Mkurugenzi Mtendaji Kamisheni ya
Maafa Zanzibar ndugu Ali Juma Hamad akifungua mafunzo ya waandishi wa
habari juu ya kujikinga na ugonjwa wa kipindupindu katika Ukumbi wa
gereji ya Wizara ya Afya Mombasa Mjini Zanzibar, (kulia) daktari dhamana
Kanda ya Unguja Dkt Fadhili Mohd na (kushoto) Mwakilishi wa WHO
Zanzibar Dkt. Ghirmay. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Washiriki wa mafunzo hayo
wakimsikiliza kwa makini Daktari dhamana Kanda ya Unguja Dkt. Fadhili
Mohamed alipokuwa akielezea njia za kukabiliana na kipindupindu katika
mafunzo ya siku moja yaliyofanyika Ukumbi wa Gereji ya Wizara ya Afya
Mombasa Mjini Zanzibar. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari
Maelezo Zanzibar Rafii Haji Mkame akiwasilisha mada ya wajibu wa
waandishi wa habari katika kukabiliana na maradhi ya miripuko katika
mafunzo yaliyofanyika Ukumbi wa Gereji ya Wizara ya Afya Mombasa Mjini
Zanzibar.
Katibu wa Jumuiya ya Maafisa wa Afya Zanzibar Ahmed Suleiman
Said akitoa elimu ya kupambana na maradhi ya kipindupindu kwa wananchi
wa shehia ya Shaurimoyo Mjini Zanzibar. Picha na Makame Mshenga-Maelezo
Zanzibar.
Baadhi ya wananchi wa shehia ya
Shaurimoyo Mjini Zanzibar wakifuatilia juu ya elimu ya ugonjwa wa
Kipindupindu iliyotolewa na Jumuiya ya Maafisa wa Afya Zanzibar.Picha na
Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
…………………………………………………………………………………………………………………….
Mwashungi Tahir – Maelezo Zanzibar.
Daktari dhamana kanda ya Unguja
Dkt. Fadhil Mohammed Abdallah amewataka wananchi kuchukua tahadhari
kuhusu maradhi ya kipindupindu ambayo kwa sasa ni tishio kubwa
Zanzibar.
Hayo ameyasema katika Ukumbi wa
Gereji ya Wizara ya Afya Mombasa kwenye mafunzo ya waandishi wa habari
juu ya kujikinga na ugonjwa huo ambao bado unaendelea katika sehemu
mbali mbali Zanzibar.
Amesisitiza kuchukuliwa
tahadhari zaidi kupambana na maradhi ya kipindu pindu ikiwemo kuweka
mazingira safi, kufuata masharti ya afya, kuchemsha maji ya kunywa
ama kutumia maji yaliyotiwa dawa ya kuulia bektiria wanaosababisha
maradhi hayo..
Dkt. Fadhil amewataka wananchi
kuacha tabia ya kula ovyo njiani, kukosha matunda na mboga mboga kabla
ya kula na kuchukua tahadhari kubwa wakati wa kumshughulikia maiti ya
maradhi ya kipindu pindu kwani ni miongoni mwa njia za maambukizi ya
maradhi hayo.
Amewataka waandishi wa habari
kutekeleza majuku yao ya kutoa elimu kwa wananchi ili wapate uelewa
mkubwa zaidi kukabiliana na maradhi hayo.
Amesema maradhi ya kipindu pindu
ingawa ni tishio kwa maisha ya wananchi lakini ni rahisi zaidi
kuyadhibiti kuliko maradhi mengine iwapo wananchi watafuata masharti ya
afya.
“Waandishi wa habari mnao
mchango mkubwa wa kutoa elimu kwa jamii katika kukabiliana na maradhi
ya kipindupindu hivyo tunategemea mashirikiano makubwa kutoka kwenu,”
alisisitiza Dkt. Fadhili
Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi
Mtendaji Kamisheni ya Maafa Zanzibar ndugu Ali Juma Hamad amesema
juhudi za pamoja zinahitajika katika kukabiliana na kipindupindu na
mchango wa kila mtu na taasisi unahitajika.
Amesema kumekuwa na changamoto
kubwa katika kukabiliana na maradhi hayo tokea yalipogundulika mwezi
Septemba mwaka jana ikiwa ni kipindi cha jua kali, kuchukua muda mrefu
na kusambaa sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba kinyume na watu
walivyozoea vipindi vya nyuma.
Akiwasilisha mada ya majukumu ya
vyombo vya Habari katika kudhibiti miripuko ya maradhi ya kuambukiza,
Mkurugenzi wa Idara y Habari Maelezo Zanzibar Rafii Haji Makame
amesema vyombo hiyo vinajukumu la lazima katika kusaidia umma kudhibiti
vifo na athari nyengine za kiuchumi na kijamii zinazosababishwa na
miripuko ya maradhi .
Katika kufanikisha majukumu hayo
Mkurugenzi Rafii ametaka kuongezwa ushirikiano kati ya vyombo vya habari
na sekta ya afya ili kupata taarifa sahihi kwa wakati katika kufikisha
ujumbe kwa umma.
Aidha amesema utoaji wa elimu ya
kudhibiti magonjwa ya kuambukiza kupitia vyombo vya habari liwe suala
endelevu ili jamii iweze kupata uwelewa na kubadilika kitabia.
Jumla ya kambi 18 zilifunguliwa
na kuhudumia wagonjwa 1066 Unguja na Pemba na kati yao wagonjwa 22
walifariki. Hivi sasa kuna kambi nne tu zinazoendelea kupokea wagonjwa
katika kisiwa cha Unguja.
Wakati huo huo Katibu wa Jumuiya
ya maafisa wa afya Zanzibar Ahmed Suleiman Saidi amewashauri wananchi
wa shehia ya Shaurimoyo kubadili tabia na kuweka mazingira wanayoishi
katika hali ya usafi ili kujikinga na kipindupindu.
Alitoa ushauri huo alipokuwa
akizungumza na wananchi wa shehia hiyo katika skuli ya Shaurimoyo
walipowatembelea kutoa taaluma juu yamaradhi hayo kwa vile shehia hiyo
ni miongozi kati ya shehia zilizoathirika na kipindupindu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment