Naibu
Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akionesha Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi kwa watendaji wa Wilaya ya Liwale (hawapo pichani), ambapo
utekelezaji wa miradi yote ya barabara hapa nchini umeanishwa humo
wakati alipowatembelea kuona hali ya mtandao wa barabara katika wilaya
hiyo, mkoani Lindi. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo Bi. Sara Chiwamba.
Mkuu
wa Wilaya ya Liwale mkoani Lindi, Bi. Sara Chiwamba akifafanua jambo
kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, kuhusu hali ya mtandao wa
barabara wilayani humo katika ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo,
mkoani humo kukagua miundombinu hiyo.
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya
Nachingwea Bi. Rukia Muwango kuhusu nia ya Serikali ya kuhakikisha
inafungua wilaya hiyo na wilaya jirani ya Liwale kwa kuwajengea barabara
kwa kiwango cha lami, mkoani Lindi.
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akisisitiza jambo kwa uongozi wa
Wilaya ya Ruangwa wakati alipofanya kikao nao wilayani hapo. Wa kwanza
kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo Bw. Joseph Mkirikiti.
Muonekano
wa sehemu ya barabara ya Ruangwa- Namichiga KM 22 ambapo Wakala wa
Barabara mkoa wa Lindi wamepewa jukumu la kuhakikisha inapitika wakati
wote.
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akitoa maelekezo kwa Mkandarasi
Mzawa kutoka Kampuni ya Southern Link, Mhandisi Felix Aminieli,
anayejenga Daraja la Nandanga lenye urefu wa mita 30 ambalo lipo katika
mto wa Lukuledi, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi. Kulia ni Mkuu wa Wilaya
hiyo, Bw.Joseph Mkirikiti.
Meneja
wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Lindi, Mhandisi Isaack
Mwanawima akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua za ujenzi wa
daraja la Nandanga lenye urefu wa mita 30 ambalo lipo katika mto wa
Lukuledi, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Muonekano
wa daraja la Nandanga ambalo lipo katika barabara ya Wilaya ya
Luchelegwa-Ndanda inayounganisha wilaya za Ruangwa mkoa wa Lindi na
Masasi mkoani Mtwara. Daraja hilo linatarajiwa kukamilika mwezi Novemba
mwaka huu.
Wananchi
wa wilaya ya Liwale na Nachingwea mkoani Lindi wameiomba Serikali
kuhakikisha inaanza ujenzi wa barabara ya Liwale - Nachingwea (Km 129)
kwa kiwango cha lami ili kutatua changamoto za usafirishaji wa abiria na
mazao katika wilaya hizo.
Akizungumza
kwa niaba ya wananchi hao mbele ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias
Kwandikwa, Mkuu wa wilaya ya Liwale Bi. Sarah Chiwamba amesema kuwa
wanachi wake wanaamini kuwa Liwale itafunguka kibiashara na kiuchumi
endapo itakuwa imeimarishwa katika mtandao wa barabara ambazo
zitaiunganisha wilaya hiyo na wilaya jirani pamoja na nchi kwa ujumla.
"Naamini
barabara hizi zikikamilika wilaya hii na mkoa wetu utaendelea kiuchumi
kwani suala la miundombinu ya barabara imekuwa ni kilio cha muda mrefu
katika wilaya yetu", amesema Mkuu wa Wilaya.
Aidha,
Bi. Sarah amefafanua kuwa wananchi wengi katika wilaya hiyo ni
wakulima, hivyo wamekuwa wakitumia miundombinu ya barabara kusafirisha
mazao ya korosho na ufuta yanayozalishwa kwa wingi kuelekea maeneo
mbalimbali ya nchi.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri huyo anayeshughulikia masuala ya Ujenzi,
amewataka wataalamu wote wa masuala ya ujenzi nchini kupitia Sera ya
Ujenzi ya mwaka 2003 ambayo itawasaidia kuwapa mwongozo katika
utekelezaji wa majukumu yao katika kutoa huduma bora kwa jamii.
Ameongeza
kwa wataalam wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kuwa
wabunifu katika ujenzi wa barabara zao ili kuondoa dhana potofu iliyopo
dhidi ya usimamizi wa barabara kati yao na Wakala wa Barabara Tanzania
(TANROADS).
"TANROADS
na TARURA shirikianeni katika kuhakikisha mnawajengea wananchi
miundombinu iliyobora, kusiwepo na utofauti kati ya barabara
mnazozisimamia", amesema Naibu Waziri huyo.
Ametoa
wito kwa uongozi wa TANROADS mkoani Lindi kuhakikisha kuwa wanaboresha
maeneo yote ya barabara ambayo ni korofi ili yaweze kupita kiurahisi
katika kipindi chote cha mwaka. Naye,
Meneja wa TANROADS mkoani Lindi, Mhandisi Isaack Mwanawima,
amemhakikisha Naibu Waziri Kwandikwa kuendelea na mpango wa matengenezo
ya barabara kwa kiwango cha lami ili kufungua fursa mbalimbali katika
mkoa huo.
Naibu
Waziri Kwandikwa yupo katika ziara ya kikazi mkoani Lindi kujionea hali
halisi ya mtandao wa barabara katika mkoa huo ambapo pamoja na mambo
mengine ametembelea na kukagua daraja la Nandanga lenye urefu wa mita 30
ambalo lipo kwenye mto Lukuledi katika barabara ya wilaya ya
Luchelegwa- Ndanda inayounganisha wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi na
Masasi mkoa wa Mtwara ili kujionea miundombinu yake.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment