Pages

CONTACT

0757092504/0678321772

Thursday, January 17, 2013

MADENGE AJIPANGA JIMBO LA IRINGA MJINI


                                            Mbunge wa jimbo la Iringa mjini  Peter Msigwa (chadema)

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Iringa, Mahamoud Madenge ameanza kazi ya kufa na kupona itakayowasaidia kulirejesha mikononi mwao jimbo la Iringa Mjini katika Uchaguzi Mkuu ujao.

 Jimbo hilo ambalo toka uchaguzi uliohusisha vyama vingi vya siasa uanze mwaka 1995 limekuwa likiongozwa na CCM, hivi sasa linaongozwa na Mchungaji Peter Msigwa wa Chadema.

Madenge ambaye pia ni mfanyabiashara anayemiliki kiwanda cha maji aina ya Ndanda ameainisha kazi kubwa nne zikazowasaidia kufikia lengo hilo.

 Kazi hizo ni pamoja na kukagua uhai wa chama kuanzia ngazi ya shina hadi wilaya na kuwakumbusha wanachama na wapenzi wa chama hicho misingi, madhumuni na itikadi ya chama hicho.

 “Nimeanza kutembelea wanachama wetu katika ngazi ya shina, tawi na kata na kwa kushirikiana na viongozi wenzangu tunatoa darasa ili waifahamu itikadi ya chama, misingi na madhumuni yake,”
alisema.

 Alizitaja kazi zingine kuwa ni kuhakikisha watendaji katika ngazi mbalimbali za serikali wanatekeleza Ilani ya CCM kama ilivyoelekezwa.

“Nitahakikisha mafanikio na changamoto zake naziwasilisha katika kikao cha Halmshauri Kuu ya Taifa ili hatua zinazostahili zichukuliwe,” alisema.

 Alisema kazi ya nne itakuwa kufanya mikutano ya hadhara na ya ndani na makundi mbalimbali ya jamii ili kueleza utekelezaji wa Ilani na kusikia changamoto zinazowakabili wananchi ili zifanyiwe kazi.
 Alisema chama hicho mjini hapa kitaanza kujibu mapigo ya wapinzani wao wakubwa wa kisiasa ambao ni Chadema kwa kuzindua rasmi mikutano yake ya hadhara kwa kuwaalika viongozi mbalimbali wa CCM wa ngazi ya Taifa.

“Tarehe 26 mwezi huu wa kwanza tutaanza na Makamu Mwenyekiti wetu Mzee Phillip Mangula, na baadaye tutaleta wengine wengi kwa kuzingatia mapendekezo ya wanachama na wananchi,” alisema.

Alisema wanaendelea pia kujipanga kulifikia kundi la vijana wa matabaka mbalimbali ili kusikiliza vilio vyao na hatimaye kwa pamoja waje na mapendekezo yatakayolenga kuboresha hali zao.

Madenge alichaguliwa kuwa mjumbe wa NEC katika Uchaguzi Mkuu wa chama hicho uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana baada ya kuwashinda Vitus Mushi ambaye ni Diwani wa Kata ya Mtwivilla mjini hapa na mfanyabishara Michael Mlowe. Imeandaliwa na mdau wa matukio toka Iringa Francis Godwin.

No comments:

Post a Comment