Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Jenister Mhagama amewataka
wanasiasa kuacha kuingilia taaluma ya walimu hasa wanapochukua hatua za
kinidhamu kwa wanafunzi hatua inayodaiwa kuua maadili kwa watoto.
Mhagama alisema hayo baada ya kuitembelea shule ya sekondari
ya wavulana Njombe (Njoss) iliyofungwa na serikali kwa muda wa mwezi mmoja kuanzia
Oktoba 8 hadi Novemba 8 mwaka huu, baada ya wanafunzi kuchoma moto bweni,
karakana na kuharibu mali mbalimbali za shule na kuharibu majengo ya shule ya
msingi Kilimani iliyopo jirani hatua inayodaiwa kusababishwa na utovu wa
nidhamu kwa baadhi ya wanafunzi.
Katika ziara hiyo pia alitumia fursa hiyo kuzungumza na
walimu wa shule hiyo na shule za sekondari jirani za Joseph Mbeyela na Mpechi
ambao walimweleza kero rukuki wanazokumbana nazo katika utendaji wao wa kazi.
Baadhi ya kero hizo ni kuchelewa kupandishwa madaraja,
malimbikizo ya fedha za kujikimu, wanasiasa kuwaingilia wanapochukua hatua za
kinidhamu kwa watoto, ukosefu wa miundombinu mizuri ya makazi ya walimu, umeme
na maji.
Akisoma taarifa ya kufungwa kwa shule hiyo kwa Naibu Waziri
huyo, Mkuu wa shule Bernard William, alisema inatokana na wanafunzi hao kufanya
vurugu tarehe 7 ya mwezi huu usiku, zilizosababisha kuchoma bweni, karakana,
kuharibu nyumba mbili za walimu na kuvunja gari na duka zote zikiwa mali za
mwalimu wa nidhamu.
Alisema chanzo cha tukio hilo kilitokana na wanafunzi 29
waliotoroka shule usiku wa Septemba 6, mwaka huu kwenda disko katika chuo cha
maendeleo ya jamii Njombe ambako walifanya fujo zilizosababisha mwenzao mmoja
kuvunjika mguu.
William alisema baada ya kuzidiwa nguvu katika fujo hizo
walikimbilia shuleni na kuanza kuwaamusha wenzao kwenda disko kulipiza kisasi,
lakini hawakufanikiwa kutokana na walimu kuingilia kati kwa kuwaamru wakalale.
“Tarehe 7, 10,2014 bodi ya shule ilikutana na kuamru
wanafunzi hao warudi nyumbani na wazazi wao kusubiri maelekezo ya namna ya
kurejea shuleni, lakini cha kushangaza siku hiyo hiyo majira ya saa 3 usiku
zilisikika sauti za watu wachache wakisema wanataka waliorudishwa nyumbani kwa
kosa la kwenda disko walejeshwe shuleni mara moja, na ndipo vurugu zilipoanza,”
alisema William.
Mwalimu William alimweleza Naib Waziri huyo kuwa uchunguzi
uliofanyika ndani na nje ya shule umebaini kuwa hakukuwa na sababu nyingine ya
msingi zaidi hiyo, na kwamba kutokana na vurugu hiyo tathmini imefanyika na
kubaini uharibifu huo umesababisha hasara ya sh. 144,340,000 milioni, ingawa
taarifa ya polisi inasema hasara iliyotokana na tukio hilo ni sh. 113,050,000.
Alisema kila mwanafunzi ameamriwa kurudi shuleni na sh
150,000 kama fidia ya uharibifu huo pindi shule itakapofunguliwa tarehe
8.11.2014. na kuongeza kuwa wanakusudia kuanza ujenzi wa bweni hilo kuanzia
mwezi Novemba mwaka huu na kumalizika Januari mwakani.
Akijibu baadhi ya kero za walimu hao, Mhagama aliwataka
wanasiasa kuacha kuingilia taaluma ya
walimu hasa pale wanapochukua hatua za kinidhamu kwa wanafunzi kwa kusema:
“Nawaomba wanasiasa wenzangu tuache kuingilia taaluma ya walimu, mwalimu
anapochukua hatua za kinidhamu hapaswi kuingiliwa na wanasiasa, na suala hili
la nidhamu kwa wanafunzi tutalipa nguvu zaidi kwa walimu ili tuweze kupata
wasomi wenye maadili.”
Alisema nidhamu ina mfanya mwanafunzi kuwa na maadili mema,
na hivyo kuimarisha amani katika jamii ikiwemo taasisi husika, na kuwataka walimu
kusimamia ipasavyo nidhamu ya wanafunzi, huku akiwasisitizia nidhamu kuanza na
watumishi wa kada hiyo kama walezi wa watoto wa muda mwingi ikilinganishwa na
wazazi.
“Amani kwenye taasisi yeyote
ni muhimu sana, hasara iliyopatikana hapa haizungumziki. Walimu simamieni
nidhamu ya wanafunzi lakini nidhamu ianze na ninyi wenyewe kwa kulinda maadili
ya taaluma yenu,” alisema Mhagama.
“Kuna baadhi yenu wanavunja maadili hilo msikatae. Mfano
nilifanya ziara ya kushutukiza katika shule moja pale Dodoma nikakuta mwalimu
amevaa nguo fupi ya kubana , na kuna tukio jingine kule Rukwa mwalimu wa kike amezaa
na mwafunzi wa kidato cha pili sasa hapa nani aliumiwe? Alihoji Mhagama na
kuongeza.
“Nidhamu ya watoto wetu imeshuka sana na ninyi ndio wenye jukumu
kubwa la kuhakikisha wanafunzi hawa hawaharibikiwi kimaadili. Walimu tuna
maadili yetu ya kuvaa, kutembea, kuongea na hata kuamkia watu lazima
tuyazingatie,” alisema.
Aidha alitumia fursa hiyo kuwaeleza walimu hao kuwa serikali
inashughulikia madai mbalimbali ya walimu ikiwemo malimbikizo ya fedha zao
pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili kama vile nyumba za
kuishi na miundombinu ya maji na umeme
shuleni.
Alisema hata hivyo matatizo ya walimu yatapungua kabisa au
kumalizika pindi itakapoanza tume ya utumishi wa walimu iliyoingizwa katika
rasimu ya katiba pendekezwa, ambayo alidai itakuwa na jukumu la kusimamia kero
mbalimbali za walimu ikiwemo upandishwaji wa madaraja na kusimamia nidhamu ya
watumishi hao ambayo inadaiwa kushuka kwa baadhi yao kutokana kukosekana kwa
chombo maalum cha kuwasimamia.
Alitumia fursa hiyo kuwataka walimu hao kuisoma rasimu hiyo
na kuelewa maadhui yaliyomo badala ya kusomewa watu.
Katika tukio hilo wanafunzi 15 wa shule hiyo kati ya 987
walishikiliwa na polisi kwa mahojiano.
No comments:
Post a Comment