Dk.
Sophia Mlote, mkazi wa Kinyerezi Zimbili jijini Dar es Salaam akiweka
sawa vifaa mbalimbali kwenye banda lake la kilimo ambamo amepanda
nyanya. Dk. Mlote anatekeleza kilimo hai kupitia mradi wa Green Voices
unaofadhiliwa na taasisi ya Foundation for Women of Africa ambayo
inaongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, María Teresa Fernández de la Vega. (Makala na Picha zimeandaliwa na www.brotherdanny.com
Bw. Abdon Hamaro, Ofisa Kilimo kutoka TAHA na mwezeshaji wa mafunzo ya akinamama wa kikundi cha ‘Green Voices Kinyerezi’,
akiendelea kuwaelekeza wanakikundi (hawapo pichani) namna ya kuendesha
kilimo hai cha nyanya. Mafunzo hayo yalifanyika hivi karibuni Kinyerezi,
jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa mradi wa Green Voices, Bi. Secelela
Balisidya (kulia), akiwa makini kuangalia Bw. Hamaro akiandaa mambo
mbalimbali kwa ajili ya kuwaelekeza wanakikundi namna bora ya kuendesha
kilimo hai cha nyanya.
Wanakikundi cha Green Vocies Kinyerezi wakifuatilia mafunzo hayo.
Christina
Lwiza (kushoto) akipokea pakiti ya mbegu ya nyanya kutoka kwa Dk.
Sophia Mlote tayari kwa kuwatika ili kuanzisha kilimo hai cha nyanya.
Bw.
Hamaro akiandaa tray maalum kwa ajili ya kuwapa wanakikundi kupandikiza
mbegu kabla ya kupeleka kwenye vitalu vyao. Hii ilikuwa ni sehemu ya
mafunzo ya vitendo.
Wanakikundi wakijaza udongo maalum kwenye tray kabla ya kuanza kupandikiza mbegu.
Bw. Hamaro akiwaelekeza kwa vitendo wanakikundi namna ya kupandikiza mbegu hizo.
Hapa wanakikundi wakiendelea kupandikiza mbegu kwenye tray.
10. Banda maalum ambalo ni shamba muhimu kwa ajili ya kilimo hai (green house) ambamo ndani yake nyanya zimestawi.
Picha ya pamoja ya wanakikundi cha Green Voices Kinyerezi.
NDANI
ya banda kubwa lililoezekwa na kuzungushiwa plastiki maalum katika Mtaa
wa Kinyerezi Zimbili jijini Dar es Salaam, Dk. Sophia Mlote akiwa
ameongozana na mtaalamu wa kilimo, Bw. Abdon Hamaro, anaonekana akipanga
vizuri vifaa vya kilimo pembeni ya matuta yaliyostawisha vizuri nyanya.
Pembeni
ya banda hili lenye ukubwa unaokadiriwa kuwa wa meta 8 kwa 12,
akinamama kadhaa wamezunguka wakitazama ustawi wa zao hilo huku Bw.
Hamaro akiendelea kutoa maelekezo ya namna ya kuendesha kilimo hai kinacholimwa katika mabanda maalum yajulikanayo kama green houses ikiwa ni sehemu ya mafunzo ya vitendo ya akinamama hao katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuongeza kipato.
Tofauti
na nyanya ambazo watu wamezoea kuziona zikilimwa katika mashamba
makubwa na bustani za wazi, nyanya hizi zinalimwa ndani ya banda ambao
ukubwa wake utategemea pia na eneo lililopo pamoja na uwezo wa mhusika
katika kulijenga banda hilo.
Hiki
ni kilimo hifadhi ambacho kinahimizwa kwa sasa ulimwenguni kote ili
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na uharibifu wa mazingira
na vyanzo vya maji.
“Mtu
yeyote anaweza kuendesha kilimo cha mazao mbalimbali kwa kutumia Green
house hata katikati ya Jiji la Dar es Salaam kama tunavyoona, ni rahisi
na rafiki wa mazingira kwa sababu unaweza kuendesha hata kwenye uwa wa
nyumba yako kama hivi,” Bw. Hamaro anaendelea kuwaeleza akinamama hao,
ambao ni wanakikundi wa mradi wa ‘Green
Voices’ unaofadhiliwa na taasisi ya Foundation for Women of Africa
yenye makao yake katika mji wa Madrid, nchini Hispania.
