Pages

CONTACT

0757092504/0678321772

Saturday, July 13, 2013

HALI YA AMANI: Mkapa ashtushwa CCM


Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa

RAIS mstaafu, Benjamin William Mkapa, ameonyesha wazi kutoridhishwa na mwenendo wa matukio ya uvunjifu wa amani hivi sasa.
 Mkapa, mmoja wa viongozi ambao wanajiamini katika kauli zao, amewataka Watanzania kutochoka kusali na kuiombea nchi ili amani iendelee kutawala. Alisema jukumu hilo linawahusisha watu, wakiwamo viongozi wa dini ambao wana dhamana kubwa kwa waumini wao.

Mkapa alitoa kuali hiyo jana mjini Mwanza, muda mfupi baada ya kuweka jiwe la msingi, katika jengo la ghorofa nne la Chuo Kikuu cha Sayansi, Tiba na Afya, kinachomilikiwa na Hospitali ya Bugando. “Watanzania tukitaka uchumi wetu ukue, lazima nchi iwe na amani, bila hali hiyo hakuna chochote kitakachofanyika.

"Ndugu zangu, nawaomba Watanzania wote kwa itikadi zao, tuwaombee viongozi wetu wa dini ili wawe na ushirikiano mzuri...na wao waliombee taifa hili, hii ni tunu tuliyopewa,” alisema Mkapa.

Pamoja na Mkapa kuzungumza kwa kifupi, alifichua siri nzito ambayo hajawahi kuitoa hadharani.

Siri hiyo, ni ile ambayo alidai wakati akiwa mdogo, wazazi walitaka asomee masomo ya upadri, lakini hakufanikiwa kufikia lengo hilo.

“Wazazi wangu walikuwa walitaka niwe padri, kwa bahati mbaya ndoto ya wazee wangu haikutimia,” alisema Mkapa.

Alisema yeye anatambua Mungu alimpangia kuongoza Watanzania, jambo ambalo lilitimia kwa kipindi cha miaka 10 ya kuliongoza taifa.

Habari zaidi zinasema, jana jioni alitarajiwa kuongoza harambee ya kukusanya Sh milioni 900, kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo la Chuo Kikuu cha Sayansi, Tiba na Afya, ambayo itahudhuriwa na watu mbalimbali.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Bugando, Profesa Jacob Mutabaji, alisema fedha zitakazopatikana zitasaidia kazi ya ujenzi wa majengo ambayo yamegharimu Sh milioni 400.

Alisema kama jengo hilo likikamilika, litapewa jina la Mwalimu Nyerere na litakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,400.

Juzi, Rais Jakaya Kikwete wakati akifunga kongamano la amani lililoandaliwa na Kituo cha Taasisi ya Demokrasia Tanzania (TCD), alikiri kuwapo na viashiria vya uvunjifu wa amani nchini.

Alisema katika siku za karibuni, kumeibuka viashiria vingi, vikiwamo vya watu kutangaza kuanzisha vikundi vya mgambo kwa ajili ya kujilinda.CHANZO CHA HABARI HII NI MTANZANIA

No comments:

Post a Comment