Jeshi la vijana
Watafuta Njia (PFC) wakionesha programu maalum katika sherehe ya kumuaga
Mch. Amosi Lutebekela (hayupo pichani) iliyofanyika katika kanisa la
waadventista wasabato Manzese jana.
Kwaya ya wasabato
ya Mbiu wakikabidhi zawadi ya kwaya kwa Mch. Amosi Lutebekela na Mkewe
kwenye sherehe ya kuwaaga iliyofanyika jana katika kanisa la wasabato
Manzese.
Kwaya ya
Wasabato Ruvu kitonga wakimtukuza Mungu kwa njia ya uimbaji wakati wa
sherehe ya kumuaga Mch. Amosi Lutebekela iliyoandaliwa na kanisa la
wasabato mtaa wa Manzese.
Kwaya
ya Angaza wakiimba wimbo maalum wa kumuaga Mch. Amosi Lutebekela kwenye
sherehe ya kumuaga iliyoandaliwa na kanisa la wasabato mtaa wa Manzese.
………………………………………………………………………………………………………………….
Na. Sarah Reuben
Mkurugenzi wa Sauti ya Unabii,
Uchapaji na Maeneo Mapya Mch. Amosi Lutebekela jana amekemea tabia mbaya
ya baadhi ya waumini wa kanisa la waadventista wasabato wanaoshindwa
kutimiza kiapo chao cha ndoa na kuanza kudai kuvunja ndoa kwa sababu
zisizokubalika kibiblia.
Akizungumza wakati wa ibada kuu
katika kanisa la waadventista wasabato Manzese, jijini Dar es Salaam,
Mch. Lutebekela alisema hivi karibuni idadi ya wanandoa ambao wanaomba
kuvunja ndoa inaongezeka tena kwa sababu zisizokubalika kibiblia.
“Mimi kama msajili wa ndoa
nimekuwa nikishughulikia changamoto mbalimbali za wanandoa ambao
wamekuwa wakiomba kuvunja ndoa kama suluhisho la migogoro yao. Ninakemea
wanandoa wote wenye malengo ya kuvunja ndoa kinyume na utaratibu wa
biblia. Tabia hiyo ikome mara moja kwa jina la Yesu, alisisitiza.
Katika hotuba yake vilevile Mch.
Lutebekela aliwataka vijana ambao hawajaingia katika ndoa kuzingatia
sifa za kiroho zaidi badala ya kutegemea mivuto ya kimwili yaani sura
nzuri na muonekano wa nje. “Ninapenda kuwaasa vijana wa kiume na wakike
epukeni sana kutafuta wenzi wa maisha kwa kuangalia mivuto ya nje yaani
sura na muonekano. Sura inachakaa lakini roho na tabia njema haitachakaa
hata umri wenu ukisonga, alifafanua Mch. Lutebekela.
Mch. Amosi Lutebekela aliyasema
hayo katika sherehe ya kumuaga rasmi iliyoandaliwa na Kanisa la
Waadventista Wasabato Mtaa wa Manzese baada ya kuteuliwa kuwa mkurugenzi
wa Sauti ya Unabii, Uchapaji na Injili katika maeneo mapya hivi
karibuni. Kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi, Mch. Lutebekela alikuwa
mchungaji anayesimamia Mtaa wa Manzese.
No comments:
Post a Comment