Mbunge
wa jimbo la Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo (katikati) katika picha ya pamoja na baadhi ya wazee wa
jimbo la Musoma Vijijini mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa jimbo.
Mbunge
wa jimbo la Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo akizungumza na wananchi hawapo pichani wakati wa
mkutano wake na wananchi wa jimboni mwake.
Baadhi
ya wananchi wa Musoma Vijijini waliohudhuria mkutano wa Mbunge wa jimbo
hilo na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (hayupo
pichani)
Wananchi wa Musoma vijijini wametakiwa kuondokana na kilimo cha kizamani ili kujiongezea kipato.
Wito
huo umetolewa hivi karibuni katika kijiji cha Murangi Mkoani Mara, na
Mbunge wa jimbo hilo na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo katika mkutano wake na wananchi wa jimbo hilo.
Profesa
Muhongo alisema kuwa tayari mbegu za zao la alizeti zipatazo kilogramu
2,025 zimegawiwa kwa wakulima jimboni humo na huku zingine kilogramu
2,000 zitagawiwa ndani ya wiki hii. “Tumegundua kilimo cha pamba
hakifanyi vizuri hapa kwetu, sasa tunajaribu kilimo cha alizeti na tena
alizeti inachukua muda mfupi baada ya miezi mitatu unavuna.”Alimuagiza
Afisa Kilimo kusimamia upandaji wa mbegu hizo ili kuwe na tija na
vilevile kushirikiana na wakulima mara kwa mara.
Vilevile
Profesa Muhongo alisema kilimo kinachotarajiwa jimboni humo ni kilimo
cha kisasa na pia kitakuwa cha umwagiliaji wa kitaalamu ambao hautokuwa
na athari.Alisema alikwisha agiza wasaidizi wake jimboni humo kufanya
tathmini ili kubaini vijiji vingapi vinahitaji visima ili kuanza kwa
shughuli hiyo na kuongeza kwamba kilimo cha kisasa ndiyo ajira ya sasa
na hivyo atahakikisha wakulima jimboni humo wanafaidika na kilimo
husika.
Mbali
na hilo, Profesa Muhongo alibainisha kwamba amemkaribisha Profesa wa
Kilimo kutoka Dakawa ili kufanya utafiti zaidi ya kuwa na kilimo chenye
tija na vilevile kutoa mafunzo kwa wataalamu wa kilimo pamoja na
wakulima jimboni humo.Alisisitiza umuhimu wa uundaji wa vikundi ili iwe
rahisi kusaidiwa kuwa na kilimo chenye tija ikiwa ni pamoja na kupatiwa
vifaa maalum vya umwagiliaji. “Ninataka jimbo hili liwe ni jimbo la
mfano; wengine waige kwetu,” alisema.
Naye
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ambaye ni Diwani wa Kata
ya Mgango, Charles Magoma akizungumza wakati wa mkutano huo, alipongeza
juhudi zilizoonyeshwa na Profesa Muhongo katika kuliletea maendeleo
jimbo hilo.Alisema amejifunza kutoka kwa Profesa Muhongo kwamba kuwa na
uhusiano mzuri na watu ni jambo jema. “Nimejifunza kwa mbunge, kumbe
kuwa na mahusiano mazuri ni jambo jema kama tuonavyo hapa namna ambayo
ameweza kufanya mambo makubwa katika kipindi kifupi.”
Alimuahidi
Profesa Muhongo ushirikiano wa kutosha pamoja na kuhakikisha yote
aliyoagiza yanatekelezwa. Vilevile aliwasisitiza wananchi waliohudhuria
mkutano huo kumuombea Mungu Profesa Muhongo ili azidi kuliletea jimbo
hilo maendeleo endelevu.
No comments:
Post a Comment