Na Erasto Ching’oro -
Msemaji Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
Naibu Waziri wa Maendeleo
ya Jamii, Jinsia na Watoto Mhe. Pindi H. Chana akiwasilisha Taarifa ya Nchi
Kuhusu Hali ya Maendeleo ya Wanawake, Ulinzi na Maendeleo ya Watoto kwenye
Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliofanyika New York Marekani, tarehe
17/10/2014.
Naibu waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mhe. Pindi Chana (Mb.)amepongeza Bunge la
Katiba kwa kuzingatia haki za msingi za watoto katika mapendekezo ya Rasimu ya
Katiba ya nchi kwa kujumuisha Ibara Na. 53 (1) – (3) inayohusu haki za watoto
nchini.
Taarifa ya Sensa ya
Taifa ya Idadi ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, inaonyesha kuwa, Tanzania Bara
ilikuwa na watoto 21,866,258 wenye umri wa chini ya miaka 18 ambao ni sawa na
asilimia 51 ya watu wote. Hata hivyo kundi hili lina changamoto mbalimbali za upatikanaji
wa huduma za malezi, mkuzi na maendeleo ya mtoto.
Mhe. Pinda
ametanabaisha kuwa, kukosekana kwa huduma hizi husababisha vifo, ukatili,
ongezeko la watoto wa mazingira hatarishi, mmomonyoko wa maadili, unyanyapaa
kwa watoto wenye mahitaji maalum, ukeketaji, na ndoa za utotoni.
Kero hizi zinahitaji jitihada tahbiti
madhubuti ili kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi.
Mhe. Chana
anabainisha kuwa, kwa sasa suala la haki za watoto limezingatiwa katika rasimu
ya Katiba ya nchi inayopendekezwa, kwa kupatiwa sura kamili namba 53.
Lengo kuu
la Serikali likiwa ni kuhakikishwa kuwa haki za msingi za watoto zinatekelezwa
kikamilifu ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi, kulidwa, kuendelezwa,
kushirikishwa, na kutobaguliwa.
Kwa mujibu wa Ibara
Na. 53 (3) ya Rasimu ya Katiba, mtoto anatambuliwa kama mtu mwenye umri wa
chini ya miaka kumi na nane.
Akizungumza wakati akitoa majumuisho ya ziara yake
ya kutembelea vituo vya kulelea watoto, jijini Dar es salaam, Mhe. Pindi Chana
amepongeza Bunge la Katiba kwa kupendekeza Ibara Na. 53 ambayo inawataka wadau
wa haki za mtoto kuwa na mikakati
jumuishi itakayo hakikisha kuwa mtoto anapata jina, na uraia wa kusajiliwa.
Tafiti zinaonyesha
kuwa, kiasi cha asilimia 14 tu ya watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano
hapa nchini ndio waliokuwa wamesajiliwa na asilimia 6.2 ya watoto wote nchini
waliokuwa na vyeti vya kuzaliwa.
Kwa vile suala hili ni moja ya agenda ya
watoto, limeingizwa katika katiba ya nchi ili kuongeza uwajibikaji miongoni mwa
watoa huduma za ulinzi kwa ajili ya uimarishaji wa maslahi ya watoto ikiwemo
haki ya uraia na kuusajiliwa.
Pindi Chana ameongeza
kuwa ibara Na.53 (b) ya Katiba ya nchi imezingatia haki ya watoto kutoa mawazo
yao, kusikilizwa na kulindwa dhidi ya uonevu, ukatili, udhalilishaji, na
utumikishwaji na inapinga madhara yanayotokana na mila potofu.
Kundi hili ni
kubwa hivyo linahitaji uangalizi makini katika malezi, makuzi na maendeleo yao
ili hatimaye kuwa na raia wema walioandaliwa na kuwa na mchango thabiti katika
familia zao na taifa kwa ujumla.
Watoto na wananchi
kwa ujumla wanakumbushwa kutoa taarifa za vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa
watoto, ili wanaoendeleza uaktili dhidi ya watoto waweze kuchukuliwa hatua
stahiki. Taarifa hizo zinaweza kutolewa kupitia kwa maafisa wa madawati ya
jinsia, Namba maalum ya msaada wa mawasiliano kwa watoto na. 116, walinzi wa
amani walio karibu, wadau wa ulinzi wa watoto na Wizara yenye dhamana kwa
Watoto, na raia wenye mapenzi mema kwa watoto.
Wizara yenye dhamana kwa masuala
ya watoto itaendelea kuratibu utoajai wa elimu na uhamasishaji wa wadau
mbalimbali kuhakiksha kuwa jamii inashiriki kuwalinda watoto katika ngazi zote.
Rasimu ya Katiba
imependekeza kuhusu kuwawekea watoto mazingira bora ya kucheza na kupata elimu
ya msingi.
Serikali inatambua kuwa katika hatua za awali za mtoto, huduma za
uchangamshi wa awali na michezo ni
muhimu kwa ajili ya kujenga upeo wa uelewa wa mtoto.
Hili ni pamoja na
kujifunza, kuelekezwa mambo mbalimbali, kuimba, kucheza na kufanya mazoezi ya
vitendo vya uchangamshi. Katiba inazingatia kuwa, katika umri wa chini ya miaka
18 watoto wanahitaji kupatiwa elimu bora na kutambuliwa na kuendelezwa vipaji
vyao tangu hatua ya awali.
Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa
ushirikiano na wadau ili kuona kuwa maslahi ya watoto wanafikiwa katika
utimilifu wake.
Sura ya 53(e) ya
Rasimu ya Katiba inapendekeza mtoto kupata lishe bora, huduma ya afya, makazi
na mazingira yanayomjenga kimwili, kiakili na kimaadili.
