MFANYABIASHARA wa jijini Dar es Salaam,
Brayan Kikoti ameonesha nia ya kuwania ubunge katika jimbo la Kilolo
linaloongozwa na Profesa Peter Msolla.
Akizungumza na wanahabari mjini Iringa
hivi karibuni, Kikoto anayesoma Diploma ya Juu ya Utatuzi wa Migogoro katika
Chuo cha Ustawi wa Jamii, jijini Dar es Salaam alisema atawania jimbo hilo
kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Endapo atapitishwa, alisema atahakikisha
wananchi wa jimbo hilo wanakabiliana na umasikini kwa kutumia ardhi nzuri
waliyonayo.
“Kilolo ina ardhi nzuri na hali ya hewa
nzuri. Inahitaji kiongozi atakayewasaidia wananchi wa jimbo hilo namna ya
kuitumia rasilimali hiyo kubadili maisha yao nay a Taifa kwa ujumla,” alisema.
Alisema wana Kilolo wanatakiwa kukaa upya
na kuangalia kwa kina namna walivyoteleza na kuigawa ardhi yao kwa wawekezaji
wa miti.
“Wapo baadhi ya wananchi waliouza ardhi
yao kwa bei chee kwa wawekezaji hao na leo wanatafuta vipande vya ardhi kwa
ajili ya shughuli zao zingine lakini hawapati; tutapitia upya makubaliano ya
uuzaji wa ardhi kwa wawekezaji hao ili tuone kama kulikuwa na udanganyifu tuweze
kuufanyia kazi kwa faida ya wananchi,” alisema.
Kikoti alisema ambaye pia ni Mwenyekiti
wa Wafanyabiashara wanaofanya biashara zao Machinga Complex jijini Dar es
Salaam amewahi kuwa msaidizi wa mbunge wa Wawi, Hamda Rashid alipokuwa Kiongozi
wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Ni mtoto wa nane kati ya tisa wa Mzee
Kikoti na Paulina Luhwago; alizaliwa katika kijiji cha Ng’ing’ula alikopata
elimu yake ya msingi kabla ya kujiunga na elimu ya sekondari katika shule ya
sekondari Udzungwa na baadaye kusoma kozi ya kompyuta jijini Nairobi.
Baada ya kumaliza kozi hiyo ya kompyuta,
Kikoti alijiunga na Chuo cha Ualimu Morogoro kabla hajajiunga kwa kozi nyingine ya Diploma ya
Kufundisha Watoto wadogo. Baada ya kuhitimu mafunzo hayo alijikita katika
biashara zikiwemo za Utalii anazoendelea nazo mpaka sasa.
No comments:
Post a Comment