Saturday, May 17, 2014
WANANCHI WAKOSA KUSOMEWA HESABU ZA MAPATO NA MATUMIZI KWA MIAKA 3,MHASIBU WA KIJIJI IGOSI ASIMAMIA MAPATO YA KIJIJI BADALA YA MTENDAJI WA KIJIJI WILAYANI WANGING'OMBE
Wananchi wa Kijiji cha Igosi Wilayani Wanging'ombe mkoani Njombe wamekataa kupokea taarifa ya hesabu za mapato na matumizi ya kijiji ambayo hawajasomewa kwa kipindi cha Miaka mitatu na kumuomba diwani wa kata hiyo kutolea ufafanuzi juu ya Muhasibu kuwa na mamlaka ya kukusanya michango na ushuru wa kijiji pamoja na kutoa maamuzi ya kuuza mali za kijiji huku zaidi ya shilingi milioni moja za mapato ya kijiji zikidaiwa kupotea.
Wakizungumza kwenye Mkutano wa hadhara wananchi wa Kijiji cha Igosi wamesema kuwa miongoni mwa mambo wanayolalamikia ni pamoja na afisa mtendaji wa kijiji hicho kutoshiriki kukusanya michango na mapato ya ushuru wa vibanda vya biashara,mapato ya michango ya mradi wa maji kutosomwa kwa wananchi pamoja na Mhasibu huyo kushiliki kuuza msitu wa kijiji pasipo kutolea taarifa za kuuzwa kwa msitu huo.
Aidha wananchi hao wamesema kuwa uongozi wa kijiji hicho umekuwa na tabia ya kuahirisha mikutano ya kijiji pasipo kuwajulisha wananchi kuahirishwa kwake kutokana na sababu wanazo zijua wao huku viongozi hao wakidaiwa kutumia vibaya madaraka yao katika kuwanyanyasa baadhi ya wananchi wanaohoji uhalali wa matumizi ya michango ambayo imekuwa ikichangiwa.
Akizungumza kwenye Mkutano huo Diwani wa kata ya Igosi bwana Elly Chengula amepiga marufuku kwa viongozi wa vijiji vyote vya kata hiyo kuruhusu wahasibu kuhusika na ukusanyaji wa mapato ya kijiji na kwamba mwenye mamlaka ya kushika michango hiyo ni afisa mtendaji wa kijiji na siyo mwenyekiti ama Mhasibu kwenda kudai michango hiyo kwa wananchi.
Kwa upande wake afisa mtendaji wa kijiji hicho bwana Lupyana Fute ametolea ufafanuzi sababu ya kutoshiriki kukusanya michango na ushuru wa kijiji tangu alipohamishiwa kijijini hapo kwa madai alizuiliwa na wajumbe wa serikali ya kijiji akiwemo mwenyekiti kwamba mapato yote ya kijiji hukusanywa na Muhasibu jambo ambalo limesababisha kufanya kazi katika mazingira magumu.
Akijibu maswali ya wananchi Mhasibu wa kijiji cha Igosi bwana Bedon Dembe amekili kufanya kazi za kukusanya mapato ya michango na ushuru wa kijiji na kutowasomea taarifa za hesabu za mapato na Matumizi wananchi kwa takribani miaka mitatu huku akikiri kupoteza zaidi ya shilingi milioni moja ya mapato ya kijiji hicho na kwamba ameshindwa kukabidhi vitabu vya michango kutokana na wananchi kumtaka asome hesabu za mapato na matumizi kwanza ndipo aachia ngazi.
Hata hivyo Mkutano huo umeahirishwa pasipo suluhu ya kero za wananchi na utafanyika tena mnamo mei 20 mwaka huu kutokana na viongozi wa kijiji hicho kutotoa taarifa zilizo sahihi kuhusiana na taarifa za hesabu za mapato na Matumizi ya michango ya ushuru na Mradi wa maji ambao unatekelezwa kijijini hapo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment