JAMANI MBEYA MATUKIO HAYAISHI KWA NINI.
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida wananchi wa
kijiji na kata ya Mkwajuni Wilaya ya Chunya Mkoani hapa wamemzika Mwanakijiji
mwenzao akiwa hai wakimtuhumu kusababisha kifo cha Mkazi mmoja kijijini hapo.
Tukio hilo la kusikitisha limetokea Apri 26
mwaka huu majira ya Saa Nane Mchana katika Kitongoji cha Maweni
Makaburini baada ya Mhanga aliyefahamika kwa jina la Victory Mwachirui(68)
kuhudhuria mazishi ya Pita Barton(28)aliyefariki baada ya kuugua kwa muda
mrefu.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Thobias
Ismail amesema marehemu alipatwa na umauti akiwa anapatiwa matibabu kwa mganga
wa jadi ambaye jina lake halikuweza kujulikana maramoja.
Amesema wakati taratibu za mazishi zikiendelea
Ndugu wa marehemu walidai kuwa kifo cha Marehemu kilisababishwa na Mwachirui
ambaye ni Katekista mstaafu kwa imani za kishirikina.
Ameongeza kuwa wakati kaburi likichimbwa kwa
ajili ya kumzika marehemu ndipo vijana waliokuwa wakichimba waliagiza
Wazee wa Mila wafike makaburini kwa ajili ya kuangalia utaratibu wa mazishi na
kukagua ukubwa wa Kaburi ambalo lilikuwa limekwisha chimbwa.
Kutokana na mwito huo walifika wazee wanne
akiwemo Mzee Mwachirui ambaye walimsisitiza kusogea jirani na kaburi ambapo
baada ya kusogea alipigwa na Sururu kichwani na kuangukia kaburini huku
akisindikizwa na marungu.
Baada ya Mzee huyo kupoteza fahamu Vijana
hao walianza kutandika fito ndani ya kaburi kisha kufukia kwa udongo kiasi kwa
lengo la kutenganisha na Mwili wa Marehemu Pita uliokuwa kwenye jeneza baada ya
kuwazika kwenye kaburi moja.
Baada ya kukamilika kwa zoezi la mazishi kundi
la vijana lilielekea hadi nyumbani kwa Mzee aliyezikwa akiwa hai na kuiteketeza
nyumba yake huku wakiapa kutotoa siri wakidai Siri ya Jeshi.
Hata hivyo baadhi ya wananchi walitoa taarifa
kwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho aliyefahamika kwa jina la Credo Kayanza ambaye
pia alitoa taarifa kwa Diwani wa Kata hiyo Chesco Ngairo ambao kwa pamoja
walitoa taarifa Jeshi la Polisi ambao baada ya taarifa hiyo walifika eneo la
tukio huku wakidhani lililotokea ni kuchomwa kwa nyumba pekee.
Jeshi la Polisi baada ya kufanya upelelezi na
kubaini kitendo hicho waliwaamuru baadhi ya Vijana kufukua kaburi hilo zoezi
ambalo lilifanyika baada ya Vijana hao kulipwa.
Baada ya kufukuliwa kwa kaburi hilo Mwili wa
Marehemu Mzee Mwachirui ulichukuliwa na kupelekwa katika Hospitali ya Misheni
ya Mkwajuni kwa ajili ya Uchunguzi huku Mwili wa Pita ukizikwa upya palepale.
Baada ya kukamilika kwa uchunguzi mwili wa
marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi ambapo Marehemu alizikwa
katika eneo tofauti na alipokuwa amefukiwa awali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo pia ametoa wito na kuwaasa
wananchi na jamii kuacha tabia ya kuamini mambo ya ushirikina na uchawi
kwa madai kuwa hauna faida kwao bali huchochea migogoro katika jamii zao.
Aidha ameongeza kuwa wakumbuke kitendo cha
kujichukulia sheria mkononi ni kosa kisheria ambapo pia amewaomba wenye
taarifa za walipo waliohusika na mauaji hayo kuzifikisha polisi haraka ili
hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao ingawa hakuna aliyekamatwa kuhusika na
tukio hilo.
Picha na E. Kamanga wa Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment