Na Mwandishi Wetu
MAASKOFU wa madhehebu mbalimbali
wa Makanisa hapa Tanzania wamempongeza Makamu wa Rais Samia Suluhu
Hassan kukubali kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Krismasi
linalotarajia kufanyika Desemba 25 kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee
jijini Dar es Salaam.
Tamasha hilo linalokwenda sambamba
na Shukrani kwa Mungu baada ya uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 kwa
amani na utulivu, uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Askofu wa Kanisa la KKKT, Dk Alex
Malasusa anasema ni jambo jema kumshukuru Mungu baada ya uchaguzi Mkuu
uliofanyika kwa amani na utulivu kiasi cha kumpata rais mchapakazi.
Amefurahishwa na kukubali kuwa
mgeni rasmi kwa kuitikia wito wa ombi la madhehebu mengine ingawa yeye
ni Muislamu kwani kufanya hivyo ni kuzidi kuvunja makundi ya udini ndani
ya nchi yetu.
Anasema ni wakati wa kumshukuru
Mungu baada ya tukio kubwa la uchaguzi Mkuu ambako kabla yalifanyika
maombi ya kumuomba Mungu kuwapitisha katika uchaguzi Mkuu ambao
ulifanyika kwa amani na utulivu.
Askofu Dk. Valentino Mokiwa wa
Kanisa Anglican, jimbo Kuu la Dar es Salaam, amempongeza Msama
Promotions kwa kuandaa matamasha ya kumuimbia na kumtukuza Mungu
kupitia matamasha yake.
Askofu Mokiwa anasema ni suala la
kujivunia ikiwa ni mara ya kwanza kuwa na mgeni rasmi ambaye ni mwanamke
wa kwanza nchini kuwa Makamu wa Rais na kitendo chake kinaonekana kuwa
ni cha kizalendo.
Anasema ni jambo la kumshukuru
Mungu baada ya kufanikisha kumalizika kwa uchaguzi mkuu uliofanyika
Oktoba 25 mwaka huu hivyo amemtaka Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex
Msama kuendelea kujitolea kuandaa matamasha kama hayo yenye tija kwa
taifa.
Naye Askofu Mkuu wa jimbo la Mashariki la Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Dk Lawrence Kameta
anasema amefurahishwa na Makamu wa Rais, kuonesha uzalendo na
kukubali kuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo ambalo lenye lengo la
kushukuru baada ya uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Anasema kuwa kitendo hicho cha
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mgeni rasmi kimezidi
kuiaminisha Dunia kuwa Tanzania ni ya amani na haina matabaka ya kidini
na ukabila.
Katibu Mkuu wa Makanisa ya
Kipentekoste nchini, Askofu David Mwasota amesema kwamba
Tanzania imezaliwa upya kwa kutinga katika neema ambayo ilikuwa
inatarajiwa na wengi.
Askofu Mwasota anasema kuwa Rais
Magufuli hakukosea kumteua mama Samia kuwa makamu wa Rais wa jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Askofu wa Kanisa la Wasabato,
Warwa Marekana anasema wamefurahishwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu
Hassani kukubali kuwa mgeni rasmi katika tamasha la Krismasi ambalo
linakwenda sambamba na kushukuru Tanzania kupita kwenye uchaguzi Mkuu
uliofanyika Oktoba 25.
Marekana anasema kukubali kuwa
mgeni rasmi inathibitisha kwamba tamasha hilo halina ubaguzi wa dini
kwani Waislamu na Wakristo
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo
la Morogoro, Telesphor Mkude amesema kuwa kama amani itakuwepo nchini
ana amini serikali ya Awamu ya Tano chini ya John Pombe Magufuli
kutakuwa na mabadiliko makubwa ya kimaendeleo.
Amesema kuwa wao kama viongozi wa
dini wanafurahishwa na jinsi kiongozi mwanamama shupavu tena muislamu
kuamua kuabudu pamoja na wakristo katika tamasha hilo la shukrani.
Hiyo ni nzuri na sisi kama
viongozi wa dini tunaiunga mkono kampuni ya Msama Promotions kwa kutoa
mwaliko kwa Makamu wa Rais hivyo tunaamini atakuwa chachu ya kuwahimiza
wananchi wengine ambao sio wakristo kujumuika katika kutoa shukrani kwa
mungu mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu.
Alisema, hata kama Magufuli
atakuwa ni kiongozi bora kiasi gani lakini kama amani haitapatikana
itakuwa ni kazi bure hivyo amewataka wananchi kuienzi amani iliyopo.
Alisema amekuwa akifuatilia
matamasha yanayoandaliwa na kampuni ya Msama Promotions, yamekuwa
yakilenga katika jamii hivyo ni kitu cha kushukuru kwa kampuni hiyo
kuandaa matamsha kwa lengo la kuenzi amani.
Amesema angeomba hali hiyo
iendelee hata mikoani ili kuwafanya wananchi wa mikoani kuona umuhimu
wa amani haiitajiki Dar es Salaam pekee.
Amesema kuwa anashukuru kumaliza
kwa uchaguzi mkuu kumalizika salama na nchi imepoa baada ya kupatikana
Rais ambaye anaonekaa kuwa na dhamira ya kweli katika kuhakikisha
anaipelekea Tanzania katika uchumi wa kati.
Askofu Mkude amesema suala la
amani ni muhimu na amewataka Maaskofu na Mapadri kuhakikisha wanahubiri
amani wanapokuwa katika ibada zao.
Askofu wa Kanisa la Menonite, Amos
Mhagache amesema ni nafasi yetu kumshukuru Mungu kwa kutubariki kupita
katika kipindi kigumu cha uchaguzi Mkuu.
Askofu Mhagache anasema kwamba
Yesu Kristo ni mwokozi hasa sasa hivi ndio nchi Mungu aliyotupa katika
kipindi hiki baada ya uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25.
No comments:
Post a Comment