Mwandishi
wa habari mzoefu, Luqman Maloto akikitambulisha kitabu chake
kijulikanacho kwa jina la “The Special One 2015 Nani Ajaye?” wakati
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Mwandishi
wa habari mzoefu, Luqman Maloto akimkabidhi mwandishi wa habari wa
televisheni ya TBC, Angella Msangi kitabu chake kijulikanacho kwa jina
la “The Special One 2015 Nani Ajaye?”.
Mwandishi
wa habari mzoefu, Luqman Maloto akimkabidhi mwandishi wa habari wa
gazeti la Tanzania Daima, Tatu Mohamed kitabu chake kijulikanacho kwa
jina la “The Special One 2015 Nani Ajaye?”.
Mwandishi
wa habari mzoefu, Luqman Maloto akimkabidhi mwandishi wa habari wa
televisheni ya Azam, Temeluge Kasuga kitabu chake kijulikanacho kwa jina
la “The Special One 2015 Nani Ajaye?”
Na Mwandishi wetu
Mwanahabari
mzoefu nchini, Luqman Maloto amezindua kitabu kinachoelezea wasifu wa
wagombea Urais wa uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba kijulikanacho kwa jina
la ‘The Special One 2015 Nani Ajaye?’ ambacho kwa sasa kipo mitaani.
Akizungumza
jijini, Maloto amesema kuwa ameamua kuandika kitabu hicho kutokana na
kutambua wajibu wake na kutoa mchango kwa nchi yake kama raia hasa kwa
kutumia taaluma yake ya uandishi wa habari ili kuwawezesha wapiga kura
kumchagua kiongozi bora.
Maloto
alisema kuwa kitabu hicho kitawarahisishia wapiga kura kumchagua
kiongozi huku wakiwa na ufahamu wa kutosha kwani ameweza kuwachambua
wasifu wa viongozi ambao wamejitangaza au kutajwa kuwa mstari wa mbele
kukielekea kiti cha urais.
“Kwa
mujibu wa kalenda iliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
imebaki miezi mitano tu ili Watanzania kwa utashi wetu, tuweze kumchagua
Rais Ajaye, vilevile wabunge na madiwani wetu. Kwa kutambua umuhimu wa
uchaguzi na kwa kuona nami ninao wajibu wa kutoa mchango kwa nchi
yangu,” alisema Maloto.
Alisema
kuwa kusudio kubwa la kitabu “The Special One 2015 Nani Ajaye” ni
kumfanya Mtanzania kutambua kwamba tupo kwenye kipindi cha mabadiliko
kutokana na ukweli kuwa kwa sasa tunatoka kwenye maisha ya mazoea na
lengo la sasa ni kujenga nchi yetu katika misingi ya ukweli
unaojitosheleza.
“Lazima
kuondokana na kasumba ya kufanya uamuzi kama kuuziwa mbuzi kwenye
gunia. Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni dhamana kubwa sana,
hivyo lengo kuandika kitabu hiki ni kuwatambua japo kwa ukaribu wagombea
wanaotajwa, kuelekea kiti cha Urais katika Uchaguzi Mkuu 2015,”
alisema.
Alifafanua
kuwa Kitabu hiki kimegusa majina 25, miongoni mwao wapo waliojitangaza
kwa nia zao, wengine wanapendekezwa na wapo ambao wanatajwa chini kwa
chini. Wote wameandikwa ili wajulikane. Lengo ni kumsaidia Mtanzania
kufanya uamuzi sahihi.
Kwa
mujibu wa Maloto, kila jina limemulikwa katika pande mbili. Upande
uliojaa utukufu, upo ule wenye kasoro ambazo zinatambulika. Hili
limefanyika kwa ajili ya kutengeneza mzani wenye ulinganifu. Kitabu hiki
siyo jukwaa la kumsaidia mtu kisiasa, ila ni tochi la kuwaangazia
Watanzania kuwajua wale wenye uelekeo wa kushika hatamu ya uongozi mkuu
wa nchi yao.
Alisema
kuwa ni kitabu cha vyama vyote, majina ya wanaotajwa au kufikiriwa kuwa
mmoja wao anaweza kusimamishwa kugombea Urais 2015, katika ushirika wa
vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), yamechambuliwa.
Alisema
kuwa ameweza kuchambua majina manne yaliyochomoza katika Ukawa; Freeman
Aikaeli Mbowe, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, James Francis Mbatia na
Dk. Willibroad Peter Slaa, yamechambuliwa. Utafiti wa kuwatambua
wahusika umefanyika na utakachokisoma ndani ni uchambuzi baada ya
utafiti.
Pia
ameyachambua kwa kina majina 20 ya CCM yamechambuliwa baada ya utafiti.
Edward Ngoyai Lowassa, Dk. Asha-Rose Mtengeti Migiro, Profesa Mark James
Mwandosya, Stehen Masato Wasira, William Mganga Ngeleja, Lazaro Samuel
Nyalandu, Dk. Hamisi Andrea Kigwangalla, Zakhia Hamdan Meghji, Emmanuel
John Nchimbi na Fredrick Tluway Sumaye.
Wengine
ndani ya CCM ni Samuel John Sitta, January Yusuf Makamba, Anne Semamba
Makinda, Jaji Augustino Mathew Ramadhan, Charles Makongoro Nyerere,
Mwigulu Lameck Nchemba, Dk. Ali Mohamed Shein, Mizengo Peter Pinda, John
Pombe Magufuli na Bernard Kamillius Membe.
“Ni
imani kubwa kwamba miongoni mwao, ndiyo atapatikana Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, kwa hiyo vema kuwasoma na kuwaelewa, kwani
hatutarajii kupata Rais kutoka mbinguni kwamba Mungu atamteremsha,”
alisema.
Alisema
kuwa kitabu kimeonesha kwa upana kabisa kila mmoja na ubora wake. Kisha
udhaifu wake. Hii inamaanishwa kuwa hatwendi kumchagua malaika. Ni
binadam, kwa hiyo lazima kumuelekea yule mwenye afadhali, kwa maana
ubora wake unakuwa mkubwa kuliko udhaifu.
Maloto
alisema kuwa kila mwisho wa uchambuzi wa kila jina kuna hitimisho
ambalo linaweka ulinganifu kwa kutaka apimwe kwa mazuri yake na
kuoanisha kasoro alizonazo. Kwamba je, uzuri na ubaya upi unakuwa mkubwa
zaidi? Kwa maana hutampata asiye na kasoro. Huyo ambaye hana kasoro
utampataje?
Kitabu hiki kisaidie Watanzania kuwajua viongozi wao na kufanya uamuzi kwa uhakika na siyo kwa kubahatisha.
“Natumaini
kupata ushirikiano mzuri kutoka kwako, ili taarifa za kitabu hiki
ziweze kuwafikia watanzania, vivyo hivyo kiweze kusomwa na wengi na
kuwawezesha wapiga kura kumchangua mgombea wanayemjua,” alisema.
No comments:
Post a Comment