Mgogoro mkubwa umeibuka katika
kijiji cha Kwa Ugolo wilayani Arumeru mkoani Arusha baada ya zaidi ya
wakazi 500 wa kijiji hicho kuvamia shamba la mwekezaji na kwa madai
shamba hilo ni mali yao halali.
Tukio hilo lilitokea juzi
wilayani humo ambapo wananchi hao walivamia shamba la kampuni ya
Flycathter lenye ukubwa wa ekari 106 na kisha kuanza kujigawia ardhi
huku wakisisitiza kwamba hawana mahali pa kwenda kulima.
Akizungumza katika eneo la
tukio mkazi wa eneo hilo,Eliakim Mollel alisema ya kwamba shamba hilo ni
halali yao kwa kuwa wamekuwa wakifanya shughuli nbalimbali kama kulima
na kuokota kuni kabla ya wawekezaji hao kulichukua.
Mollel,alisema kwamba kumekuwa
na mvutano mkubwa baina yao na wawekezaji hao kugombea shamba hilo kwa
kipindi kirefu jambo ambalo limepelekea mahusiano mabovu baina ya pande
mbili.
Baadhi ya wakazi wengine wa
eneo hilo kwa nyakati tofauti bila kutaja majina yao hadharani walisema
kwamba wameamua kuvamia na kugawana ardhi ndani ya shamba hilo kwa kuwa
wamekosa sehemu ya kulima na kukosa hata mlo mmoja kwa siku.
Wakazi hao walidai kwamba
wamevumilia kwa muda mrefu lakini serikali haitaki kuwakabidhi haki yao
na kusisitiza kwamba wamechoka kuvumilia na kuamua kuchukua hatua ya
kuvamia na kisha kugawana shamba hilo ili wafanye shughuli mbalimbali.
Akizungumzia tukio hilo meneja
wa shamba hilo aliyejitambulisha kwa jina la Aikbar alisema kuwa shamba
hilo ni mali yao kisheria na wanashangazwa na hatua ya wakazi hao
kuvamia na kisha kujigawia maeneo.
Alisema kwamba tayari
wameshatoa taarifa mbele ya jeshi la polisi huku akisisitiza kwamba
wamepata hasara ya kiasi cha zaidi ya sh,500 milioni baada ya wananchi
kuvamia na kisha kukata mazao pamoja na kuharibu mali mbalimbali
zilizopo ndani ya shamba hilo.
Kamanda wa jeshi la polisi
mkoani Arusha,Charles Mkumbo ameliambia gazeti hili kwamba jeshi lake
lina taarifa kuhusu tukio hilo na linaendelea kusimamia usalama wote na
kuwataka wananchi wa eneo hilo kufuata sheria,kanuni na taratibu endapo
wakitaka kudai haki yao bila kuleta uvunjifu wa amani.
No comments:
Post a Comment