Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akiwaelekeza wakulima wa pamba
kijiji cha Msai wilayani Iramba, vipimo vya kati ya tuta na tuta, shimo
na shimo kwa kutumia kamba na vijiti ili waweze kupanda kitaalamu na
kuvuna kwa wingi.
Wakulima
wa pamba kijiji cha Msai wilayani Iramba, wakishiriki kwa vitendo
mafunzo yya kupima urefu kati ya tuta na tuta, shimo na shimo kwa
kutumia kamba na vijiti ili waweze kupanda kitaalamu na kuvuna kwa
wingi.
Katibu
Tawala Wilaya ya Iramba Pius Songoma akishiriki kuwaelekea wakulima wa
pamba kijiji cha Msai wilayani Iramba, vipimo vya kati ya tuta na tuta,
shimo na shimo kwa kutumia kamba na vijiti ili waweze kupanda kitaalamu
na kuvuna kwa wingi.
Konyo
Mjika ambaye ni mkulima hodari wa pamba wilaya ya Iramba kutoka kijiji
cha Msai akimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Singida kwa zawadi ya kilo tano za
mbegu ya pamba aliyopewa.
Zakaria
Marko Mwakilishi wa Kampuni ya Biosustain itakayosambaza mbegu za pamba
tani 300 mkoani Singida akizungumza na wakulima wa zao hilo Katika
kijiji cha Msai Wilayani Iramba.
……………
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya
Iramba Emmanuel Luhahula, asimamie kuvunjwa kwa bodi ya Ushirika wa
Kijiji cha Msai Wilayani Iramba ndani ya wiki mbili, kutokana na tuhuma
za ubadhirifu wa zaidi ya shilingi milioni 50.
Dkt
Nchimbi ametoa agizo hilo mwishoni mwa wiki alipokuwa katika mkutano na
wakulima wa Pamba wa Kijiji cha Msai, ambao wamemueleza kutokuwa na
imani na viongozi wa bodi hiyo kutokana na upotevu wa fedha hizo na
wakiwa hawajachukuliwa hatua yoyote.
Wakulima
hao wamemueleza Mkuu wa Mkoa kuwa fedha zaidi ya milioni 50 zilitolewa
na seikali kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la ghala la ushirika wa kijijini
hapo lakini hakukuwa na ujenzi wowote uliofanyika huku wakifuatilia
hawapewi majibu sahihi.
Wamesema
wana ushirika walijitahidi kutuma mwenyekiti wa Kijiji hicho kufuatilia
upotevu huo bila mafanikio jambo lililowakatisha tamaa ya kuendelea na
ushirika.
Dkt
Nchimbi amesema “moja ya Muhimili wa mafanikio ya kilimo cha pamba ni
ushirika ulio imara, tunakoelekea kwenye kilimo cha pamba chenye tija
hawa wasiowaaminifu kwenye bodi watatukwaza na kutukwamishwa, kama bodi
haifanyi kazi vizuri kwanini iendelee?, Mkuu wa Wilaya naimani kwa
utendaji wako mzuri hili halitachukua zaidi ya wiki mbili”.
Aidha
amemtaka Afisa Ushirika Mkoa wa Singida kusimamia na kutoa ushauri wa
kitaalamu wakati wa kuvunjwa kwa bodi hiyo kwakuwa kazi ya mkoa ni
kusuluhisha sio kutafuta maelezo marefu huku wananchi wanapotezewa muda.
“Afisa
Ushirika hakikisha tarehe ishirini mwezi huu bodi hiyo iwe imeivunjwe
na kuundwa bodi mpya ambayo itasimamia ushirika kwa umakini ili kuinua
kilimo cha pamba Iramba”, amesisitiza Dkt Nchimbi.
Aidha
Dkt Nchimbi amewatoa hofu wakulima kwakuwa mbegu aina ya UKM 08 za
manyoya pamoja na viuatilifu zitafika na kusambazwa kwa wakati huku
akiwataka kupanda kitaalamu ili kwa ekari moja iwe na miche elfu 22 na
mkulima avune zaidi ya kilo elfu moja za pamba.
