Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikagua mashine ya ukaguzi wa mizigo katika sehemu ya kuwasili abiria ya uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, upande wa uwanja wa zamani (Terminal One) wakati wa ziara yake ya ghafla aliyoifanya Ijumaa tarehe 13 Mei, 2016. Kulia kwa Rais ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda na kushoto ni Kaimu Meneja uendeshaji Lilian Minja.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuuliza maswali Meneja wa Uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere Bw. Paul Rwegasha, kuhusu dosari zilizopo katika mashine za kukagulia mizigo ya wageni wanaowasili kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, upande wa uwanja wa zamani (Terminal One)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwabana maswali maafisa wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere kuhusu dosari ya kutofanya kazi kwa mashine za ukaguzi katika sehemu ya kuwasili abiria ya uwanja wa zamani (Terminal One) .
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi,
Mawasiliano na Uchukuzi kwa kushirikiana na vyombo vya dola kuchukua hatua mara
moja dhidi ya dosari za ukaguzi zilizopo katika kitengo cha ukaguzi wa mizigo
na abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (Terminal One) Jijini Dar es salaam.
Rais Magufuli
ametoa agizo hilo leo tarehe 13 Mei, 2016 alipofanya ziara ya kushtukiza katika
uwanja huo na kubaini kuwa mashine za ukaguzi za sehemu ya kuwasili abiria na
mizigo hazifanyi kazi kwa muda mrefu.
Maafisa wa uwanja
wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere waliokuwa wakitoa maelezo juu
ya hali ya kitengo cha ukaguzi wa mizigo na abiria katika uwanja huo, walikuwa
wakitoa taarifa zinazotofautiana kuhusu utendaji kazi wa mashine za ukaguzi, hali
iliyosababisha Dkt. Magufuli aamue kuiagiza wizara husika kwa kushirikiana na
vyombo vya dola kuchukua hatua mara moja.
"Unajua mimi
sipendi kudanganywa, ni vizuri uzungumze ukweli tu, kwa nini nimeanzia hapa
huwezi ukajiuliza? eeeh sasa sipendi kudanganywa, ukinidanganya nitachukia sasa
hivi, wewe umenidanganya kwamba hiyo ndio mbovu na hii ndio nzima, nikawaambia
muiwashe hiyo nzima, akaja huyu mwenzako amezungumza ukweli kabisa, akasema hii
ni mbovu kwa miezi miwili. Dkt. Magufuli
aliwahoji Maafisa wa uwanja wa ndege.
"Kwa hiyo
mizigo inayoingia humu huwa hamuikagui kwa namna yoyote ile, kwa hiyo mtu
nikiamua kuja na madawa yangu ya kulevya, nikaja na dhahabu zangu, na almasi
zangu na meno ya tembo kwa kutumia hizi ndege ndogondogo napita tu"
Rais Magufuli aliendelea kuwabana
maafisa hao wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.
Rais Dkt. John
Pombe Magufuli amefanya ziara hii ya kushtukiza mara baada ya kuwasili katika
uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere akitokea Jijini Kampala nchini Uganda
ambako jana alihudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe.
Yoweri Kaguta Museveni.
Gerson Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es
salaam
13 Mei,
2016
No comments:
Post a Comment