WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameliagiza Baraza la Madiwani la Manispaa ya
Dodoma lifanye marekebisho ya kodi inayotozwa kwenye soko la Majengo ambayo imepandishwa
kutoka sh. 20,000 hadi sh. 150,000 kwa mwezi.
Amesema anatambua maamuzi ya Baraza ni ya kikao halali lakini hakubaliani
na ongezeko hilo ambalo ni sawa na asilimia 650 kwani linawaumiza wananchi.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Oktoba Mosi, 2016) wakati
alipotembelea soko hilo akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo ya kutolea huduma
za jamii mjini Dodoma.
Amesema soko hilo linatakiwa lifanyiwe mapitio ili liwekwe kwenye hali
nzuri na Manispaa ihakikishe maboresho hayo yanafanyika bila ya kuwaumiza
wafanyabiashara.
“Kwa kuwa uamuzi wa kupandisha kodi ulifanyika kisheria na kupitishwa na
baraza la Madiwani, sitaki kuvunja sheria. Nawaagiza mkazungumze tena katika
baraza na muangalie namna ya kupunguza gharama hizo,” amesema.
“Hali hii haiwezekani kuachwa iendelee, huku ni kuwaumiza wananchi. Mkurugenzi
wa Manispaa nenda kaitishe tena kikao, mfanye mazungumzo upya kwenye baraza
lenu na mje mnieleze mmekubaliana nini” amesisitiza.
Pia ameitaka Manispaa hiyo ihakikishe makusanyo yote ya fedha katika soko
hilo yanakusanywa kwa njia ya kielektroniki ili fedha hizo ziweze kuleta tija
na kuwataka Mkuu wa mkoa na wilaya kuwachukulia hatua wotewatakaobainika kuiba
fedha hizo.
Amesema Manispaa hiyo inatakiwa kupanua masoko kwa kujenga masoko mapya
makubwa katika maeneo ya Nkuhungu, Kisasa, Mlimwa na Barabara ya Iringa ili
huduma hizo zisambazwe.
Mapema akisoma risala yake, Mwenyekiti wa soko hilo, Bw. Godson Rugazama
alimueleza Waziri Mkuu changamoto zinazolikabili soko hilo kuwa ni pamoja na
ongezeko la kodi isiyozingatia uhalisia wa maisha na shughuli za wajasiriamali
sokoni hapo. “Kodi imeongezeka kutoka sh. 20,000 hadi 150,000 kwa mwezi,”
alisema.
Mwenyekiti huyo alitaja changamoto nyingine ni uchakavu wa mifereji ya
maji machafu, kuvuja kwa paa la soko, bidhaa kuuzwa katika maeneo yasiyokuwa rasmi
na kusababisha wateja kutoingia sokoni.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu ametembelea
hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma na kukagua maeneo mbalimbali zikiwemo wodi
za wagonjwa, jengo la wazazi na jengo jipya la wagonjwa wa Bima ya Afya (NHIF).
Akiwa hospitalini hapo, pia alizungumza na watumishi wa sekta ya afya na
kuwataka wawahimize wananchi wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambao
unawawezesha mtu kulipia bima ya matibabu kwa ajili ya mhusika, mwenza wake na
watoto/watemezi wanne na serikali inajazia kiasi kile kile alichochangia.
Akizungumzia miundombinu ya afya mkoani humo, Waziri Mkuu alisema mkoa wa
Dodoma hauna shida ya matibabu au utoaji wa huduma ya afya kutokana na
miundombinu iliyopo hivi sasa.
Aliwataka wafanye kazi kwa uadilifu na uaminifu na kuongeza tija katika
utendaji kazi wao huku wakitanguliza utunzaji wa mali ya umma.
“Ninawasihi mjenge tabia ya huruma kwa wagonjwa huku mkitambua unyeti wa
kazi mliyonayo. Ninaamini mtatunza vifaa mlivyonavyo na siyo kuvichukua na kuvipeleka
kwenye zahanati zenu au maduka yenu binafsi ya dawa,” alionya.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMAMOSI, OKTOBA MOSI, 2016
No comments:
Post a Comment