Frank Nyalusi, Mwenyekiti wa Chadema Iringa Mjini |
CHAMA
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jimbo la Iringa Mjini jana limeshindwa
kufanya maandamano ya amani kama ilivyotangazwa kwa kile kilichoelezwa na
Mwenyekiti wake, Frank Nyalusi “tumepokea zuio kali kutoka jeshi la Polisi.”
Akizungumza
na habarileo jana, Nyalusi alisema walitoa taarifa kwa jeshi hilo siku mbili
zilizopita wakielezea nia yao ya kufanya maandamano hayo ikiwa ni kuitikia wito
uliotangazwa na Mwenyekiti wao wa Taifa, Freeman Mbowe wa kufanya maandamano ya
amani yasio na ukomo yenye lengo la kushinikiza kusitishwa kwa Bunge la Katiba.
Alisema
pamoja na jeshi hilo kuwazuia kufanya maandamano hayo, jana hiyo hiyo waliruhusiwa
kufanya mkutano wa hadhara uliotarajiwa kufanyika mtaa wenye machinga wengi
maarufu kama magari mabovu, Kitanzini.
“Kwahiyo
tutakuwa na mkutano wa hadhara utakaohutubiwa na mimi mwenyewe na viongozi
wengine wa chama kuanzia saa 10 jioni, hivisasa tupo kwenye kikao cha kamati
tendaji kuweka maazimio kuhusu zuio la maandamano hayo ya amani” alisema kwa
njia ya simu.
Akieleza
kushangazwa na maamuzi ya Polisi ya kuzuia maandamano yao, Nyalusi alisema maazimio
yatakayofikiwa katika kikao hicho atayatangaza kwenye mkutano huo.
Wakati
Chadema wakidai kudhibitiwa kufanya maandamano hayo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa
wa Iringa, Ramadhani Mungi alisema jeshi hilo halijapokea barua yoyote kutoka
katika chama hicho inayoonesha wameomba kufanya maandamano hayo.
Akitoa
ufafanuzi huo kwa njia ya simu, Mungi alisema “nchi hii kama zilivyo nchi
nyingine inaendeshwa kwa sheria, taratibu na kanuni.”
Alisema
watanzania bila kujali wanatoka kundi gani ni lazima wafanye mambo wanayotaka
kufanya kwa kuzingatia sheria vinginevyo mkono wa sheria utawafukuzia.
Alisema
mji wa Iringa upo shwari na kwamba jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu
kukabiliana na hali yoyote ile itakayoonekana inataka kuhatarisha amani.
No comments:
Post a Comment