BALOZI SEIF ALI IDI: SHEREHE ZA MIAKA 52 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR ZIPO KAMA KAWAIDA.
Balozi Seif Ali Iddi akinukuu
kifungu cha Katiba ya Zanzibar kinachomruhusu Dkt. Ali Muhamed Shein
kuendelea kuiongoza Zanzibar mpaka atakapoapishwa Rais mwengine.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu
maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kufikia
miaka 52 Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Baadhi ya Waandishi wa habari
waliohudhuria mkutano wa Makamu wa Pili wa Rais w Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi wakifuatiliia mkutano huo uliofanyika Ofisini kwake Vuga Mjini
Zanzibar.
……………………………………………………………………………………………….
Na Khadija Khamis – Maelezo
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
imesema kuwa Maadhimisho ya Shereha za Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar
yapo kama kawaida na yanatarajiwa kuanza rasmi tarehe 3.12.2016 kwa
kazi za usafi wa mazingira katika maeneo mbali mbali ya makaazi pamoja
na sehemu za kutolea huduma za kijamii kama vile Hospitali Sokoni na
maeneo mengine.
Kauli hiyo imetolewa na Makamo
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipokuwa akizungumza
na waandishi wa habari Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema ingawa zoezi la usafi
hufanyika kila tunapoanza maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi lakini
kwa muda huu wananchi wanapaswa kuchukuwa juhudi maalum ili
kuhakikisha kuwa maeneo yote yanakuwa safi muda wote kwa vile hivi
sasa nchi inakabiliwa na tatizo kubwa la kuenea kwa maradhi ya
kipindupindu.
“Zoezi la usafi wa mazingira
litakuwa la lazima na kutaandaliwa utaratibu maalum kwa kila Mamlaka za
Mikoa ,Wilaya Baraza la Manispaa Mabaraza ya Miji na Halmashauri za
wilaya kuratibu zoezi la usafi na viongozi Wakuu wa Kitaifa wataungana
nasi katika katika maeneo watakayopangiwa, “Alisisistiza.
Amesema mbali na usafi wa
mazingira, katika maadhimisho ya mwaka huu kutakuwa na shughuli mbali
mbali zikiwemo ujenzi wa Taifa ,uwekaji wa mawe ya msingi na ufunguzi
wa miradi mbali mbali ya maendeleo pamoja na burudani na michezo na
kilele cha maadhimisho hayo itakuwa siku ya Jumanne katika Kiwanja cha
Amaani.
“Kama kawaida kila ifikapo
tarehe 12 Januari ya kila mwaka nchi yetu huadhimisha sherehe za
Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, kwa mwaka 2016 tutakuwa
tunatimiza miaka 52 tangu viongozi na wazee wetu walivyokomboa nchi
yetu,” alisema Balozi Seif Ali Iddi.
Alikumbusha kuwa mafanikio na
maendeleo yaliyopatikana Zanzibar yanatokana na imani na jitihada
kubwa za viongozi ambao ni wanamapinduzi chini ya uongozi wa Marehemu
Sheikh Abeid Amani Karume aliyeweka msingi imara wa mashirikiano .
Alisema siku ya kilele cha
maadhimisho hayo katika Uwanja wa Amaani kutakuwa na Gwaride la
Vikosi vya Ulinzina Usalama , Burudani ya Ngoma za Utamaduni pamoja na
Maandamano ya Wananchi wa Mikoa Mitano ya Zanzibar.
Makamo wa Pili Balozi Seif Ali
Iddi alisema kuwa sherehe hizo zitahudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa
Serikali na vyama vya siasa kutoka Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania .
Amewataka wananchi kujitokeza
kwa wingi katika maadhimisho ya miaka 52 ya Mpinduzi ya Zanzibar na
amewahakikishia Serikali imejipanga kikamilifu kuona kunakuwa na hali
ya utulivu na usalama mkubwa katika maeneo yote ya Zanzibar wakati wa
maadhimisho hayo.
No comments:
Post a Comment