Na Shaban Lupimo, Njombe.
Wakulima wa kata ya Utalingoro wilaya ya Njombe, wameanza
kunufaika na mfumo mpya wa serikali wa kutoa pembejeo za kilimo kupitia vyama
vya ushirika, baada ya kuanza kukopa pembejeo za kilimo kwa bei nafuu kupitia
chama chao cha kuweka na kukopa cha Twitangage Saccos.
Wakulima walisema hayo katika mkutano wa kuchagua uongozi
mpya wa Saccos hiyo na kueleza kuwa mfumo huo unawasaidia kuondoka na mfumo
uliokuwepo wa kutumia mawakala ambao ulikuwa unawayumbisha wakuma.
“Mfumo uliokuwa unatumiwa zamani na serikali wa mawakala
ulikuiwa unatuyumbisha sana wakulima kutokana na baadhi yao kuchakachua mbolea
lakini mfumo huu wa sasa unamjali mkulima na unamwezesha kupata mbolea anayohitaji
badala ya mfumo ulikuwepo ambapo mkulima alikuwa analazimishwa kuchukua hata
mbolea asiyohitaji,” alisema Senjawike.
Rose Kitalima alisema: “Saccos yetu inatusaidia sana
kuondokana na adha ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo, kwa sababu ilifikia mahali
paka wafanyabiashara wakawa wanachakachua mbolea wanatuuzia mchanga wa
kutengenezea simenti wakitudanganya ni mbolea ya DAP, lakini kupitia mfumo huu
hatutegemei kupata hasara kama hiyo.”
Mwenyekiti wa bodi ya Saccos hiyo, Markus Ngole alisema
mwanachama anaweza kupata pembejeo za kilimo kwa kununua moja kwa moja au kwa kukopeshwa kwa riba nafuu na kwamba
hata wakulima wengine walioko katika kata hiyo wateweza kununua pembejeo hizo
kupitia bajrti hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya mikopo wa Saccos hiyo
Erasto Mpete alisema mfumo huo ni suluhisho pekee la kuondokana na malalamiko
waliyokuwa nayo wakulima ya kupata
pembejeo za ruzuku, hasa ya kupinga kupewa mbolea kwa kulazimishwa kuchukua
mbolea ya minjingu amabayo walikuwa hawaitaki kutokana na kutotoa matokeo
mazuri ya mazao.
Alisema katika Saccos yao wanachama 400 watanufaika na mfumo
huo huku wakitarajia idadi hiyo kuongezeka kutoka kwa wakulima wengine
wasiokuwa wanachama wa Saccos hiyo kutaka kupata pembejeo hizo kupitia Saccos
yao.
Alisema kupitia mfumo huo mwanachama ataweza kununua au
kukupa mbolea kwa asilimi mbili huku ada ya kiingilio ikiondolewa ili
kuwawezesha wakulima kulima mazao ya kutosha na kupiga hatua kiuchumi, ambapo
atarejesha mkopo huo kwa amu mbili kwa mwaka mwezi Novemba wakati wa mauzo ya
mahindi na mwezi machi wakati wa mauzo ya viazi mviringo.
Katika uchaguzi wa Saccos hiyo Ngole aliendelea kushilikilia
kiti cha wenyekiti kwa kupata kura 65, makamu Mwenyekiti ni Richard na nafasi
ya Mwenyekiti wa mikopo ikiendelea kuchukuliwa Erasto Mpete kwa kura 47.
No comments:
Post a Comment