Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akitoa taarifa ya siku 100 za kwanza za Serikali ya awamu ya tano.
TAARIFA YA SIKU 100 ZA KWANZA ZA SERIKALI YA
AWAMU YA TANO ILIYOTOLEWA NA
BALOZI OMBENI Y. SEFUE, KATIBU MKUU KIONGOZI,
IKULU, TAREHE 12 FEBRUARI, 2016
__________________________
Utangulizi
Serikali
ya awamu ya Tano imetimiza siku 100 tangu iingie madarakani tarehe 5 Novemba,
2015. Japo siku 100 ni chache sana kufanya tathmini ya kina, zinatosha kuonesha
muelekeo wa serikali na kupata kionjo cha uthabiti wa dhamira yake ya
kutekeleza ahadi zake kwa wananchi.
Kumekuwa na shauku kubwa ya wananchi
kujua kilichofanywa na Serikali hii katika siku zake 100 za mwanzo. Ni shauku
ya haki ambayo sisi katika Serikali hii lazima tujaribu tuwezavyo kuikidhi.
Ndio maana kuanzia juzi Mawaziri mbalimbali wanazungumzia mafanikio katika hizo
siku 100, kila mmoja akienda kwa undani kwenye sekta yake. Nawaomba wananchi
wafuatilie kwa karibu yale ambayo Mawaziri hawa wanayatolea taarifa kwenu ikiwa
ni sehemu ya uwajibikaji wao kwa wananchi.
Mimi pia, kwa nafasi yangu ya Katibu
Mkuu Kiongozi, ambaye ni Katibu wa Baraza la Mawaziri na Mkuu wa Utumishi wa
Umma, nimepokea maswali mengi ya waandishi wa habari na wananchi wengine kuhusu
siku 100 za kwanza za uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Maeneo yanayohusu sekta mbalimbali yatazungumzwa na Mawaziri wanaohusika.
Lakini nimeona baadhi ya maswali yanaweza kujibiwa tu na ofisi hii, yaani
Ikulu.
Nimeyaweka maswali hayo katika
makundi matano na nitayazungumzia kwa ujumla:
· Yapo maswali yanayohusu uongozi wa Rais wetu;
· Yapo maswali yanayohusu sifa binafsi za Rais wetu;
· Yapo maswali yanayohusu utendaji wake;
· Yapo maswali yanayohusu mahusiano yake na sekta binafsi kwenye utawala
wake; na
· Yapo maswali yanayohusu mwelekeo wake kwenye mambo ya nje na diplomasia
ya Tanzania.
Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano Ukoje?
Wahenga
walisema, “Nyota njema huonekana asubuhi.” Naam! Katika siku 100 za kwanza,
Rais Magufuli amethibitisha kwa uwazi zaidi kuwa yeye ni kiongozi bora na wa
kupigiwa mfano. Taarifa tunazoletewa na wananchi ni kuwa kwa kauli, matendo na
dhamira yake, wananchi wengi wamemwelewa, wamemkubali na wanamwamini. Katika
hizi siku 100, Rais amewathibitishia Watanzania kuwa yeye ni kiongozi, mwenye sifa muhimu za uongozi.
Sifa hizo ni pamoja na:
· Kiongozi bora lazima awe na dira, maono na malengo
kuhusu anakotaka Taifa liende. Katika siku 100 za kwanza Rais Magufuli
amedhihirisha kuwa ana sifa hiyo.
· Lakini dira bila mkakati ni ndoto. Kiongozi bora
lazima awe na mikakati ya kutekeleza dira na maono yake, pamoja na kufikia
malengo katika vipindi tofauti. Katika siku 100 za kwanza Rais Magufuli
amedhihirisha anayo sifa hiyo.
· Kiongozi bora lazima aheshimike na awe na mvuto wa
kuwafanya wananchi wamwamini, na kumfuata. Katika siku 100 za kwanza za utawala
wake, Rais amewafanya hata ambao hawakumpigia kura, wamwamini, wamwombee na kumfuata.
· Kiongozi bora anagawa majukumu, na haogopi kufanya
hivyo, lakini anafuatilia. Katika siku 100 za kwanza Rais Magufuli
amethibitisha kuwa anayo sifa hiyo.
· Kiongozi bora anajua na haogopi kuweka vipaumbele
na mpangilio wake wa utekelezaji na kuvisimamia. Katika hizi siku 100 Rais
Magufuli amethibitisha anayo sifa hiyo muhimu ya uongozi.
· Kiongozi bora haogopi kufanya maamuzi magumu.
Hakuna mwenye shaka kuwa katika hizi siku 100, Rais wetu amedhihirisha kwa
kauli na kwa vitendo kuwa, anapotetea maslahi ya Taifa na wananchi, haogopi
kufanya na kusimamia maamuzi magumu.
Rais ana Maono na Mikakati pevu ya kutimiza maono
yake
No comments:
Post a Comment