KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemuapisha
Balozi Mhandisi John William Kijazi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.
Hafla
ya kuapishwa Balozi Kijazi imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo
Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mheshimiwa
Kassim Majaliwa, Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, Makatibu wakuu
na Naibu Katibu Wakuu.
Balozi
Kijazi ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi alikuwa
Balozi wa Tanzania nchini India, anachukua nafasi ya Balozi Ombeni Sefue
ambaye atapangiwa kazi nyingine.
Wakati huo huo, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameagana
na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi
(UNHCR) anayemaliza muda wake Bi. Joyce Mends-Cole Ikulu Jijini Dar es
Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine amemshukuru kwa kazi kubwa ya
kuhudumia wakimbizi kwa kipindi chote alichokuwepo hapa nchini.
Kwa
upande wake Bi. Joyce Mends-Cole amempongeza Rais Magufuli kwa kazi
nzuri inayofanywa na Tanzania kuzisaidia nchi zenye matatizo, hususani
migogoro ya kisiasa ambayo husababisha watu wake kuwa wakimbizi.
Pia
amepongeza kuteuliwa kwa Rais Mstaafu wa awamu ya Tatu Mheshimiwa
Benjamin William Mkapa, kusaidia usuluhishi wa mgogoro wa Burundi ambao
umesababisha idadi kubwa ya wakimbizi kukimbilia Tanzania.
Hata
hivyo amesema idadi ya wakimbizi wanaokimbilia Tanzania imepungua
kutoka wakimbizi 3,000 waliokuwa wakiingia hapa nchini kwa wiki, wakati
Mgogoro wa Burundi ulipoanza hadi kufikia wakimbizi takribani 1,000
wanaingia hapa nchini kwa wiki hivi sasa.
Aidha,
Bi. Joyce Mends-Cole amewashukuru Watanzania kwa ushirikiano alioupata
kwa kipindi cha miaka mitatu aliyofanya kazi hapa nchini, na ameahidi
kuwa Balozi wa kuitangaza vyema Tanzania.
Gerson Msigwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
07 Machi, 2016
No comments:
Post a Comment