Pia
amewaagiza maafisa ugani wote kulima pamba ili mashamba yao yawe
mashamba darasa, huku wakitakiwa kuhakikisha hakuna makosa katika hatua
yoyote kuanzia kwenye kuandaa mashamba, kupanda na kwenye upuliziaji
dawa, bila kusahau kutoa taarifa kwa wananchi katika kila hatua.
Dkt
Nchimbi amewapa wakulima wawili hodari wa zao la pamba zawadi ya kilo
tano kwa kila mmoja kama kianzio huku akiwaahidi kuwa mbegu za kutosha
na viuatilifu kwa ajili ya maeneo yao watapatiwa.
Akisistiza
kaulimbiu ya Singida mpya kwa pamba yenye tija amewataka Wanasiasa,
watendaji wa serikali na viongozi wa dini washirikiane na serikali kwa
pamoja katika kutoa hamasa na elimu ya kilimo cha pamba.
Dkt
Nchimbi ametoa onyo kwa wauza pembejeo na wasambaaji wasio waaminifu
ambao husambaza dawa zisizo halisi kuwa serikali itawabaini na kuwapa
adhabu kali huku akiwataka wakulima wasinunue dawa bila ushauri wa
maafisa ugani.
“Kuna
dawa nyingine ukipuliza kwenye wadudu waharibifu wa pamba badala ya kufa
wananenepeana, sasa ole wako serikali ikukamate wewe unayemuuzia
mwananchi dawa feki hakika tuakushughulikia ipasavyo”, amesisitiza Dkt
Nchimbi.
Kwa
upande wake Konyo Mjika ambaye ni mkulima hodari wa pamba wilaya ya
Iramba kutoka kijiji cha Msai amesema msimu wa mwaka jana amelima ekari
nane na kupata kilo elfu sita ambapo ameweza kujenga nyumba nne za bati,
kununua ng’ombe kadhaa na kuhudumia familia yake.
Mjika
ameongeza kuwa ameweza kuvuna pamba nyingi kutokana na kusikiliza
ushauri wa wataalamu wa kupanda kwa kufuata mistari, kuweka mbolea na
viuatilifu mapema.Kutokana
na mafanikio hayo Mkulima Mjika amesema kwa msimu huu anatarajia kulima
ekarini shirini pamoja na kuwashauri wanakijiji wenzake walime pamba
kwa wingi huku wakifuata ushauri wa wataalamu ili waweze kuvuna kwa
wingi.
Naye
Zakaria Marko Mwakilishi wa Kampuni ya Biosustain inayojihusiha na
kilimo cha zao la pamba kwa mkataba amesema kwa msimu huu kampuni hiyo
itasambaza mbegu za pamba tani 300 mkoani Singida.
Marko
ameongeza kuwa uzalishaji wa pamba mkoani Singida umekuwa mdogo
ukilinganisha na mahitaji ya kiwanda chao ambapo mwaka jana zilipatitana
kilo milioni 1 na mwaka huu zikaongezeka hadi kilo milioni 1.5 kutokana
na jitihada za wakuu wa wilaya, Mkuu wa Mkoa na viongozi mbalimbai.
Ameongeza
kuwa Kijiji cha msai chenye wakulima wa pamba zaidi ya mia tano
wameweza kuzalisha kilo laki tano huku wilaya ya Iramba yote ikizalisha
kilo laki nane na nusu kwa msimu wa mwaka jana na mategemeo yakiwa
makubwa zaidi kwa mwaka huu.
Marko
amesema kutokana na msukumo wa serikali na Viongozi wa Mkoa wa Singia ni
matarajio yake kiwanda cha Bio Sustain sasa kitazalisha kwa faida
kutokana na kupata pamba ya kutosha hapa Singida na sio kuifuata mikoa
ya jirani kama ilivyokuwa hapo awali.

No comments:
Post a Comment