Pages

CONTACT

0757092504/0678321772

Wednesday, November 30, 2016

UFAULU DARASA LA SABA WAPANDA MKOA WA SINGIDA; ELFU KUMI NA NNE KUJIUNGA NA KIDATO CHA KWANZA 2017.


Kiwango cha ufaulu wa mitihani ya kumaliza elimu ya msingi Mkoani Singida kimepanda kutoka wastani wa asilimia 58.41 mpaka asilimia 69.25 ikiwa ni ongezeko la asilimia 11 huku wanafunzi 14,759 wakichaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari kwa kidato cha kwanza kwa mwaka 2017.
Buhacha Baltazar Kichinda akiongoza kikao cha uteuzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka 2017 kama Kaimu Katibu Tawala Mkoa na mwenyekiti wa kikao hicho amesema mkoa umefaulisha wavulana 6,852 na wasichana7,907 huku akiwapongeza waalimu wote kwa bidii ya ufundishaji iliyopelekea mkoa wa singida kushika nafasi ya 12 kati ya Mikao 26 ya tanzania bara.
Kichinda ameipongeza halmashauri ya Itigi kwa kushika nafasi ya kwanza kati ya halmasahuri saba za mkoa wa singida na ya 38 kitaifa kati ya halmashauri 186 za Tanzania bara huku ikifaulisha kwa asilimia 80.41. Aidha amewatia moyo halmasahuri ya Mkalama kwa ufaulu hafifu wa 57.51 na kuwa nafasi ya 155  kitaifa.
Kichinda ameongeza kuwa kwa sasa kila Mkurugenzi wa halmasahuri anapaswa kukaa na wadau wake wa elimu ili kupanga mikakati ya kuboresha zaidi elimu, amesema lengo kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kila mwanafunzi aliyefaulu anajiunga na kidato cha kwanza na kumaliza elimu ya sekondari.
Amesema sekta ya elimu inachangamoto mbalimbali ikiwemo utoro wa walimu na wananfunzi, miundombinu ya vyumba vya madarasa kutotosheleza mahitaji halisi, upungufu wa waalimu, uhaba wa nyumba za walimu pamoja na waalimu wenyewe kuwa wachache tofauti na mahitaji halisi hivyo amewata wadau wa elimu kujipanga kutatua changamoto hizo na sio kusubiria serikali kuu kufanya kila kitu.
Aidha kichinda amesema kuwepo na utaratibu wa kuwapongeza waalimu hasa kwenye shule zilizofanya vizuri ili iwe motisha kwa kazi wanayoifanya huku akiitangaza shule ya msingi Utaho ya halmasahuri ya Ikungi kuwa ya kwanza kimkoa kwa shule zenye wananfunzi zaidi ya 40 na shule ya msingi Aghondi ya Itigi kuwa ya kwanza kimkoa kwa shule ambazo zina wanafunzi chini ya 40.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo amesema ili kuboresha elimu mkoani Singida msisitizo uwepo wa kuhakikisha wananfunzi wote wanapata chakula shuleni ili waweze kusikiliza kwa umakini mzuri.
Tarimo ameongeza kuwa wazazi wanapaswa kutambua kuwa elimu bila malipo haiwaondolei wajibu wao kama wazazi wa kuhakikisha wanafunzi wanakula, wanalala na kuvaa hivyo hivyo watakaposhirikishwa katika kuchangia chakula, ujenzi wa mabweni au shuguli za elimu wajitoe kwani wamiliki wa shule ni wazazi.
Amesema utaratibu wa kufanya ukaguzi ili kuwatambua waalimu watoro au wazembe ufanyike katika halmashauri zote na kwa viongozi wote wanaotembelea vijijini bila ya kusubiri ziara maalumu ya ukaguzi na kuongeza kuwa hali hiyo itawaongezea umakini waalimu katika kutekeleza majukumu yao lakini pia watendaji watabaini changamoto za waalimu na shule na kuzitatua kwa uharaka.

No comments:

Post a Comment