JESHI
la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanamke mmoja Mwanahawa
Nasoro(32) Mkazi wa Mtaa wa Airport Kata ya Iyela Jijini Mbeya
akituhumiwa kumfanyia vitendo vya unyanyasasaji Mtoto wa ndugu yake.
Mwanamke
huyo anatuhumiwa kumtesa, mtoto John Msumba(3) ambaye ni Shangazi yake
baada ya kumfungia ndani kumnyima chakula na kumpa kipigo kikali
kilichompelekea kuwa na majeraha mwilini mwake pamoja na maumivu makali
yaliyosabisha kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa matibabu
zaidi.
Akizungumza na Mtandao huu, Mjumbe wa Mtaa wa Airport, Rehema Mohammed alisema kuteswa na kukamatwa kwa Mwanamke huyo kuligundulika Machi 12, Mwaka huu majira ya saa nne asubuhi kufuatia kuwepo kwa msiba jirani na nyumba yake.
Alisema
wakati watu wako msibani na mlango wa nyumba ya Mwanamke huyo ukiwa
umefungwa na kufuli kwa nje ilisikika sauti ya Mtoto akilia ndani jambo
ambalo liliwashangaza wengi ndipo alipotoa taarifa kwa Mwenyekiti wa
Mtaa Enock Mwampagama ambaye pia alitoa taarifa kwa Mtendaji wa Mtaa
aliyelitaarifu Jeshi la Polisi.
Alisema
baada ya Mwanamke huyo kubanwa alikiri kuwepo kwa Mtoto ndani na kwamba
alikuwa akimfanyia hivyo kutokana na tabia yake ya kujisaidia haja
kubwa hovyo hali iliyokuwa imemchosha na kuamua kumpa adhabu kama hiyo.
Alipoulizwa kuhusiana na wazazi wa Mtoto huyo alidai kuwa hafahamu mahali alipo mama mzazi na kuongeza kuwa baba yake aliyefahamika kwa jina la Sumba Dinda kuwa yupo machimboni Wilayani Chunya kwenye Migodi ya Dhahabu.
Jeshi
la Polisi limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa
Mwanamke huyo anashikiliwa hadi hapo Afya ya mtoto ambaye ni mhanga wa
Tukio hilo itakapoimarika ndipo atakapofikishwa mahakamani kujibu
mashtaka yanayomkabili.
Wakati
huo huo baadhi ya Wasamaria wema wameziomba taasisi zinazoshughulikia
masuala ya unyanyasaji wa kijinsia na watoto zikiwemo Mtandao wa
Waandishi wa habari Wanawake na Jinsia (TAMWA) na Taasisi ya Jinsia
(TGNP) kuingilia kati maswala hayo ili kukomesha vitendo hivyo katika
jamii.
Aidha
baadhi ya wasamaria wema wajitokeza kuchangia fedha za matibabu ya
mtoto huyo yanayoendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya baada ya
mmoja wa Waandishi wa Mtandao huu ambaye pia ni Mtangazaji wa Kituo cha
Redio cha Bomba cha Jijini Mbeya
kuendesha harambee fupi katika kipindi chake na kufanikiwa kukusanya
shilingi 35,000/= zilizotumika kununulia madawa.
Mbali
na hilo TAMWA inaombwa kushughulika moja kwa moja na mtoto huyo ili
kuhakikisha haki inapatikana ikiwa ni pamoja na kupiga vita unyanyasaji
wa kijinsia uliokithiri ndani ya jamii kutokana na juhudi ziliooneshwa
na mtandao huo katika kukabiliana na hali hiyo kwa kutoa Elimu kwa
wanahabari mara kwa mara katika kuibua vitendo hivyo na kuvikemea.
|
No comments:
Post a Comment