CHANZO CHADEMA BLOG
.................................................
MLIPUKO wa
bomu uliotokea wiki iliyopita katika mkutano wa kufunga kampeni za
udiwani kwa CHADEMA mkoani Arusha na kuua watu wanne, umeiweka kwenye
wakati mgumu serikali ya CCM, Jeshi la Polisi na Bunge.
Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, alisema juzi bomu lililolipuliwa katika mkutano wa
CHADEMA ni la kijeshi na limetengenezwa China na uzoefu unaonesha
hutumiwa na wanajeshi kujihami wakiwa katika makabiliano na maadui
vitani.
Wakati Pinda
akitoa kauli hiyo bungeni, viongozi wa CHADEMA wamelihusisha Jeshi la
Polisi na tukio hilo huku wakidai wanao ushahidi unaonesha askari
aliyevalia sare akilirusha kwenye mkutano huo.
Baadhi ya
wachambuzi wa masuala ya kijamii, wamelidokeza Tanzania Daima kuwa
kukiri kwa serikali kuwa bomu hilo limetengenezwa China, inapaswa iibane
nchi hiyo ieleze iliyemuuzia na alivyoliingiza nchini.
“Kwanini
isiundwe tume huru nchini ili nchi ya China iulizwe baada ya kutengeneza
bomu hilo ilimuuzia nani? Na kama haikuiuzia serikali, basi ni dhahiri
tuiulize China kwanini inafadhili vikundi vya kigaidi nchini kwetu?
“Je, kama
bomu lilitengenezwa China, tuangalie kama mkataba wa majukumu ya mataifa
duniani kuhusu silaha, nchi hiyo inatakiwa kutoka na kauli kuhusu bomu
hilo na kwa kukaa kimya maana yake wanakubaliana na maelezo ya
serikali,” alisema.
Wakati
maswali hayo yakionekana kuumiza vichwa vya watawala, viongozi wa
CHADEMA kwa upande wao wamegoma kutoa ushahidi walionao kwa Jeshi la
Polisi mpaka Rais Jakaya
Kikwete atakapounda tume ya kijaji itakayosikiliza ushahidi huo na kuendesha kesi hiyo.
Hali ya
mambo ikiwa hivyo, viongozi wa CCM na wabunge wameanza kulitumia Bunge
kukishambulia CHADEMA kuhusu mlipuko huo kwa lengo la kukinusuru chama
chao, Tanzania Daima limedokezwa mbinu hiyo.
Naibu Katibu
Mkuu (Bara), Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, juzi
bungeni walidai kuwa CHADEMA ndio wamekuwa wakihusika na vurugu zote
zinazohusisha mauaji nchini.
Kauli za
viongozi hao zinakuja takriban siku tano tangu Katibu wa Halmashauri Kuu
(NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye,
kudai CHADEMA kiliandaa na kuratibu shambulio hilo ambalo lilitokea
kwenye mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi wa madiwani.
Licha ya
Mwigulu kujadili jambo lililokuwa nje ya mjadala wa bajeti na
linaloendelea kuchunguzwa na Jeshi la Polisi, Spika wa Bunge, Anne
Makinda, alimwacha aendelee kukilaumu CHADEMA ikionekana ni mkakati
rasmi wa kulinasua Jeshi la Polisi na serikali ya CCM kwenye tuhuma
hizo.
Katika madai
yake, Mwigulu alianza kusema kuwa jambo la usalama wa nchi hii amekuwa
akiliongelea kwa haraka haraka, hivyo watu wamekuwa hawamwelewi.
“Leo naomba
nilisema kwa utaratibu, jambo la usalama nimekuwa nikilisema na kuomba
kama Elia aliyemwambia mtumishi wake kuwa anamwombea Mungu amfungue
macho ya kimungu ili aone jinsi yeye anavyoona.
“Jambo
limetokea kama hili la Arusha, nimeyaongea sana mambo haya na sasa hivi
ilipotokea mimi nitasema tena na wenzetu nikiwasema mara wanasema
wataenda jimboni. Nawashauri wasiende tu jimboni, bali wajenge kabisa
makao makuu ya chama chao,” alisema.
Mwigulu
ambaye alikuwa akishangiliwa na baadhi ya wabunge na baadhi ya mawaziri
akiwemo William Lukuvi, George Mkuchika, Ghasia, Mary Nagu na wengine
alisema anausema ukweli.
“Ni lazima
tuwaze tuvuke mipaka, kuna mambo yanawezekana kabisa yakawa yamejificha
pale. Watu wanaangalia, wanaojitoa ufahamu wanafikiria CCM inaweza
kushiriki.
“Mimi
niwaambie CCM, hata bila kushiriki, moja kwa moja inawekwa kwenye
lawama, jambo kama hilo likitokea.
Ila CCM haina ushiriki katika jambo
kama hili kwa sababu ndio watu wake kupitia serikali yake inatakiwa
kuwahakikishia usalama,” alisema.
Alisema kuwa
ni lazima waangalie maana wengine waliojaa ushabiki linapotokea jambo
wanakwenda moja kwa moja kuwa inawezekana CCM imeshiriki.
Mwigulu
aliongeza kuwa lazima yaangaliwe mazingira ya nchi kwa sasa, hasa
kipindi hiki ambapo wanakuja wageni wakubwa wakiwamo marais wa China na
Marekani, kwamba mataifa mengine ambayo yanajua ujio wa wageni ni
biashara, wanaweza kuichafua Tanzania.
