AFISA ELIMU SHULE ZA SEKONDARI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA NJOMBE ISACK MGAYA AKIWA OFISINI KWAKE AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI.
Halmashauri Ya Wilaya ya Njombe inatarajia kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya wazazi,walezi na wafanyabiashara ambao wamehusika na utoroshaji wa watoto wa shule na kukatisha masomo yao kwani kitendo hicho kinamfanya mwanafunzi kushindwa kupata haki ya elimu.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Elimu shule za sekondari wa halmashauri ya Wilaya ya Njombe bwana Isack Mgaya, Kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete la kuwataka wakuu wa Mikoa,Wilaya, Wataalamu wa Elimu na viongozi wengine kuhakikisha wanasimamia kikamilifu suala la utoro lisiendelee shuleni.
Aidha Bwana Mgaya amewataka wafanyabiashara mbalimbali kuwaacha watoto wasome badala ya kuwaajili katika shughuli zao ambapo Wazazi wanatakiwa kufuatilia maendeleo ya watoto wao ikiwa ni pamoja na kuwapa mahitaji mbalimbali ya shule ili wanafunzi wasipate vishawishi vya kutoroka masomo.
Bwana Mgaya amesema halmashauri ya Wilaya ya Njombe Imejipanga kikamilifu kufuatilia watoto waliochaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari kwa kutembelea shule mbalimbali za halmashauri hiyo kuanzia augost 11 mwaka huu ili kubaini wazazi ambao hawajawapeleka watoto shuleni kujiunga na masomo hayo.
Amesema takwimu zinaonesha kuwa wanafunzi wa Kiume ndiyo wanaotoroka masomo shuleni na kwenda kutafuta ajira zikiwemo kuendesha pikipiki,bajaji,kufanya biashara za baa na grosari Kwa watoto wa kike jambo ambalo limesababisha vijana wengi kutokuwa na elimu ya ujuzi ambao ungewasaidia katika maisha.
Diwani wa kata ya Ikuna bwana Valentino Hongori amesema kata yake imejipanga kikamilifu kufuatilia utoro wa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari na kuwataka wazazi, viongozi na walimu wa shule husika kushirikiana kuwabaini watoto watoro na kuwarejesha shuleni.
Kwa upande wao wadau wa elimu Wilayani Njombe wametaka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao ili kudhibiti utoro shuleni kwa kushirikiana na walimu,viongozi na jamii inayowazunguka.
Tatizo la utoro kwa wanafunzi limetajwa kushamiri nchini ambapo linatokana na baadhi ya wazazi na walezi kuwatelekeza watoto wao na wakati mwingine watoto wenyewe kushindwa kufahamu umuhimu wa elimu jambo ambalo linasababisha kutoroka masomo.
No comments:
Post a Comment