Mbali
ya kutunza mazingira, Bw. Hamaro kutoka Chama cha Wakulima wa Bustani
Tanzania (TAHA) anasema, kilimo hai kinasaidia kuzalisha vyakula visivyo
na kemikali ambavyo ni rafiki wa afya ya binadamu.
Katikati
ya Jiji la Dar es Salaam watu wamekuwa wakishuhudia kilimo cha mboga
mboga kwenye mabonde ya mito midogo, ambacho kinatumia umwagiliaji wa
maji machafu na yenye kemikali za kutoka viwandani, ambazo ni hatari kwa
afya ya binadamu.
“Mbegu
zinazotumika zimetengenezwa maalum na hazifanani za zile GMO
zinazopigiwa kelele, lakini pia unatakiwa kutumia mbolea za asili kama
mboji na samadi, kwa sababu ukitumia kemikali nyingi kwenye udongo,
mimea inanyonya na kemikali hizo zinabaki kwenye vyakula na hatimaye
kuingia miilini mwetu,” anafafanua Hamaro.
Vile
vile, Hamaro anasema kilimo cha Green house kinaweza kutumika hata kwa
matunda na kwamba kinatumia maji kidogo huku pia kikimpunguzia gharama
mkulima hasa kwa kuepukana na magonjwa mbalimbali ambayo yanasababishwa
na wadudu.
“Kwa
kuwa banda limefunikwa na kukingwa, hakuna wadudu waenezao magonjwa ya
mimea wanaoweza kuingia, lakini faida nyingine ni kwamba, unaweza
kudhibiti hali ya hewa kwa kupunguza ama kuongeza joto ili kuifanya
mimea kukua vizuri,” anaongeza.
Dk.
Mlote mwenyewe, ambaye ni Ofisa Mwandamizi katika Wizara ya Kilimo,
Chakula na Mifugo, ni mshiriki wa mradi wa Green Voices ambaye baada ya
mafunzo aliyoyapata, sasa anaieneza elimu hiyo kwa wanawake wenzake
majirani wa mtaa huo.
Yeyé ni miongoni mwa wanawake 15 waliopatiwa mafunzo ya
kuongeza ujuzi wa jinsi ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi ambayo
yaliendeshwa nchini Hispania chini ya ufadhili mkubwa wa taasisi ya
Foundation for Women of Africa inayojihusisha na maendeleo ya wanawake
wa Afrika, ambayo inaongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania,
María Teresa Fernández de la Vega.
“Niliamua
kuchagua mradi huu kwa sababu, kwanza ni rahisi kuuendesha kwa kuwa
shughuli zote zipo hapa nyumbani na hata kama nitarudi usiku kutoka
kazini, bado ninaweza kuingia humu shambani na kuhudumia mimea kwa kuwa
banda hili lina taa,” anaeleza.
Aidha,
anasema, kwa kuwa anakaribia kustaafu, na kwa elimu ya kilimo na uchumi
aliyonayo pamoja na utaalamu alioupata, ameona ni vyema aanzishe mradi
ambao siyo tu utampatia kipato, lakini pia utasaidia kutunza mazingira
pamoja na kuwa msaada kwa jamii kutokana na mazao yatakayovunwa.
“Niliamua
kuwaelimisha wanawake wenzangu katika mtaa huu na kuwashawishi waunde
kikundi hiki na tayari wamekwishapata mafunzo ya kutosha ambapo kila
mmoja amekuja na wazo la kuanzisha bustani ndogo nyumbani kwake ya
mtindo huu kwa mazao ambayo anaona yanafaa,” anaongeza Dk. Mlote, ambaye
ameeleza kwamba, anakusudia kupanua kilimo hicho kwa kupanda hata miti
ya matunda.
Kikundi
hicho cha ‘Green Voices Kinyerezi’ kinaundwa na wanawake 10, ambapo
mbali ya kujifunza kwa nadharia namna ya kuendesha kilimo hai kwa njia
ya green house, walipata fursa ya kufanya kwa vitendo kwa kupandikiza
mbegu za mazao mbalimbali ya mboga mboga kama nyanya, kabichi, hoho,
matango na matikiti maji kwenye bando hilo ambapo yatakapoota kila mmoja
atakwenda kupanda nyumbani kwake.
Christina
Lwiza, mmoja wa wanakikundi hicho ambaye anajishughulisha na biashara
ya uuzaji vinywaji kwenye grocery yake mwenyewe, anasema ameshawishika
kuanzisha kilimo cha nyanya nyumbani kwake ambacho kinaweza kumpatia
mapato ya nyongeza pamoja na kukidhi mahitaji ya nyumbani.