Tafiti zinaonyesha
kuwa asilimia 58 tu ya kaya nchini ndizo zinauwezo wa kununua chakula na
asilimia 6 zinategemea msaada ili ziweze kupata chakula (USAID; 2011).
Hali hii
inaathiri upatikanaji wa lishe bora na hivyo kurudisha nyuma huduma ya malezi,
makuzi na maendeleo ya mtoto hususan katika umri wa miaka 0 - 8. Kuingizwa kwa
kifungu hiki kitatoa msukumo katika uzingatiaji wa lishe kwa watoto.
Mhe. Chana amefafanua
kuwa, Sura 53(e) inahimiza utoaji wa huduma ya afya kwa mtoto kwani haki ya
kuishi inaanza pale mama anapopata ujauzito.
Vile vile, kuishi kwa watoto baada
ya kuzaliwa kunategemea upatikanaji wa chakula cha kutosha, huduma bora za afya
na ulinzi katika kuhakikisha mtoto anakuwa na afya ya kutosha kumwezesha kukua
na kufikia ndoto zake.
Kupatikana kwa huduma hii katika mfumo jumuishi
kutamwezesha mtoto kuwa salama katika nyanja zote za malezi na makuzi yake.
Vile vile, kifungu
hicho kimeeleza kuhusu huduma ya makazi na mazingira yanayomjenga mtoto
kimwili, kiakili na kimaadili. Naibu Waziri Chana anasema kuwa, tatizo la
ukosefu wa maji na uchafu wa mazingira
lipo katika maeneo ya kuelea watoto, shule, na makazi yetu.
Hali hii
inakwamisha juhudi za taifa katika utoaji wa huduma za malezi, makuzi na
maendeleo ya mtoto.
Kuhusu ushiriki wa
watoto, Rasimu ya Katiba inapendekeza mtoto kushiriki katika shughuli
zinazolingana na umri alionao kama inavyoelezwa katika sehemu ya 53(e).
Wizara
ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inatambua kuwa maendeleo ya ukuaji wa
mtoto hutegemea ushiriki wake katika masuala yanayomuhusu na yale yanayohusu
jamii kwa ujumla.
Hali hii humwezesha mtoto kutoa mchango katika maamuzi
yanayohusu maendeleo yake na yale yanayo paswa kutekelezwa na jamii.
Hatua za ushiriki wa
mtoto zinaanzia umri wa miaka mitatu hadi anapokuwa mtu mzima ambapo aina ya
masuala anayopaswa kushirikishwa hutegemea umri wake.
Misingi hii ya ushiriki,
imeelekezwa katika mikataba ya kimataifa ya haki za watoto, katiba, sheria na
kanuni mbalimbali.
Wizara ya maendeleo ya jamii, Jinsia na Watoto imetoa
maelekezo ya kuundwa mabaraza ya watoto kama hatua moja ya kuimarisha ushiriki
wa watoto katika ngazi mbalimbali za kijamii.
Kwa kutambua hili, kuna umuhimu
mkubwa wa kuelimisha wazazi na jamii kukuza uelewa kuhusu ushirikishwaji wa
watoto katika masula mbalimbali ili kukuza maslahi ya watoto na viwango vya utoaji
huduma stahiki kwa watoto wetu.
Halikadharika,
kifungu 53(g) kinapendekeza mtoto kupata malezi na ulinzi kutoka kwa wazazi,
walezi, jamii au mamlaka ya nchi, bila ya ubaguzi wowote.
Ubaguzi ambao
umeripotiwa ni ule wa kijinsia ambao mtoto wa kike au wa kiume anabaguliwa na
wazazi au jamii; na ule unaotokana na hali ya ugongwa, ulemavu na uyatima.
Wizara na wadau wake wamekuwa wakielimisha jamii kuhusu madhara ya ubaguzi wa
watoto.
Hata hivyo bado kuna taarifa za watoto wanaowabaguliwa kwa sababu moja au
nyingine jambo ambalo Mhe. Pinda Chana analikemea vikali kwani lina madhara
makubwa kwa watoto kisaikolojia na kiakili.
Mhe. Pindi Chana
anahitimisha kwa kubainisha kuwa, mapendekezo ya Rasimu ya Katiba yameelekeza
kuwa, ni wajibu wa kila mzazi, mlezi, jamii na mamlaka ya nchi kuhakikisha kuwa
watoto wanalelewa katika maadili stahiki kwa umri wao.
Kama agizo hili
likifanyiwa kazi na kusimamiwa na walinzi wa watoto, tutapunguza kwa kiasi
kikubwa matukio ya uaktili kwa watoto na kuwa na taifa la watoto na vijana
makini walioandaliwa kubeba dhamana katika familia na taifa kwa ujumla.
Kimsingi, uwezo wa
taifa lolote lile kwa kiwango kikubwa unategemea ni kwa kiasi gani maslahi ya
watoto yamezingatiwa kwa kuwekeza katika malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto.
Kushindwa kutoa kipaumbele katika upatikanaji wa haki za watoto kutaongeza
athari mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa ukatili, vifo katika umri
mdogo, utoro shuleni, mimba za utotoni, watoto wanaoishi katika mazingira
hatarishi, ajira hatarishi na hivyo kuongeza gharama kwa familia na taifa letu.
Taifa ambalo limezingatia ulinzi na uwekezaji katika maslahi ya watoto linakuwa
taifa thabiti maana liliandaa mustakari wa watoto wake kwa wakati unaofaa.
Simu:
0715496900
No comments:
Post a Comment