I: UTANGULIZI
a) Masuala ya jumla
Mheshimiwa Spika,
1. Leo
tunahitimisha shughuli za Mkutano wa Kumi na Sita na Kumi na Saba wa
Bunge lako Tukufu. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi
wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo.
Mheshimiwa Spika,
2. Mkutano huu ulijumuisha kujadili kazi kubwa zifuatazo:
Kwanza: Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2015/2016;
Pili: Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi wa Mwaka 2014 [The Tax Administration Bill, 2014];
Tatu: Muswada wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani wa Mwaka 2014 [The Value Added Tax Bill, 2014];
Nne: Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2014 [The Public Private Partnership (Amendment) Bill, 2014]; na
Tano: Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa Mwaka 2014, [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2014].
Aidha, ni hivi mapema leo Miswada 11 ya Sheria ya Serikali kuhusu mambo mbalimbali ilisomwa kwa mara ya kwanza.
Mheshimiwa Spika,
3. Nitumie
nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kushiriki katika
Kamati ya Mipango hapa Bungeni kwa kujadili kwa kina mapendekezo
yaliyowasilishwa na Serikali kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2015/2016. Maoni
na Ushauri tuliopokea kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge tutauzingatia
wakati wa maandalizi ya Bajeti ya mwaka 2015/2016. Vilevile, niwashukuru
kwa kujadili na kupitisha Miswada ya Sheria niliyoitaja hivi punde.
b) Maswali
Mheshimiwa Spika,
4. Katika Mkutano huu, Waheshimiwa
Wabunge wamepata fursa ya kuuliza maswali ya kawaida na yale ya Papo
Papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Jumla ya maswali 241 ya msingi na 662 ya nyongeza yameulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Aidha, Maswali 18 ya msingi na 13 ya nyongeza yaliulizwa na kujibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
c) Kauli za Mawaziri
Mheshimiwa Spika,
5. Waheshimiwa
Wabunge watakumbuka kuwa tarehe 17 Novemba, 2014 nilipata fursa ya
kutoa Kauli ya Serikali kuhusu Mgogoro kati ya Wakulima na Wafugaji
Wilayani Kiteto. Aidha, baadhi ya Waheshimiwa Mawaziri walipata nafasi
ya kutoa Kauli mbalimbali za Serikali kama ifuatavyo:
i) Kauli
ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuhusu taarifa
zilizotolewa na Vyombo vya Habari za shutuma dhidi ya Serikali za China
na Tanzania kujihusisha na Biashara Haramu ya Pembe za Ndovu na ile
inayohusu Kuridhia Mkataba wa Umoja wa Afrika kuhusu Demokrasia,
Uchaguzi na Utawala wa Mwaka 2007;
ii) Kauli ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii kuhusu Hali ya Dawa Nchini na Matibabu ya Saratani Nchini; na
iii) Kauli
ya Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika kuhusu Mwenendo wa Soko la
Nafaka na Mpango wa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo.
Maazimio
Mheshimiwa Spika,
6. Tarehe 7 Novemba, 2014 Waheshimiwa
Wabunge walipata fursa ya kujadili na kupitisha Azimio la Bunge la
Kumpongeza Mheshimiwa Anne Semamba Makinda (Mb.), Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa
kuwa Rais wa Mabunge ya Nchi Wanachama wa Jumuiya
ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-PF). Aidha, katika Mkutano
huu Waheshimiwa Wabunge walipata pia fursa ya kujadili na kuridhia Maazimio mengine yafuatayo:
i) Azimio la Bunge kuhusu Itifaki ya Kuanzishwa kwa Tume ya Utafiti wa Afya, Jumuiya ya Afrika Mashariki;
ii) Azimio
la Bunge la Kufuta na Kusamehe Madai au Hasara itokanayo na Upotevu wa
Fedha na Vifaa vya Serikali kwa Kipindi Kilichoishia tarehe 30 Juni,
2011;
iii) Azimio la Bunge la kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu Ushirikiano katika Masuala ya Kiulinzi [The East African Protocol on Cooperation in Defence Affairs]; na
iv) Azimio
la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Uzuiaji wa Vitendo Haramu dhidi ya
Usalama wa Miundombinu ya Kudumu iliyojengwa chini ya Bahari katika
Mwambao wa Bara ya Mwaka 1988 [The Protocol for the Suppression of
Unlawful Acts Against the Safety of Fixed Platforms located on the
Continental Shelf – SUA, 1988].
e) Taarifa Maalum za Kamati
Mheshimiwa Spika,
7. Mwisho, lakini siyo kwa umuhimu, Waheshimiwa Wabunge walipokea Taarifa Maalum ya Kamati ya Hesabu za Serikali (Public Accounts Committee - PAC) Kuhusiana na Miamala iliyofanyika katika Akaunti ya “ESCROW” ya TEGETA pamoja na umiliki wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Mheshimiwa Spika,
8. Naomba
nitumie fursa hii, kwanza kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika kwa
kuruhusu Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwasilisha Taarifa hii
Maalum kwenye Bunge lako Tukufu kwa mujibu wa Kanuni za Bunge. Aidha,
niwashukuru Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Kamati kwa uchambuzi wao wa
kina na Mapendekezo yao kama yalivyowasilishwa katika Mkutano huu.
Nitumie fursa hii pia kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri waliozungumza kwa
niaba ya Serikali nzima kutoa maelezo yaliyolenga kutoa ufafanuzi wa
hali halisi ya suala hili la Akaunti ya ESCROW ya TEGETA na pia kujibu baadhi ya Hoja za Kamati.
HAPA AMEONGELEA MASUALA YA ESCROW ACCOUNT.
UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA
a) Maandalizi ya Kupiga Kura tarehe 14 Desemba, 2014
Mheshimiwa Spika,
9. Uchaguzi
wa Viongozi wa Serikali za Mitaa Tanzania Bara unatarajiwa kufanyika
tarehe 14 Desemba, 2014. Uchaguzi huo ni wa kawaida na unahusisha
Uchaguzi wa Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji, Mitaa, Wajumbe wa Halmashauri za Vijiji na Wajumbe wa Kamati za Mitaa. Taarifa nilizonazo ni kwamba hadi sasa maandalizi ya Msingi kuwezesha Uchaguzi huo kufanyika yamekamilika.
Mheshimiwa Spika,
10. Ili
kuhakikisha kuwa Uchaguzi huo unafanikiwa, maandalizi ya Kanuni za
Uchaguzi yalifanyika kupitia Vikao vya Wadau mbalimbali ili kupata
maoni, mapendekezo na ushauri ambao umesaidia katika kuboresha Kanuni za
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Wadau walioshirikishwa ni pamoja na
Viongozi wa Vyama vya Siasa vyenye Usajili wa Kudumu; Makatibu Tawala wa
Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Asasi Zisizo za
Kiserikali (AZAKI).
b) Uandaaji wa Kanuni za Uchaguzi za Mwaka 2014
Mheshimiwa Spika,
11. Katika
maandalizi ya awali, orodha ya Vijiji, Mitaa na Vitongoji iliandaliwa
na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 22 Agosti, 2014 lenye
Tangazo la Serikali Namba 300 kwa Halmashauri za Miji na Tangazo Namba 301 kwa Halmashauri za Wilaya. Orodha hiyo imejumuisha Kata, Vijiji na Mitaa. Katika Uchaguzi wa mwaka huu, jumla ya Vijiji 12,443, Vitongoji 64,616 na Mitaa 3,741 vitahusika kwenye Uchaguzi.
Mheshimiwa Spika,
12. Ili
kufanikisha Uchaguzi huo, Serikali imekwishaandaa na kuchapisha
Vipeperushi, Fomu za Wagombea, Rejesta ya Wapiga Kura, karatasi za
kuonyesha Vituo vya Kupigia Kura, Mabango na Matangazo mengine kuhusu
Elimu kwa Mpiga Kura. Tayari vifaa hivyo vimepelekwa Mikoani na vingine
vinaendelea kupelekwa. Aidha, Masanduku ya Kupigia Kura yameshanunuliwa
na tayari yameshasambazwa katika Mikoa yote Tanzania Bara.
Mheshimiwa Spika,
13. Kwa
vile siku zilizobakia kufikia tarehe ya Kupiga Kura ni chache, natoa
Wito kwa Wananchi ambao hawajajiandikisha katika Rejesta ya Wapiga Kura
wafanye hivyo bila kukosa. Aidha, Viongozi wa Vyama vya Siasa wawahimize
Wanachama wao na Wananchi kwa ujumla wajitokeze kwa wingi kujiandikisha
na hatimaye wajitokeze siku ya Kupiga Kura. Aidha, Wasimamizi wa
Uchaguzi wahakikishe vifaa vya Uchaguzi vinafika kwenye maeneo yao kwa
wakati.
Mheshimiwa Spika,
14. Napenda
nitumie nafasi hii kutoa Rai kwa Viongozi wa Vyama vya Siasa waendeshe
kampeni kwa amani na kuepuka maneno ya uchochezi, kubaguana kwa misingi
ya ukabila, rangi, udini ama hali ya mtu mambo ambayo yanaweza
kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani. Aidha, nawaomba Viongozi wa
Vyama vya Siasa na Wanachama wao, wakishapiga kura wasiendelee kukaa
katika Vituo vya Kupigia Kura, bali watawanyike na kusubiri muda wa
matokeo.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
15. Leo
nimeona nizungumzie masuala muhimu yanayochangia kusukuma Gurudumu letu
la Maendeleo. Kabla sijahitimisha hotuba yangu, naomba nitumie nafasi
hii kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu. Kipekee
nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika, pamoja na Naibu Spika kwa kutuongoza
vizuri. Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri ya kuongoza vikao
vya Bunge lako Tukufu. Aidha, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa
kazi nzuri na kwa michango mbalimbali wakati wa Mkutano huu.
Mheshimiwa Spika,
16. Naomba
pia nimshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake wote pamoja na
Wataalam wote wa Serikali na Taasisi zake ikijumuisha Taasisi za Sekta
Binafsi, kwa misaada ya Kitaalam na huduma mbalimbali za kufanikisha
Mkutano huu. Niwashukuru pia Waandishi wa Habari kwa kazi nzuri
walizofanya kuhakikisha kuwa taarifa za majadiliano na maamuzi
mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia Wananchi. Niwashukuru Madereva
kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuwasafirisha kwa usalama Waheshimiwa
Wabunge, Viongozi mbalimbali, Wataalam na Wasaidizi wote walioshiriki
katika Mkutano huu.
Mheshimiwa Spika,
17. Nimalizie kwa kuwatakia wote safari njema mnaporejea kwenye maeneo yenu ya kazi na katika majimbo yenu. Aidha,
niwatakie mapumziko mema ya Sikukuu ya Christmas na Mwaka Mpya wa 2015.
Ninaamini kwamba, Mwenyezi Mungu atatulinda na kutuvusha salama sote
kama tulivyo hadi kuuona Mwaka Mpya wa 2015. Baada ya kusema hayo,
naomba sasa kutoa Hoja kwamba, Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi
tarehe 27 Januari, 2015 saa 3:00 Asubuhi litakapokutana katika Mkutano wa 18 kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.
Mheshimiwa Spika,
18. Naomba kutoa Hoja.
No comments:
Post a Comment