Mkwara
wa Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Fredrick Mwakalebela, umewafanya wafanyakazi
wa halmashauri ya wilaya hiyo kuhamia katika eneo lao la kazi kata ya Igwachanya
yalipo makao makuu ya wilaya hiyo, kutoka ofisi za halmashauri mama ya Njombe.
Hatua
imekuja baada ya hivi karibuni Mkuu huyo wa wilaya, kuandika waraka uliosomwa
katika baraza la madiwani wa halmashauri hiyo, ukiwataka watendaji wote wa
halmashauri hiyo kuhamia katika makao hayo, ili kusogeza huduma kwa wananchi
kama ilivyokuwa makusudi mazima ya serikali kuanzisha wilaya hiyo, na kwamba
watakaokaidi agizo hilo atachukua maamuzi magumu dhidi yao.
“Naagiza
watumishi wote wa halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe kuhamia Igwachanya ili
waweze kutekeleza majukumu yao
vyema ya kuwatumikia wananchi wa Wanging’ombe, atakayeshindwa kutekeleza agizo
hili nitachukua maamzi magumu dhidi yake,” alisema Mwakalebela katika waraka huo.
Kitendo
hicho cha mkuu wa wilaya kulivalia njuga suala hilo
kimewafanya watumishi hao kuhamia wilayani humo ili kuendelea na majukumu yao ya kulitumikia taifa.
Madiwani
wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe wakiongozwa na Mwenyekiti wa halmashauri
hiyo, Anthony Mahwata, walipongeza hatua hiyo ya mkuu wa wilaya, kwa kusema
kuwa kitendo hicho kimesaidia utekelezaji wa huduma za kijamii kwa wananchi kwa
sasa kwenda kasi, tofauti na awali wakati ambapo watumishi hao walikuwa
wakiishi mjini Njombe.
“Tunampongeza
sana mkuu wetu wa Wilaya Mwakalebela (Fredrick) kwa kuamru watumishi hawa
kuhamia katika makao makuu ya wilaya hapa Igwachanya, maana tukiangalia kwa
sasa huduma za kijamii zinaenda kwa kasi na miradi mbalimbali ya maendeleo
inasimamiwa kwa karibu zaidi, kwa kweli ni kiongozi bora,” alisema Mahwata.
Akizungumza
na gazeti hili, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, Emmanuel
Kilundo, alisema sababu zilizokuwa zikiwafanya watumishi hao wasihamie katika
makao makuu ya wilaya hiyo ni ukosefu wa miundombinu ya kufanyia kazi, ikiwemo
ofisi na nyumba za kuishi pamoja na madai ya uhamisho wao.
Alisema
kwa sasa wameamua kuhamia wilayani humo kutokana na agizo hilo
la mkuu wa wilaya, na baada serikali kuahidi kuwalipa madai yao hivi karibuni.
“Siyo
kwamba watumishi walikuwa hawataki kuhamia hapa Igwachanya ila kilichokuwa
kinakwamisha ni changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa miundombinu ya ofisi,
nyumba za kuishi na madai ya kuhamishwa, hata sasa hivi wamehamia hapa lakini bado
wanaidai serikali ingawa imeahidi itawalipa hivi karibuni,” alisema Kilundo.
Katika
hatua nyingine, Mwakalebela aliwaagiza wakandarasi wanaojenga ofisi na nyumba
za watumishi wilayani humo, kukamilisha haraka ujenzi huo kwa mujibu wa
mikataba, ili kuwawezesha watumishi wa wilaya hiyo, kuwa na ofisi bora za
kufanyia kazi pamoja na nyumba za kuishi.
Alisema
kukamilika kwa majengo hayo katika Kata ya Igwachanya, pia kutasaidia kuondoa
mvutano uliopo kuhusu makao makuu ya wilaya hiyo, kati ya Igwachanya
yalipotangazwa na kupitia gazeti la serikali na maeneo mengine ya kata za
Ilembula, Wanging’ombe na Mdandu yanayotajwa kwa sababu za kisiasa, na hivyo
kuwavuruga na kuwachanganya wananchi kutokufahamu ni wapi yalipo makao makuu
halali ya wilaya hiyo.
>>>>>>END.
No comments:
Post a Comment