Spika wa Bunge Mhe Job Ndugai
akizungumza na Viongozi wa Kamati Tendaji ya Skauti waliomtembelea
Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam mapema leo. Wa pili kushoto kwake ni
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Tenkonolojia Mhe Eng. Stella Manyanya
(Mb) na anayefutia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya Skauti
Tanzania Balozi Nicholas Kuhanga.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi
na Tenkonolojia Mhe Eng. Stella Manyanya (Mb) aliyeambatana na Viongozi
wa Kamati Tendaji ya Skauti Tanzania akimueleza jambo Spika wa Bunge Mhe
Job Ndugai wakati walipotembelea Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya
Skauti Tanzania Balozi Nicholas Kuhanga akimueleza jambo Spika wa Bunge
Mhe Job Ndugai wakati walipomtembelea ofisini kwake Jijini Dar es
Salaam.
Spika wa Bunge Mhe Job Ndugai
(aliyekaa kulia) na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Tenkonolojia Mhe
Eng. Stella Manyanya (Mb) katika picha ya pamoja na Viongozi wa Kamati
Tendaji ya Skauti Tanzania mara baada ya kuzungumza nao Ofisini kwake
Jijini Dar es Salaam.
Picha na Ofisi ya Bunge
Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe Job Ndugai amewaahidi Viongozi wa Chama cha
Skauti Tanzania ushirikiano katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za
chama hicho ikiwemo maadhimisho ya Siku ya Skauti Afrika na Maadhimisho
ya miaka mia moja ya Skauti hapa nchini.
Mhe Spika aliyasema hayo wakati
alipokutana na kuzungumza na Viongozi wa Kamati ya Utendaji ya Skauti
Tanzania Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam ambao walimuomba awaunge
mkono katika shughuli zao.
Spika Ndugai aliwaeleza Viongozi
hao kwamba kwa niaba ya Wabunge wote ameupokea ujumbe huo na atajitahidi
sana katika kuhufikisha kwa Waheshimiwa Wabunge.
“Ninawashukuru sana kwa ujumbe huu
na niwaahidi kwamba tupo pamoja si katika hili tu bali katika mambo
yoyote ambayo mtakuwa mkiyafanya na nawaahidi pia ushiriki wa
Waheshimiwa Wabunge katika maadhimkisho hayo,” alisema Mhe Spika.
Awali akimuelezea Mhe Spika
kuhusiana na Shughuli mbalimbali za Skauti hapa nchini Naibu Waziri wa
Elimu, Sayansi na Tenkonolojia Mhe Stella Manyanya ambaye aliambatana na
Viongozi hao wa Skauti alisema pamoja na majukumu mengine Chama hicho
cha Skauti kina kazi kubwa ya kuandaa maadhimisho ya Siku ya Skauti
Dunia na Maadhimisho ya miaka mia moja ya Skauti hapa nchini.
Mhe Manyanya alisema kuwa
maandalizi ya Maadhimisho ya siku Skauti Afrika ambayo yanatarajiwa
kufanyika tarehe 8 hadi 11 Machi mwaka huu mkoani Arusha yanaendelea
vizuri ingawa kuna changamoto kubwa ya kifedha katika maandalizi ya
maadhimisho ya miaka mia moja ya Skauti hapa nchini ambayo yanatarajiwa
kufanyika kuanzia Juni hadi Julai Mkoani Dodoma.
“Mhe Spika kumekuwa na jitihada
mbalimbali za kufanikisha maadhimisho haya lakini kumekuwa na changamoto
katika kufikia malengo na ndio maana tumefikana hapa ili kukuomba
utuunge mkono” alisema Mhe Manyanya.
Mhe Manyanya aliongeza kuwa Wizara
imendelea kutambaua kazi kubwa ambayo Chama cha Skauti inafanya katika
kuendelea kuhimiza nidhamu miongoni mwa Vijana na kuwajengea moyo wa
kujitolea.
“Chama hiki Mhe Spika kimekuwa
kikiendelea kufanya kazi kubwa katika kuwajengea Vijana wetu moyo wa
kujitolea na kwa sasa tunataka kazi zao zifanyike kwa nguvu zaidi
tofauti na hapo mwanzo”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Kamati ya Utendaji ya Skauti Tanzania Balozi Nicholas Kuhanga alisema
anathamini sana mchango wa Mhe Spika na kwamba anashukuru kwa kauli yake
ya kuwaunga mkono.
Balozi Kuhanga aliongeza kuwa kwa sasa Uongozi wake unajipanga katika kuhakikisha kuwa Skauti inazidi kukua hapa nchini.
“Mhe Spika nia ni kuona Vijana wa
Shule za Msingi hadi Chuo Kikuu wanaingia katika Skauti na hivyo
tunataka twende mbele zaidi ya hapa tulipo kwa sasa,” alisema Balozi
Kuhanga.
No comments:
Post a Comment