakumbwa
na changamoto kubwa ya msongamano wa abiria wanaohitaji huduma ya viza
baada ya uchache mashine zinazosimamiwa na Idara ya Uhamiaji
zilizokuwepo na kufanya abiria wanaohitaji huduma hiyo kutumia muda
mrefu kuipata.
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na
Mawasiliano), Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto)
akiwaeleza jambo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (kulia) na Kaimu Mkurugenzi
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes
Munanka katika eneo la kuchukua mizigo baada ya kuwasili.
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw.
Richard Mayongela (aliyenyoosha mkono), akimfafanulia jambo Naibu Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano),
Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye (wa nne kulia) wakiwa kwenye eneo la
abiria wanaowasili kutoka nje ya nchi.
Bw.
Kaanankira Mbise, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhamiaji Kiwanja cha Ndege
cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), akieleza namna abiria
anavyopata huduma ya viza mbele ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano), Mhe. Mhandisi Atashasta
Nditiye (kushoto), huku Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (kulia) akisikiliza kwa makini.

No comments:
Post a Comment