HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA
KUSHIKILIWA NA KIKOSI KAZI MAALUM CHA
KUPAMBANA NA UJANGILI KWA MHIFADHI MWANDAMIZI GENES SHAYO.
Mhifadhi
Mwandamizi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Genes Shayo (60) anashikiliwa
na Kikosi Kazi Maalum cha kupambana na ujangili nchini kufuatia taarifa
za kuhusishwa kwake na upatikanaji wa jino la tembo wilayani Arumeru
mkoani Arusha.
Shirika
la Hifadhi za Taifa kupitia taratibu za utendaji kazi lilipokea taarifa
za kintelijensia tarehe 14.05.2016 zikimhusisha mwananchi mmoja mkazi
wa Ngarenanyuki, Arumeru Emmanuel Nassari (46) ambaye ni Mchungaji wa
Kanisa TAG kumiliki jino la tembo na kuwa alihitaji kupata mtu wa
kufanya naye biashara. Baaada ya kupata taarifa hizi shirika
liliwasiliana na Kikosi Kazi Maalum cha Kitaifa kinachohusika na masuala
ya ujangili ili kushirikiana kwa ajili ya ufuatiliaji.
Kikosi
Kazi hiki mara baada ya kupata taarifa hizi kiliendelea na taratibu zake
za kiuchunguzi na baada ya ufuatiliaji walifanikiwa kumkamata Emmanuel
Nassari tarehe 15.05.2016 akiwa na jino moja la tembo ambapo katika
mahojiano yaliyofanyika alimhusisha Mhifadhi Mwandamizi wa TANAPA Genes
Shayo kuwa anazo taarifa za yeye kuwa na jino hilo na hivyo kukamatwa
tarehe 16.05.2016 kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Shirika
la Hifadhi za Taifa linaendelea kutoa wito kwa raia wema wa nchi hii
kuendelea kutoa taarifa za kufichua vitendo vya ujangili na kwamba
halitasita kuchukua hatua stahiki kwa yeyote anayehusika na vitendo hivi
ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wake watakaobainika kisheria kuhusika na
vitendo hivi.
Imetolewa na Idara ya Mawasiliano
Hifadhi za Taifa Tanzania
S.L.P 3134
ARUSHA
Simu: +255 027 254 4082
Baruapepe: dg@tanzaniapaks.go.tz
Wavuti: www.tanzaniaparks.go.tz
No comments:
Post a Comment