Pages

CONTACT

0757092504/0678321772

Wednesday, February 14, 2018

BIL. 161.9 ZIMETUMIKA KUBORESHA VITUO VYA AFYA 170-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetumia sh. bilioni 161.9 kuboresha vituo vya afya 170 nchini pamoja na kugharamia huduma ya Afya ya Mama na Mtoto kwa lengo la kuokoa maisha yao.

Amsema Serikali itaendelea kukarabati na kupanua miundombinu ya kutolea huduma pamoja na kununua vifaa vya kisasa katika Hospitali za Mloganzila, Benjamini Mkapa, Dodoma na Hosptali za Rufaa katika Mikoa na Kanda.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Februari 14, 2018) wakati akizindua jengo  jipya la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa-Amana iliyopo wilayani Ilala jijini Dar es Salaam.

Jengo hilo la ghorofa mbili limejengwa kwa ufadhili wa kundi la kampuni za AMSONS na lina thamani ya sh bilioni 1.2.

Amesema uzinduzi wa jengo hilo  unakwenda sambamba na azma ya Rais Dkt. John Magufuli za kuimarisha sekta ya afya na kuifanya kuwa miongoni mwa sekta za kipaumbele.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha inasogeza huduma za afya karibu na wananchi. “Mfano, Hospitali za Rufaa za Amana, Mwananyamala na Temeke, zimeendelea kuhudumia wagonjwa kutoka Zahanati, Vituo vya Afya vya Serikali, binafsi na vya dini kutoka mikoa jirani ya Pwani, Morogoro na Lindi.

Pia amesema Serikali itaendelea kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 – 2020, kuhusu kuwapatia wananchi huduma bora za afya pamoja na kujenga hospitali nyingine za Rufaa kwa ajili ya Kanda ya Kusini, Kati na Magharibi.

Akizungumzia kuhusu changamoto ya idadi ndogo ya watumishi na ukosefu wa huduma za uangalizi maalumu (ICU) katika hospital ya Amana, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kufanyia kazi changamoto zote zilizopo katika sekta ya afya zikiwemo n aza hospital hiyo.

Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuthamini na kutambua mchango wa wadau mbalimbali pamoja na kuendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha kuwa huduma za afya nchini zinaboreshwa.

Hivyo, alitumia fursa hiyo  na kulipongeza kundi la kampuni za AMSON’s lililoamua kujenga jengo la mama na mtoto katika hospital hiyo kwa ushawishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul Makonda.

Awali, Mganga Mkuu Hospitali ya Rufaa ya Mkoa – Amana, Dkt. Meshack Shimwella alisema wazazi wanaolazwa katika hospitali hiyo kwa siku ni 180 hadi 250 na uwezo wa hospitali ni vitanda 353, ambapo vitanda 250 vinatumika wodi ya wazazi.

Alisema idadi hiyo hailingani na idadi ya wagonjwa, hivyo kusababisha wakati mwingine wagonjwa kulala zaidi ya mmoja kwenye kitanda kimoja kutokana na kasi ya ongezeko wa wagonjwa wanaolazwa hususani wodi ya watoto na akinamama.

Dkt. Shimwella alisema wamefanikiwa kuongeza jingo la kutolea huduma ya mama na mtoto lenye ghorofa mbili ilililojengwa kwa ufadhili wa AMSONS lenye uwezo wa vitanda 100, ambalo ndilo liliongeza idadi ya vitanda kutoka 253 hadi kufikia 353.

“Kutokana kukamilika kwa jengo hilo kwa sasa akinamama wanaonyonyesha wanalala wakiwa mmoja mmoja, watoto wachanga wanahudumiwa katika mazingira mazuri yanayofanana na viwango Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.”

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Makonda aliwashukuru wafadhili waliojenga jengo hilo kwa sababu si kila mtu anayekwenda hospitali na kukuta changamoto na akaamua kuzifanyia kazi.

Bw. Makonda alisema awali akinamama walikuwa wanalala hadi watatu katika kitanda kimoja, hivyo madhumuni ya ujenzi wa jego hilo ni kupunguza msongamano katika wodi ya wazazi.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, FEBRUARI 14, 2018.

No comments:

Post a Comment