Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo (mbele katikati), akiongea jambo wakati wa
kikao kati yake na wawekezaji katika Sekta ya Nishati, katika Ukumbi wa
Tanesco, Jijini Dar es Salaam. Kulia kwa Waziri ni Mkurugenzi wa Kituo
cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Julieth Kairuki.
Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo, akiongea jambo na baadhi ya wawekezaji mara
baada ya kikao chake na wawekezaji ambao wameonesha nia kuwekeza katika
vyanzo mbali mbali vinavyopatikana nchini na baadhi wamefika kupata
taarifa kuhusu uwekezaji.
Baadhi ya Watendaji kutoka
Taasisi zilizo chini ya Wizara na Maafisa kutoka Wizarani wakifuatilia
kikao kati ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo na Wawekezaji
katika Sekta ya Nishati,
Baadhi ya Wawekezaji
wakiwasilisha taarifa zao za uwekezaji kwa Waziri wa Nishati na Madini
Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani). Baadhi ya maswali ambayo
Profesa alihoji kutoka kwa wawekezaji hao wao ni uwezo wao kifedha,
kiteknolojia,utaalam na uzoefu wa kazi katika vyanzo walivyochagua
kuwekeza nchini.
…………………………………………………………………………………………..
Asteria Muhozya na Nuru Mwasampeta, Dar es Salaam
Kutokana na mahitaji makubwa ya
Nishati ya umeme barani Afrika, ambapo kiasi cha wananchi wake
wapatao bilioni 1 wanatajwa kuwa bado wapo gizani Tanzania ikiwa
miongoni mwao, imeelezwa kuwa, wawekezaji katika sekta hiyo wanavyo
vyanzo vya uhakika vya kupata fedha za uwekezaji.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati wa mwendelezo wa
vikao vyake na wawekezaji katika sekta ya Nishati vilivyoanza tarehe
15-18 Februari, 2016, ambavyo vililenga kukutana na wawekezaji wenye
nia ya kuwekeza katika vyanzo mbalimbali vya nishati vinavyopatikana
nchini ili kuhoji na kubaini kampuni ambazo ziko tayari na zina uwezo wa
kuwekeza.
Prof. Muhongo amevitaja vyanzo
hivyo kuwa ni pamoja na Mpango wa Serikali ya Marekani kusaidia
maendeleo ya sekta ya umeme barani Afrika unaoitwa ‘Power Africa
Initiative’ ambao umetengewa Dola za Marekani Bilioni 6 ambapo Tanzania
ni moja ya nchi zinazopewa kipaumbele katika mpango huo.
Aidha, ameongeza kuwa, Tanzania
ni miongoni mwa nchi ambazo ipo katika nafasi nzuri ya kufaidika na
fedha za Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Nishati Endelevu kwa Wote
(SE4ALL) ambapo mpango huo unaelekeza kuwa, ifikapo mwaka 2030 kuwe na
upatikanaji umeme kwa wote na ongezeko maradufu la utumiaji umeme wa
nishati jadidifu na matumizi bora.
Pia, Profesa Muhongo ameeleza
kuwa, kutokana na mahitaji ya umeme Duniani kupanda kwa asilimia 26
tayari kiasi cha Dola za Marekani trilioni 48 zimetengwa, ili kuongeza
kiasi cha watumiaji wa nishati hiyo ifikapo 2020-2035, ambapo dola za
Marekani trilioni 40 zikiwa zimetengwa kwa ajili ya kusambaza umeme na
kiasi cha dola za Marekani trilioni 8 kwa ajili ya matumizi bora ya
nishati.
Vilevile, ameutaja mpango wa
‘China Afrika Partnership’ ambapo kiasi cha Dola za Marekani bilioni 60
zimetengwa kwa ajili ya miundombinu , huku nishati ikipewa kipaumbele na
kuongeza kuwa, kutokana na urafiki wa muda mrefu na mahusiano mazuri
kati ya Serikali ya Tanzania na Watu wa China, Tanzania iko katika
nafasi nzuri za kupata fedha hizo.
Halikadhalika, Profesa Muhongo
ameleeza kuwa, Umoja wa nchi za Ulaya (European Union) pia ni chanzo
kingine kwa wawekezaji kupata fedha kwa kuwa, nishati imekuwa kipaumbele
kwa taasisi hiyo.
“Wawekezaji makini macho yote
sasa yapo Afrika. Tunataka fedha hizo zote zije Tanzania kuwekeza katika
sekta ya nishati. Jipangeni vizuri mwende, ‘Power Africa’ na sehemu
nilizotaja, fedha za uhakika za umeme zipo. fedha,”amesisitiza Prof.
Muhongo.
Aidha, kutokana na umuhimu na
uharaka wa kutekeleza mipango hiyo, Profesa Muhongo amewataka wawekezaji
ambao wako tayari kuwekeza nchini kuzingatia muda na ratiba ya
kutekeleza majukumu yao na kuongeza kuwa, “ikiwa kuna jambo
litacheleweshwa na watendaji wa Serikali, tutachukua hatua, na ikiwa
mwekezaji umeshindwa kwenda na muda wetu vizuri basi mradi wako utaachwa
na wengine kupewa nafasi,”ameongeza Muhongo.
Profesa Muhongo amebainisha kuwa
fursa za uwekezaji katika sekta ya nishati zinapatikana katika maeneo ya
gesi asilia, makaa ya mawe, nishati jadidifu umeme wa maji, upepo,
umeme wa jua biogas na vyanzo vingine.
No comments:
Post a Comment