Ulinzi ulinzi mkali uliimalishwa mahakamani hapo
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya
imewahukumu kifungo cha miaka 30 kila mmoja aliyekuwa askari wa Jeshi la Polisi
na wenzie wanne wakituhumiwa kwa unyang’anyi wa kutumia silaha.
Akisoma hukumu hiyo mahakamani hapo Hakimu mfawidhi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite alisema watuhumiwa wote
kwa pamoja wanatiwa hatiani kutokana na ushahidi uliotolewa na mashahidi
wawili.
Alisema ushahidi uliotolewa na shahidi
wa kwanza ambaye alikuwa dereva Ezekia Matatira (34) na shahidi wa pili
Sreedhar Pasupelet(38) mwenye asili ya Kiasia kwamba haukuacha shaka
yoyote na ulishabihiana.
Awali Mwendesha mashtaka wa Serikali,
Archiles Mulisa akisaidiwa na Basilius Namkambe alisema washtakiwa wote kwa
pamoja wanatuhumiwa kwa kosa moja la unyang’anyi wa kutumia Silaha
kinyume cha Sheria kifungu cha 287 sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho
mwaka 2002.
Mulisa aliwataja watuhumiwa hao
kuwa ni Mshitakiwa namba moja ambaye ni Askari Polisi PC James mwenye namba
F8302,
Elinanzi Mshana(22)Mkazi wa Iyela Jijini
Mbeya, Askari Magereza mwenye namba B 500 Sajenti Juma Mussa(37) wa Gereza la
Ruanda Mbeya,Mbaruku Hamis(29) Mkazi wa Iyela na Amri Kihenya(38) Mkazi wa
Iyela.
Alisema watuhumiwa hao walitenda kosa
hilo Januari 3, Mwaka huu majira ya saa 11 jioni katika eneo la Mlima Kawetere
barabara ya Mbeya Chunya.
Alisema watuhumiwa hao kwa pamoja
walitenda kosa hilo kwa kulizuia gari aina ya Pick Up lililokuwa likiendeshwa
na Ezekia Matatira (34) Mkazi wa Iyunga Jijini Mbeya ambaye alikuwa na mtu
aliyekuwa akifahamika kwa jina la Sreedhar Pasupelet(38) mwenye asili ya Kiasia
wakitumia magari madogo mawili ambayo ni GX 100 Toyota Cresta T 782 BEU na Gari
lingine ambalo lilikuwa na namba za Chesesi GX 6011832 aina ya Grand Mark
II.
Kwa upande wake Wakili wa utetezi,
Ladilaus Lwekaza, aliiomba mahakama kuwapunguzia hukumu washtakiwa kwa kile
alichodai watuhumiwa bado ni vijana na hawana rekodi ya makosa ya nyuma.
Aliongeza kuwa washtakiwa wote kwa
pamoja wanafamilia zao ambazo zinawategemea hivyo wapewe adhabu ndogo ili
waweze kuzitumikia familia zao pamoja na taifa kwa ujumla.
Kutokana na maombi hayo Hakimu Mteite
hakukubaliana naye na badala yake alisema kwa mojibu wa sheria kutokana na kosa
la unyang’anyi wa kutumia silaha washtakiwa walipaswa kwenda jela miaka 30
pamoja na viboko.
Aliongeza kuwa adhabu ya viboko
ameifuta kutokana na mshtakiwa namba mbili kujeruhiwa kwa risasi wakati wa
tukio hivyo watasamehewa wote kwa pamoja ila watatumikia kifungo cha miaka 30
jela kila mmoja.
|
No comments:
Post a Comment