Mkurugenzi
Mtendaji wa Chama cha Wahandisi Washauri Tanzania, Mhandisi Ray Ywa
Seng’enge (kushoto) akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi ya Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kabla ya kuanza kwa
kikao hicho.
Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akifafanua
jambo kwa ujumbe kutoka Chama cha Wahandisi Washauri Tanzania ofisini
kwake mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho.
Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akiwa katika
picha ya pamoja na ujumbe kutoka Chama cha Wahandisi Washauri Tanzania
uliomtembelea ofisini kwake.
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amewataka wawekezaji
nchini kujiamini na kuwekeza katika sekta za Nishati na Madini ili sekta
hizo zitoe mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Profesa
Muhongo aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika kikao chake na
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wahandisi Washauri Tanzania, Mhandisi
Ray Ywa Seng’enge aliyeambatana na ujumbe wake. Kikao hicho
kilishirikisha watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),
Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini
(TPDC), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Mamlaka ya Udhibiti wa
Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Wakala wa Ukaguzi wa Madini
Tanzania (TMAA).
Profesa
Muhongo alisema kuwa umefika wakati wa watanzania wenye uwezo katika
uwekezaji hususan katika uzalishaji na usambazaji wa umeme vijijini
kujitokeza na kuomba kazi kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na
kufanya kazi kwa ufanisi kwani uwezo wanao.
Alisema
kuwa wawekezaji wengi wamekuwa na mtizamo hasi kuwa makampuni ya kigeni
pekee ndiyo yenye uwezo wa kuzalisha na kusambaza umeme vijijini.
“Nataka
niwahakikishie kuwa kampuni za kitanzania zina uwezo mkubwa katika
uzalishaji na usambazaji wa umeme vijijini, na kama Serikali tupo tayari
kuwasaidia ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi zaidi,” alisema
Profesa Muhongo.
Aliendelea
kusema kuwa katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini ya REA awamu
ya pili, zipo kampuni za kitanzania zilizoonesha uwezo katika miradi ya
ujenzi wa miundombinu ya umeme vijijini.
Akielekea
mikakati ya Serikali ya kuwajengea uwezo wawekezaji wadogo wazawa
Profesa Muhongo alieleza kuwa kampuni za kitanzania zimeonekana
kujifunza kutokana na ushirikiano kati yao na kampuni za kigeni kwenye
miradi ya umeme.
Awali
akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha
Wahandisi Washauri Tanzania, Mhandisi Ray Ywa Seng’enge alimpongeza
Profesa Muhongo na kuelezea shughuli zinazofanywa na chama hicho.
Akielezea
mafanikio ya chama hicho Seng’enge alisema kuwa chama kimekuwa kikitoa
huduma Serikalini na makampuni binafsi ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo
yanayohusiana na masuala ya uhandisi.
Alisema
kuwa wakiwa na kampuni ya ushauri katika masuala ya uhandisi, wamekuwa
wakishirikiana na makampuni mengine yaliyopo nje ya nchi.
Akielezea
changamoto katika utendaji wa kampuni hiyo Seng’enge alisema kuwa
kampuni yao imekuwa ikitumiwa zaidi na makampuni yaliyopo nje ya nchi
katika utoaji wa huduma na kuiomba Serikali kuwasaidia na kuahidi kutoa
ushirikiano ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
No comments:
Post a Comment