Na. Aron Msigwa- DODOMA.
SERIKALI
imesema kuwa itaendelea kuboresha maslahi ya askari wa Jeshi la Polisi
na kuwajengea nyumba za kisasa za kuishi ili waweze kutekeleza majukumu
yao ipasavyo.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira
Mhe. Luhaga Mpina wakati akijibu maswali ya wabunge kuhusu mkakati wa
Serikali wa kuboresha maslahi ya Askari wa Jeshi hilo kwa niaba ya Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Bungeni mjini Dodoma leo
Amesema
kuwa Serikali katika mwaka wa fedha 2016/2017 itatekeleza Mpango
kabambe wa ujenzi wa nyumba za Polisi 4136 ambao utakwenda sambamba na
ujenzi wa vituo vya Polisi.
Amesema
Serikali imechukua hatua za haraka kulishughulikia suala la ukosefu wa
nyumba za askari hao katika maeneo mbalimbali nchini ili kuimarisha
ulinzi na usalama katika maeneo yenye ukosefu wa nyumba hizo.
Amelieleza
Bunge kuwa Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha
kuwa maslahi ya Askari Polisi yanaimarishwa ikiwemo malipo ya Posho ya
pango kwa askari wasio na nyumba ambayo ni asilimia 15 ya mishahara yao
ili waweze kulipia gharama hizo.
Ameongeza kuwa askari
wenye utalaam maalum wakiwemo madereva na madaktari wamekuwa wakilipwa
posho ya asilimia 15 ya mishahara yao na kuongeza kuwa askari
wanaoajiriwa katika ajira mpya kama madaktari wamekuwa wakilipwa
mishahara sawa na madaktari wengine bila kujali vyeo vyao.
“Serikali
tumefanya jitihada kubwa sana kuboresha maslahi ya askari wetu, kama
Serikali tumetoa posho za nyumba, posho za utalaam maalum kwa askari
wote ambayo ni asilimia 15 ya mshahara wa kila Polisi hii yote ni
kuwafanya askari wetu waweze kumudu gharama za maisha” Amesisitiza Mhe.
Mpina.
Ameeleza
kuwa kwa askari wanaofanya kazi katika mazingira magumu wakiwemo wa
Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wamekuwa wakipewa posho ya kufanya kazi
katika mazingira magumu (Hardship allowance) kiasi cha shilingi laki
moja (100,000) kila mwezi.
Mhe.
Mpina amebainisha kuwa askari wote wanaohitimu mafunzo yao wamekuwa
wakikatiwa Bima ya Afya kwa asilimia 100 na Serikali pamoja na udhamini
wa mikopo mbalimbali katika taasisi za kifedha ili waweze kupewa mikopo
na taasisi hizo.
Aidha,
amesisitiza kuwa serikali imewapandishia kiwango cha Posho ya katikati
ya mwezi (Ration Allowance) kutoka shilingi 180,000 za awali hadi
300,000 ambazo wanalipwa kwa sasa nchi nzima.
Katika
hatua nyingine Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imetoa
ufafanuzi kuhusu vijana wa kidato cha nne kutochukuliwa kujiunga na Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi amesema
kuwa hatua ya kuwachukua vijana wote wanaomaliza kidato cha nne kwa
sasa haiwezekani kutokana na uwezo mdogo wa kifedha wa Serikali.
Amesema
kuwa uwezo wa JKT kuchukua vijana wa kujitolea kwa sasa ni 5000 hadi
7000 kwa mwaka kulingana na bajeti inayotolewa na kuongeza kuwa mpango
wa Serikali ni kuendelea kutenga fedha na kujenga kambi zaidi za mafunzo
ili kuwawezesha vijana wengi kujiunga na mafunzo hayo kulingana na upatikanaji wa fedha.
Kwa
upande wa wahitimu wa kidato cha sita wanaotakiwa kujiunga na JKT kwa
mujibu wa Sheria Mhe. Mwinyi amesema Serikali imewachukua vijana 14,000
na inaendelea kujenga uwezo wa ndani wa kuchukua vijana wengi zaidi.
Amesema
Serikali inakusudia kujenga majengo ndani ya makambi ili kuwezesha
vijana wote wanaohitimu kidato cha sita kupitia JKT kabla ya kujiunga na
vyuo mbalimbali hapa nchini.
Aidha,
Amefafanua kuwa kwa wale wanaojiunga na JKT kwa kujitolea ambao idadi
yao inafikia 5000 sio wote wanaopata nafasi ya kuajiriwa katika vyombo
vya Ulinzi na Usalama na kuongeza kuwa ni asilimia 71 ndio hupata ajira
kwenye vyombo hivyo huku waliobaki wakilazimika kurudi nyumbani.
Amebainisha
kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu inaangalia utaratibu wa
kuwawezesha vijana hao ili wanaporudi uraiani waweze kupatiwa mitaji ya
kuwawezesha kujiajiri wenyewe.
Baadhi ya Mawaziri na Wabunge wakiwa ndani ya Ukumbi wa Bunge wakati wa kikao cha 34 mjini Dodoma.
Wanafunzi
wa Shule ya Msingi na Sekondari Moga iliyoko jijini Dar es salaam
wakifuatilia shughuli za kikao cha 34 cha Bunge mjini Dodoma. Wanafunzi
90 wa shule hiyo wamelitembelea Bunge hilio kujifunza namna
linavyoendeshwa.
Naibu
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia
Ackson akiongoza kikao cha 34 cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania leo mjini Dodoma.
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akifurahia
jambo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye
ndani ya Ukumbi wa Bunge kabla ya kuanza kwa kikao cha 34 cha Mkutano
wa 3 wa Bunge mjini Dodoma.
Naibu
Waziri wa Malisili na Utalii Mhe. Ramo Makani akijibu maswali ya
Wabunge yaliyoelekezwa kwenye wizara hiyo wakati wa kipindi cha Maswali
na majibu leo, Dodoma.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu
Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Muhagama akitoa ufafanuzi kuhusu masuala
mbalimbali ya utendaji wa Serikali ndani ya ukumbi wa Bunge leo mjini
Dodoma.
Waziri
wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akiwasilisha Bungeni Makadirio
ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa Fedha 2016/2017 leo
mjini Dodoma. Wizara hiyo inaliomba Bunge lipitishe kiasi cha shilingi
Trilioni 8.7 kwa ajiri ya matumizi ya kawaida na matumizi mengine.
Waziri
wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango (kushoto) na Naibu wake Dkt.
Ashatu Kijaji wakiandika maoni ya Wabunge waliokuwa wakichangia
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara Fedha na Mipango kwa mwaka wa
Fedha 2016/2017 leo mjini Dodoma.
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa(kulia)
akimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira
Mhe. Luhaga Mpina nje ya Ukumbi wa Bunge leo.
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa(kushoto)
akisalimiana na Mbunge wa Kilolo Mhe. Venance Mwamoto nje ya Ukumbi wa
Bunge, Dodoma.
Baadhi
ya Walimu na Wanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari Moga iliyoko
jijini Dar es salaam wakiwa katika picha ya pamoja nje ya Ukumbi wa
Bunge mara baada ya kutoka ndani ya ukumbi wa Bunge kufuatilia shughuli
za kikao cha 34.
Waziri
wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango (kushoto) akizungumza jambo na
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt.
Suzan Kolimba (kulia) kwenye viwanja vya Bunge, Dodoma.
No comments:
Post a Comment