Na Lilian Lundo, Maelezo
Wafanyakazi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania wampongeza Mhe. Rais Dokta Jakaya Kikwete, kitendo cha
kuheshimu Katiba ya Nchi, Utawala wa Sheria na uhuru wa mahakama.
Pongenzi hizo zimetolewa leo na
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman wakati wa hafla ya
mahakama hiyo ya kumwuaga Rais Kikwete iliyofanyika jijini Dar es
Salaam.
Akisoma taarifa ya maendeleo ya
mahakama kwa kipindi cha miaka kumi ya Serikali ya Awamu ya Nne, Jaji
Mkuu alisema Rais Kikwete alipoingia madarakani mwaka 2005, kiwango cha
fedha kilichokuwa kimetengewa na Serikali mwaka 2005/2006 kwa ajili ya
uendeshaji wa Mahakama kilikuwa Sh. bilioni 36.6 kwa mwaka huo wa fedha
kiasi hicho kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia zaidi ya
Sh.bilioni 89.9 kwa kipindi cha mwaka huu wa fedha.
“Ongezeko hili ni asilimia
143, kutoka mwaka wa fedha wa 2005/2006 mpaka sasa kutokana na bajeti
hii shughuli nyingi za Mahakama zimeboreshwa.’’ alisema.
Jaji Mkuu pia alieleza juu ya
ongezeko la rasilimali watu kwa kipindi hicho kutoka watumishi 4,972
mpaka kufikia watumishi 6,052 ambao ni ongezeko la watumishi 1080.
Pia alimpongeza Rais Kikwete
kwa kuteua majaji wengi zaidi katika kipindi chake ukilinganisha na
majaji waliokuwepo vipindi vitatu vya Serikali iliyopita.
Jaji Mkuu alionge kuwa, kiwango
cha usikilizaji mashauri kimeongezeka mwaka hadi mwaka huku mashauri ya
muda mrefu yanaharikishwa kwa kufanyika vikao maalum Mahakama Kuu.
Pia katika kipindi hicho,
mahakama hiyo imeweza kuanzisha Mfuko wa Mahakama chini ya sheria ya
uendeshaji wa Mahakama namba 4 ya mwaka 2011.
Kwa upande wake Rais Kikwete
wakati akitoa nasaha kwa watumishi wa mahakama hiyo, alisema mafanikio
yamepatikana kwa juhudi za pamoja, yaani Serikali hiyo pamoja na
watumishi hao.
Alisema kuwa, wakati anaingia
madarakani kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005,
mahakama hiyo ilikuwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na bajeti
finyu, uhaba wa vitendea kazi, uhaba wa nguvu kazi na mahakama zilikuwa
hazitoshi.
“Lakini nafarijika kuwa
naondoka kukiwa na mabadiliko makubwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania,
ikiwa ni pamoja na kuboresha muundo wa mahakama ambao pia umeongeza
rasilimali watu na kuboresha maslahi ya Majaji ili kuwawezesha kufanya
kazi kwa bidii,” alisema Rais Kikwete.
Katika hafla hiyo Rais
Kikwete alikabidhiwa Tuzo na Jaji Mkuu ikiwa ni kumbukumbu ya rekodi
aliyoiweka ya mahusiano mema na Mahakama yanayotakiwa kuigwa na awamu
zijazo.
No comments:
Post a Comment