Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Ernest Mangu -Na Francis Godwin
Moshi. Maofisa wa Polisi wapatao
120 wa Jeshi la Polisi, waliokuwa wakihudhuria mafunzo ya kupandishwa
vyeo katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi (MPA), wametimuliwa chuoni
hapo.
Vyanzo mbalimbali vililidokeza gazeti
hili kuwa, waliotimuliwa chuoni hapo ni maofisa ambao wana ulemavu wa
aina mbalimbali walioupata wakiwa wanatekeleza majukumu yao ya kazi.
Habari hizo zilisema hadi jana saa 9:00
alasiri, maofisa hao walikuwa ofisi za mkuu wa chuo hicho wakisubiri
kupatiwa maelekezo ya namna ya kurejea katika vituo vyao vya kazi mikoa
mbalimbali.
“Wako 120 hivi walikuja hapa (MPA) kwa
ajili ya kuchukua kozi za Koplo, Sajenti, Meja na ‘Assistant Inspector’
(wakaguzi wasaidizi), lakini ndiyo hivyo wametuambia tuondoke,”
kilidokeza chanzo chetu.
Hata hivyo, ofisa mmoja alilidokeza
gazeti hili kwamba mkuu wa zamani Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema,
ambaye amestaafu, ndiye wa kulaumiwa kwa kutoheshimu mapendekezo ya
wataalamu.
“Tulimwambia IGP Mwema kwamba ni vizuri
kama maofisa wenye ulemavu kama baadhi ya vigezo wanavyo basi wapewe
vyeo huko huko mikoani, lakini wasiende chuoni,” alidokeza na kuongeza;
“Tulipendekeza yafunguliwe madarasa ya
kanda wakishafanya mtihani wa kawaida wapewe vyeo huko huko, lakini
wakija chuoni ni lazima wahudhurie vipindi vyote ambavyo vinafanya chuo
kiitwe chuo.
“Chuo chochote kile kina vigezo vyake
na kwamba ili mtu apate cheo alichokwenda kukisomea ni lazima ahudhurie
asimilia 95 ya vipindi ikiwamo kwata, medani za kivita na kuzuia
vurugu,”alisema.
Chanzo kingine kililidokeza gazeti hili
kuwa maofisa hao waliripoti chuoni hapo wiki mbili zilizopita na katika
uchunguzi, walibainika wana ulemavu ambao hawawezi kumudu mafunzo ya
ukakamavu.
Mmoja wa maofisa hao waliotimuliwa
alilalamika kuwa kitendo hicho siyo cha kiungwana kwa kuwa ulemavu huo
waliupata wakiwa kazini wakilitumikia Taifa na hawajashindwa kuingia
darasani.
“Baadhi yetu tumefanya kazi miaka 20
wengine 25. Wamekatika miguu. Wako trafiki wamegongwa na polisi wengine
wamepigwa risasi na majambazi wakapata ulemavu si sawa kutunyima vyeo,”
alidai. (MWANANCHI)
No comments:
Post a Comment