Na Benedict Liwenga, MAELEZO-Dodoma.
MJUMBE wa Bunge Maalum la Katiba ambaye pia ni
Mwenyekiti wa TCD Mhe. John Cheyo amewataka Watanzania kutodanganywa kuhusiana
na mchakato mzima wa kusaka Katiba Mpya.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mhe. Cheyo wakati
alipokuwa akifanya mahojiano katika kipindi cha asubuhi cha Jambo kinachorushwa
na Televisheni ya Shirika la Habari Tanzania (TBC).
Mhe. Cheyo amesema kuwa ni vema viongozi kuacha kusema
uwogo na kuwa waungwana katika mchakato wa kutafuta Katiba Mpya kwani si vema
kuitakia Tanzania mabaya bali ni kutaka mchakato huo wa Katiba uendelee kwa
amani.
Ameongeza kuwa Taifa la Tanzania linahitaji kuwa Taifa
lenye nguvu kwani amani haiwezu kuwekewa thamani kwa vurugu, hivyo ametaka
amani iliyopo nchini ilindwe na kuepuka kudanganywa na baadhi ya watu wasiokuwa
na nia njema na nchi.
Mhe. Cheyo ameshangazwa kwa kitendo cha viongozi wa
UKAWA kutoweka ajenda ya kurudi ndani ya Bunge hilo wala kuzungumzia kuhusu suala
hilo la kurudi ndani, bali wamekuwa wakitaka wajumbe wengine walioko ndani
watoke kwa kusema kuwa bunge hilo sio halali.
“Nawashangaa UKAWA kwa kutoweka ajenda ya kurudi ndani
ya Bunge hili Maalum la Katiba na badala yake wao wanaweka ajenda ya kutoka ndani
ya bunge hili tena kwa nguvu”, alisema Mhe. Cheyo.
Aidha, Mhe. Cheyo amewataka vijana nchini wawe na
mshikamano na kuepuka kudanganywa na viongozi kwa kuambiwa mambo yenye uwongo
huku akisisitiza kuwa Rais aliyeko sasa hivi ana nia njema ya kuipatia nchi
Katiba iliyo bora na yenye kumfaa kila Mtanzania.
“Vijana achene kuvunjika miguu yenu bure, achene
kukimbia kimbia barabarani huku mkilishwa maneno yenye uongo kuhusiana na
mchakato huu wa Katiba, vunjikeni miguu kwa kufanya kazi kwa bidiii na sio kusikiliza
uwongo”, alisema Mhe. Cheyo.
Akizungumzia kuhusu TCD, Mhe. Cheyo amefafanua kuwa
TCD ni Jukwaa la majadiliano kwa ajili ya maridhiano na mapatano pale
panapokuwa na tofauti kati ya vyama vya siasa.
“TCD ni Jukwaa kwa ajili ya kufanya majadiliano na si
vinginevyo, hii ni meza ya maridhiano na nawaambia kuwa huko mnapokwenda ni
kuchepuka, rudini ndani kwenye njia kuu”, alisisitiza Mhe. Cheyo.
Naye mjumbe wa Kamati namba Sita ya Bunge Malaam la
Katiba Mhe. Steven Wasira amewaasa Watanzania kwa kusema kuwa, watu wanaosema
kuwa Bunge limenyofoa baadhi ya mambo muhimu yanayohusu wananchi ni waongo na
wenye nia ya kupotosha Umma wa Tanzania.
“Kuna watu wanasema kuwa Bunge Maalum la Katiba
limenyofoa baadhi ya mambo muhimu yanayohusu wananchi huo ni uwongo, ni mambo
gani hayo yaliyonyofolewa? kwasababu kuna mambo mengi yameongezwa na kuboreshwa
katika mapendekezo kwa ajili ya makundi mbalimbali ndani ya hiyo Rasimu”,
alisema Mhe. Wasira.
Mhe. Wasira ameongeza kuwa katika Bunge hilo kuna
Ibara ya Rasimu ya Katiba na sio ibara za CCM, amewataka Watanzania nchini
wafanya uchunguzi na kusikiliza kwa kuchambua ili kupata ukweli wa hayo.
“Sisi tuko tayari kuvaana na viopngozi wowote kwani
tunataka Watanzania wote waamini shughuli zifanywazo ndani ya bunge hili na
waepuke kudanganywa”, alisema Mhe. Wasira.
No comments:
Post a Comment