Nabii Mpanji akimuombea Naibu Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba.
Waumini wa Kanisa la GMCL wakifuatilia Ibada
MKURUGENZI wa Kituo cha Redio
cha GMCL fm na Mwasisi wa Kanisa la GMCL lililopo Ilomba Jijini Mbeya, Nabii
Mpanji,amemtaka Naibu Waziri wa Fedha na Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu
Nchemba kuacha uoga wa kutangaza nia ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu
ujao.
Nabii huyo aliyasema hayo
alipokuwa akihubiri katika ibada ya Harambee ya kuchangia miradi ya Kanisa
ambapo Naibu Waziri alialikwa kama mgeni rasmi, na kuongeza kuwa asiwe na wasi
wasi wa kutangaza nia kutokana na kuwa na watu wengi nyuma yake.
Alisema yeye kama Nabii
ameoneshwa kuwa kuna mafuta ya uongozi kwa Mwigulu Nchemba hivyo asiogope
kutangaza nia kwa kuwahofia wazee kwani Taifa kwa sasa linahitaji kijana
mzalengo na mchapa kazi ambaye ataweza kukusanya kodi na kusimamaia Watanzania
wenye vipato vya chini.
“Wapo wanaonibeza kuwa mimi ni
Nabii wa Uongo lakini katika watu nilioneshwa wenye nia ya kwenda Ikulu na wewe
umo hivyo usiwaogope wazee,Sema leo hapa watu wakusikie, Maandiko yanasema
Fahari ya Wazee ni Mvi zao na fahari ya vijana ni nguvu sisi tunahitaji vijana”
alisisitiza Nabii Mpanji.
Aliongeza kuwa mara nyingi
viongozi wa Serikali wamekuwa wakiwataka viongozi wa dini kuliombea Taifa
pamoja na uchaguzi Mkuu ujao lakini hakuna anayerudi kuchukua majibu juu ya
maombi hayo kama Mungu amejibu nini kuhusiana na uchaguzi huo.
“Nimesimama hapa kwa niaba ya
Serikali ya Mbinguni na ninakupa mafuta ambayo mtu yoyote atakayejaribu
kuchafua nyota yake atachafuka mwenyewe kwani kinachohitajika ni Pesa mfukoni,
Yesu moyoni na akili Kichwani” alisema Nabii huyo huku akishangiliwa na waumini
wake.
Aliongeza kuwa Taifa linahitaji
mabadiliko kwa kumpata kiongozi mzalendo mwenye uchungu na mapato ya Watanzania
na kuongeza kuwa Kanisa la GMCL liko tayari kumchangia fedha za kuchukulia fomu
ya kugombea urais.
“Neno linalotoka kinywani kwa
Nabii ni sheria wako maherode wengi hao
wasikukatishe tamaa waswahili wanasema kaza buti” alimalizia Nabii Mpanji.
Kwa upande wake Mwigulu Nchemba
alijibu kauli ya Nabii kwa kunukuu maneno machache kutoka Kitabu kitakatifu cha
Biblia akisema“Heri mtu Yule asiye na mashaka na mimi” Kodi zitakusanywa na
zitatumika vizuri.
“Nawashukuru Watanzania wenye
imani na mimi bado kitambo kidogo ili taratibu za Kichama zikamilike hivyo
nitasema kwa sasa tusubiri tuko ukingoni mwa mto Jordani tunakaribia kuvuka”
alisisitiza Nchemba huku waumini wakimshangilia kwa kumuita Rais.
Na Mbeya yetu
No comments:
Post a Comment