Makamu wa
Rais Samia Suluhu Hassan anaondoka nchini leo kwenda Papua New Guinea
ambako atamwakilisha Rais John Magufuli katika mkutano wa Wakuu wa nchi
za Afrika, Caribbean na Pacific (ACP) ambao utafanyika kuanzia Mei 30
hadi Juni 01, mwaka huu.
Mkutano
wa Papua New Guinea ambao utatanguliwa na mkutano wa mawaziri wa mambo
ya nje wa nchi za ACP utafanyika chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu wa
nchi hiyo Mhe. Peter O'Neil.Kauli
mbiu ya mkutano huo wa mwaka huu ni "Umuhimu wa nchi za ACP kujipanga
kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za maendeleo endelevu."
Maeneo
ya mjadala ni pamoja na kukuza usawa na maendeleo endelevu kwa ajili ya
wananchi wa nchi wanachama, kuimarisha majukumu ya nchi za ACP katika
utawala bora na maendeleo na pia masuala ya amani, usalama and utulivu
wa kisiasa kama ni sharti mojawapo kwa maendeleo.
Kwa
sasa umoja huo wa ACP una nchi wanachama 79 ambapo kati ya hizo nchi 48
ni za kutoka kusini mwa jangwa la Sahara, 16 kutoka Caribbean na 15
kutoka Pacific.
Umoja
wa nchi za ACP ulianzishwa baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa Georgetown
mwaka 1975 kwa msaada wa iliyokuwa Tume ya Uchumi ya Ulaya kwa
madhumuni ya kuratibu ushirikiano baina ya nchi wanachama na Umoja wa
Ulaya ukizingatia kwamba nyingi ya nchi hizo ni makoloni ya nchi za
ulaya.
Katika
msafara huo Makamu wa Rais amefuatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha
na Mipango Dk. Servacius Likwelile na Mkurugenzi wa Idara ya
Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa Balozi Celestine Mushi.
Makamu wa Rais na ujumbe wake anatarajia kurudi nchini Juni 3,mwaka huu.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
27/5/2016
No comments:
Post a Comment