“Sisi
tunakimbilia tu CCM ndiyo imejaa midomoni mwa watu, lakini hoja nyingine
Tanzania imekuwa kisiwa cha amani, hivi wale ambao hawatutakii mema
hamjajua eneo wanaloweza wakagusa?” alihoji.
Huku
akinukuu ripoti ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kuhusu utekwaji wa
Mwenyekiti wake, Absalom Kibanda, katibu huyo alidai CHADEMA imetajwa
kuwa ndiyo inahusika na matukio hayo ya utekeaji kwa kushirikiana na
maofisa usalama wasio waadilifu ili kuonesha kuwa CCM imeshindwa
kuongoza na sasa inaua watu wake.
“Niliwahi
kulisema hili kuwa kuna mambo mengine yanafanyika kwa hujuma na
tumeziona hizo hujuma lakini watu wengine wanawahi kuamini haraka.
“Lakini hawa
wenzetu kama waliwahi kumvalisha raia sare za jeshi na alihukumiwa,
wanashindwaje kila wakati wanasema polisi… polisi. Tunashindwaje kuamini
kama wanaweza kumvalisha mtu nguo za polisi na akafanya yale?” alihoji.
Mwigulu
alisema taarifa ya Polisi Mkoa wa Morogoro kuhusu tukio la kifo cha
kijana Ali Zona, kilichotokea wakati wa maandamano ya CHADEMA, zinasema
chama hicho ndicho kilihusika.
“Yule kijana
aliyeuawa Morogoro taarifa zilizopo hakuuawa na polisi, ni CHADEMA wao
wenyewe walitoka pale wakatengeneza ile vurugu wakamfyatulia risasi ili
kutengeneza kwamba serikali ya CCM inakandamiza wapinzani,” alisema.
Mwigulu
ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi aliongeza kuwa hata video ya
mauaji ya Arusha iliyowekwa kwenye mtando wa You tube inaonesha wazi
kuwa yalipangwa.
“Yule
aliyekuwa anachukua video eti hakushtushwa kabisa na lile bomu,
aliendelea kufuatilia kama vile ni mkanda wa harusi. Iliwahi kutokea
wapi mchukua video kwenye mkutano wa hadhara kitu ambacho hakikupangwa
kimelipuka, kinaua watu, yeye anendelea kama anachukua ‘sendoff’?”
alihoji.
Baada ya
Mwigulu kumaliza, Hawa Ghasia ambaye ni mjumbe wa NEC alipewa nafasi ya
kuchangia bajeti hiyo kwa kujibu hoja za baadhi ya wabunge, lakini naye
akatumia muda mwingi kuilaumu CHADEMA kwa matukio ya vurugu nchini.
Ghasia
alitumia muda huo kupanda mbegu ya ubaguzi wa kimaeneo akidai kuwa
CHADEMA wamechochea vurugu Mtwara, Mwanza, Mbeya, Morogoro na sasa
Arusha ili maeneo hayo yasipate maendeleo kama Mkoa wa Kilimanjaro
wanakotoka baadhi ya viongozi wa kitaifa wa chama hicho.
Ghasia
alisema wiki iliyopita alikuwa Kilimanjaro anakotokea Mbowe na
Ndesamburo, hakuona vurugu za kuchoma matairi wala kupigwa kwa mabomu
kama ilivyo Arusha.
“Jamani tuwe
macho na hawa CHADEMA hawataki wawekezaji waende mikoa mingine tofauti
na Kilimanjaro ndiyo maana wanahamasisha vurugu katika mikoa ya wenzao.
“Wanafanya
vurugu Arusha ili watalii wagome kwenda huko, wanataka watalii
wakimbilie Kilimanjaro.
Jamani tusiwakubalie hawa jamaa wataliingiza
taifa letu kubaya,” alisema.
Naye Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji alisema
kinachofanywa na CHADEMA mkoani Arusha na kwingineko kinaathiri
uwekezaji kwani wawekezaji watakimbilia nchi jirani.
Nagu alisema kutokuwapo kwa wabunge wa CHADEMA kumelifanya Bunge liwe tulivu tofauti na linavyokuwa wakiwapo wabunge hao.
Katika kile
kinachoonekana wabunge wa CCM walijipanga kikamilifu kukisulubu CHADEMA,
kilichokosa wawakilishi, Waziri asiye na wizara maalumu, Mark
Mwandosya, alitumia kauli mbalimbali za mafumbo kukinanga chama hicho
cha upinzani.
Mwandosya
alisema anaamini uchaguzi mkuu ujao, watu watachagua amani dhidi ya
vurugu, upendo dhidi ya chuki, amani dhidi ya vita huku kwenye siasa
watachagua vyama vinavyowaelekeza katika maendeleo na si vile
vinavyowaelekeza katika vurugu, migogoro na machafuko.
Kutokuwepo
kwa wabunge wa CHADEMA pia kumeonekana kunatoa nafuu ya mijadala ambapo
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema mijadala mbalimbali iliyofanyika
kwa siku nne imekwenda vizuri na Bunge limekuwa kama la zamani.
Wakati hali
ya mambo ikiwa si shwari ndani ya CCM, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo
wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, juzi aliwaambia waandishi wa habari
kuwa wanawasiliana na makachero wao kuangalia hatua za kisheria
wanazoweza kuwachukulia viongozi wa CHADEMA waliogoma kutoa ushahidi.
Alisema
maelezo ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kwa waandishi wa habari
aliozungumza nao hivi karibuni ni tofauti na yale waliyoyatoa polisi,
hivyo jeshi hilo litaangalia njia za kuuthibitishia umma kuwa tuhuma
dhidi yao si za kweli.
No comments:
Post a Comment