“Sijawahi kulima nyanya, lakini kwa mafunzo niliyoyapata, hakika naweza kuendesha kilimo hicho bila shida,” anasema Christina.
Karibu wanakikundi wote wamehamasika, ambapo kila mmoja ameamua kubuni zao ambalo linaweza kumfaa.
Mratibu
wa mradi huo, Bi. Secelela Balisidya, anasema mradi huo wa kilimo hai
cha nyanya kwa kutumia green house ni sehemu ya miradi 10 inayoendeshwa
nchini Tanzania kupitia Green Voices ambapo inaendeshwa katika mikoa
sita ya Tanzania Bara.
Mikoa
hiyo ni Dar es Salaam, Pwani, Mwanza, Kigoma, Morogoro na Kilimanjaro
ambapo inahusisha kilimo, usindikaji, ufugaji na utafiti.
“Miradi
hiyo ni kilimo cha miti ya matunda mkoani Kigoma, kilimo cha viazi
lishe visiwani Ukerewe mkoani Mwanza, Ufugaji Nyuki mkoani Morogoro na
Pwani, ukaushaji wa mbogamboga kwa kutumia nishati ya jua mkoani
Morogoro, usindikaji wa vyakula mbalimbali kutokana na muhogo mkoani
Pwani, kilimo hai cha mbogamboga, kilimo cha uyoga mkoani Dar es Salaam,
mradi wa majiko banifu mkoani Pwani na mradi wa utafiti wa jiko
linalotumia nishati ya jua mkoani Kilimanajro,” amefafanua Secelela
Balisidya.
Aidha,
amesema kwamba, lengo kubwa la mradi wa Green Voices ni kupaza sauti za
akinamama kueneza ujuzi wao wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi ili
jamii nzima ya Kitanzania iweze kujifunza zaidi na kuzitumia mbinu hizo
katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Mradi
huo unatarajiwa kutelekezwa kwa mwaka mmoja ili kutoa fursa kwa
akinamama kutoa ujuzi wao wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi na
sauti zao kusikika, kwa sababu kazi wanazozifanya kila siku za kilimo na
utunzaji wa familia zinahusiana moja kwa moja na mazingira hivyo
kuyaelewa zaidi mazingira na jinsi ya kupambana na mabadiliko ya
tabianchi.
Malengo ya dunia.
Kilimo
hai kinaendana na masuala mtambuka ya mazingira pamoja na kukabiliana
na uhaba wa chakula na kupunguza umaskini kama inavyoelezwa kwenye
Malengo Endelevu ya Dunia yaliyopitishwa mwaka 2015.
Kwa
mujibu wa malengo hayo, mataifa mbalimbali yamekubaliana kuhakikisha
yanatokomeza umaskini kwa namna zote pamoja na kukomesha njaa na kupata
uhakika wa usalama wa chakula na kuboresha lishe kwa kuhimiza kilimo
endelevu.
“Kilimo
hai ni endelevu kwa sababu unaweza kulima wakati wowote hivyo kinaweza
kukabiliana na njaa na uhakika wa chakula ni mkubwa, lakini pia
kitasaidia familia kuongeza kipato kwa kuuza ziada ya chakula
kitakachozalishwa,” anasema Hamaro.
Lakini
pia kwa kutumia kilimo hai, lengo namba sita la dunia linaweza kutimia,
kwani ni kilimo ambacho kinatumia maji kidogo, hivyo kuhakikisha
utunzaji mzuri wa vyanzo vya maji na matumizi sahihi ya maji yaliyopo.
Aidha, kilimo hai pia kinaweza kukidhi lengo namba 13 la dunia linalohimiza kupambana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake.
Sera ya Kilimo
Kilimo
hai ni sehemu ya mapendekezo yanayotajwa kwenye Sera ya Taifa ya Kilimo
ya mwaka 2013 ambayo inaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo kuelekea
mwaka 2025 kwa kuhimiza kilimo chenye tija pamoja na utumiaji mzuri wa
rasilimali zilizopo, hususan ardhi na maji.
Kwa
maana nyingine, kuhamasisha kilimo hai ni sehemu ya utekelezaji wa
malengo, dhima na dira ya sera hiyo hasa katika kipindi hiki ambacho
dunia inakabiliwa na changamoto ya uharibifu wa mazingira na mabadiliko
ya tabianchi, ambayo serikali pia imeainisha mikakati yake katika Sera
ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2007.
No comments:
Post a Comment