Na
Jacquiline Mrisho – MAELEZO - Dar es Salaam
Serikali
imejipanga kuanzisha mikataba ya utendaji kazi kwa Taasisi za Umma katika mwaka
ujao wa fedha kwa ajili ya kuhakikisha watumishi hawafanyi kazi kwa mazoea.
Kauli hiyo
imetolewa jana Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angela Kairuki alipokuwa akifanya
mahojiano kwenye kipindi kinachorushwa na TBC1 cha ‘TUNATEKELEZA’ kinachoelezea
utekelezaji wa mipango na mikakati iliyowekwa na Wizara yake katika kipindi cha
Uongozi wa Awamu ya Tano.
Mhe. Kairuki
amesema kuwa kwa kawaida Watumishi wa Umma hupimwa utendaji kazi wao kwa kujaza
fomu za wazi zijulikanazo kama ‘OPRAS’ lakini upimwaji huo hauonyeshi utendaji
wa Taasisi nzima, hivyo ili kufahamu mipango
na malengo ya Taasisi ni lazima kuwe na upimaji wa utendaji kazi wa Taasisi nzima.
“Sisi
kama Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma tumeona kuna haja ya kuwa na mikataba ya
kupima utendaji kazi wa Taasisi husika ,tumeshakamilisha maandalizi na kila
kitu kikienda salama mwaka ujao wa fedha tutaanza zoezi hili”, alisema Mhe.
Kairuki.
Waziri
huyo ameongeza kuwa zoezi hilo limeshindikana kuanza mwaka huu wa fedha kwa
kuwa bado maandalizi yake hayajakamilika na kuongeza kuwa taasisi zote zinatakiwa
kupewa mafunzo kabla ya kusaini mikataba hiyo.
Amefafanua
kuwa Serikali itaingia makubaliano kwa taasisi husika kwa kufuata ngazi za
uongozi kuanzia kwa Mkuu wa Taasisi hadi kwa kiongozi wa juu kabisa wa Wizara
husika.
Aidha,
Mhe. Kairuki amewakumbusha Watumishi wa Umma kuwa kuvujisha nyaraka za Serikali
ni kosa la jinai hivyo kila mtumishi anatakiwa kuzingatia kanuni za kudumu za Utumishi
wa Umma ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa nidhamu na uwajibikaji wa hali ya
juu.
“Sheria
ya Usalama wa Taifa na Sheria inayosimamia masuala ya kumbukumbu za nyaraka
Serikalini inasema wazi kuwa ni kosa la jinai kuvujisha nyaraka za Serikali
kwahiyo natumia fursa hii kukemea mtu yeyote mwenye tabia hiyo kwa sababu hatua
kali zitachukuliwa dhidi yake”, alimalizia Mhe. Kairuki.
No comments:
Post a Comment