WANANCHI wa kata ya Magamba Wilaya ya Chunya
Mkoani hapa wameikataa taarifa ya mapato na matumizi iliyosomwa na Diwani wa
kata hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Wilaya na
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Mwenyekiti huyo Kapala Chakupewa,alipatwa na
mkasa huo hivi karibuni alipokuwa akiwasomea wananchi mapato na matumizi ya
kata hiyo kutokana na utaratibu wa Serikali unaotaka wananchi kujua matumizi ya
fedha walizochanga kwa ajili ya matumizi ya shughuli za maendeleo.
Taarifa iliyokataliwa na wananchi hiyo ilikuwa ni
taarifa ya miezi sita(6) iliyokuwa inahusu mradi wa ujenzi wa kituo cha afya
cha kata hiyo kutokana na mchango wa wakazi hao ulioanza kuchangishwa tangu
mwaka 2007 na kufikia jumla ya Shilingi Milioni 7.
Sababu za wananchi hao kukataa taarifa hiyo ni
kutokana na kile walichodai kuwa fedha hizo hazijafanya kazi yoyote ambapo
Mwenyekiti huyo alisoma kama fedha hizo zimetumika hali iliyosababisha wananchi
hao kuhoji eneo walilotumia fedha hizo ambapo baadaye Mwenyekiti huyo
alibatilisha kauli yake kuwa hazijatumika.
Aidha wananchi hao wameendelea kuhoji kuwa ni kwa
nini fedha za umma zitunzwe mikononi mwa watu binafsi badala ya kutunza katika
taasisi za fedha pamoja na kutoanza kwa ujenzi huo kwa zaidi ya miaka Mitano
tangu waanze kuchangishwa fedha hizo.
Hata hivyo kutokana na kutoridhika na mwenendo wa
matumizi ya fedha hizo wananchi hao kwa ujumla wao waliamua kuwa ujenzi wa
kituo cha afya usitishwe na fedha zilizochangwa zirejeshwe kwa kila kijiji
kulingana na michango yao.
Akijibu tuhuma hizo katika Mkutano wa hadhara
uliofanyika katika kijiji cha Magamba, Mwenyekiti huyo Kapala Chakupewa,
amesema sababu za kutoanza kwa ujenzi huo kwa wakati ni
kutokana na Halmashauri ya Wilaya ya Chunya kutotoa Gari la kusombea mawe kama
walivyokuwa wameahidi awali.
Amesema baada ya kuomba gari kwa mkurugenzi
aliambiwa gari hilo ni bovu hivyo halitaweza kufanya kazi ya kusomba mawe ndiyo
maana ikamlazimu kuahirisha zoezi la ujenzi wa kituo cha afya hadi gari
litakapopatikana lenye uwezo wa kufanya kazi.
Pia Mwenyekiti huyo amekiri kuwa Kaimu Ofisa
Mtendaji wa Kata hiyo Festo Pandisha kuwa anadaiwa zaidi ya Shilingi Laki nne
(400,000/=) ambazo alichangisha kutoka kwa wananchi kwa ajili ya ujenzi wa
Shule lakini Mtendaji huyo alisema hajui zilipo licha ya kukiri kuzipokea
kutoka kwa wananchi.
Aidha pia Mtendaji huyo aliahidi kuzirejesha
fedha hizo kwa kununua saruji yenye thamani ya Shilingi laki nne kwa ajili ya
ujenzi wa shule lakini hajafanya hivyo hadi siku taarifa ya fedha inasomwa hadi
wananchi kuikataa.
Kutokana na kauli za Mwenyekiti huyo kuonekana
kumtetea Mtendaji na kudidimiza maendeleo ya kata, Wananchi wameamua taarifa
hiyo ikaandaliwe upya ili isomwe wiki ijayo na fedha zote zirudishwe kwa ajili
ya matumizi mengine ambayo wananchi wenyewe wataamua.
Wamesema endapo fedha hizo na taarifa
hazitaandaliwa upya na kwa usahihi basi watapeleka malalamiko yao kwenye ngazi
za kisheria ili hatua zingine ziweze kuchukua mkondo wake ikiwa ni pamoja
na Mwenyekiti na Mtendaji kuwajibishwa kwa ubadhilifu na uzembe.
Hata
hivyo kutokana na mienendo hiyo uchunguzi uchunguzi wa Mbeya yetu
umebaini kuwa usimamizi mbovu wa michango ya fedha za wananchi
unatokana na vijiji vinavyounda kata hiyo kutokuwa na Watendaji
hali inayosababisha watu binafsi kukamishwa nyadhifa hizo na kuchangisha
michango kisha kutokomea nayo.
Kata hiyo inayoundwa na vijiji vtatu ambavyo ni
Kijiji cha Magamba, Songambele na Nahalyongo vyote vikiwa vinasimamiwana
makaimu Maofisa watendaji kutokana na kutokuwa na Maofisa wa moja kwa moja
waliojariwa na Serikali kushika nafasi hizo.
Aidha kutokana na kukosekana kwa maendeleo katika
baadhi ya vijiji umetokana na usimamizi mbovu wa fedha zinazochangwa na
wananchi wenye hali ngumu ya maisha licha ya wakazi hao kupenda kufanya
shughuli za maendeleo.
Pia baadhi ya wahusika na wasimamizi wa miradi
ndani ya vijiji wameshindwa kufafanua na kuelezea namna ya kukomesha hali hiyo
inayorudisha nyuma juhudi za wananchi.
|
No comments:
Post a Comment