Mwenyekiti wa Bodi ya Parole nchini Dkt. Augustine
Mrema (kulia) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati
alipokutana nao mapema hii leo jijini Dar es Salaam na kuwaeleza umuhimu vyombo
vya usimamizi wa sheria nchini kutoa adhabu mbadala ya kifungo cha nje kwa
wahanga wa matumizi ya dawa za kulevya nchini ikiwa ni sehemu ya barua yake kwa
Rais John Magufuli.
Na
Eliphace Marwa-MAELEZO
Dar
es Salaam
MWENYEKITI wa Bodi ya Taifa ya
Misamaha kwa Wafungwa (Parole) Dkt. Augustine Mrema amevitaka vyombo vya
usimamizi wa sheria nchini kutoa adhabu mbadala ya kifungo cha nje kwa wahanga
wa matumizi ya dawa za kulevya nchini.
Hatua hiyo inaeelezwa
itawezesha kuwapatia huduma bora za matibabu ambazo ni ngumu kuzipata pindi
wawapo mahabusu au wakitumikia kifungo katika magereza.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo Jijini Dar es Salaam, Mrema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha
Tanzania Labour Party (TLP) alisema katika siku za hivi karibuni kumezuga tabia
kwa baadhi ya askari polisi kuwageuza mtaji wahanga wa madawa ya kulevya.
“Natoa wito kwa Jeshi la Polisi
kuacha mara moja tabia ya kuwabambikia kesi wahanga hawa na badala yake
washughulike na wakubwa wa wauza madawa hayo ambao wapo katika jamii na
wanafahamika na hata baadhi ya Polisi” alisema Dkt. Mrema
Aidha Mrema alisema idadi ya
watumiaji wa madawa ya kulevya imekuwa ikiongezeka kila kukicha nchini hatua
inayoisababisha Serikali kuwa mzigo mkubwa katika kuwahudumia ikilinganisha na
mahitaji yaliyopo.
Katika barua yake
aliyoiwasilisha kwa Rais, Dkt Mrema alisema wahanga hao wamekuwa wakikabiliwa
na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa vituo vya tiba, kutengwa na kukamatwa
mara kwa mara na polisi.
Kwa mujibu wa Mrema alisema
ndani ya barua hiyo pia amemshauri Rais John Magufuli kuwasaidia wahanga hao
kupata maeneo maalum ya mashamba kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo ili
makundi hayo yaweze kujiongezea kipato.
Dkt Mrema pia aliishauri
Serikali kuwapa wahanga hao jukumu la kusafisha Jiji la Dar es Salaam na kuwa
walinzi wa wachafuzi wa mazingira. Faini iliyopangwa na jiji ni Tsh. 50,000,
kati ya hizo nashauri tsh 20,000 wapewe wahanga hawa ili iwe kama motisha kwao”
alisema Dkt Mrema.
Kwa upande wake Daktari Bingwa
wa magonjwa ya akili kutoka hospitali ya taifa muhimbili, Dkt. Cassian
Nyandindi jamii haina budi kubadili mtizamo kuhusu watumiaji wa madawa ya
kulevya, kwa kuwa wahanga hao hawakupenda kuwa wategemezi katika matumizi ya
madawa hayo.
Dkt. Nyandindi alisema
hospitali hiyo kwa kwa sasa imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya
kuwahudumia wahanga wa matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo uhaba wa watumishi
pamoja na vituo vya kutolea huduma.
Dkt. Mrema ameeleza kuwa vijana
hawa walipokuwa wakituia dawa za kulevya walidhalilika katika jamii na
kuonekana kama wanyama na kupelekea hata jamiii kuwatenga kutokana na vitendo
vya uhalifu lakini baada ya kuanza matibabu wamebadilika kitabia na hata jamii
imeanza kurudisha imani kwao.
Akielezea kero wanazokutana
nazo Dkt. Mrema amesema kuwa wahanga wengi wamekuwa wakikamatwa na Polisi kwa
kukutwa na kete moja au mbili na kufunguliwa mashtaka mahakamani.
“Nimetoa ushauri badala ya
kuwapeleka magerezani wasioanza tiba bali wapelekwe hospitalini na waanzishiwe
tiba ili kuwarejesha katika utu wao,” alisema Dkt. Mrema.
No comments:
Post a Comment