Pages

CONTACT

0757092504/0678321772

Monday, October 17, 2016

LUKUVI ATOA HATI KWA WANANCHI WA MAKAZI HOLELA MOROGORO.



Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi katika ziara yake ya mkoani Morogoro (17-10-2016) ameendelea kutekeleza program ya kurasimisha makazi holela kwa wananchi 116, ambapo amegawa hati 60 za awali na kumuagiza Afisa ardhi kuhakikisha anatoa hati zilizobakia ndani ya mwezi mmoja.

Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika mpango wake wa kuboresha maendeleo ya wananchi na makazi yao, imeanzisha program ya kurasimisha makazi holela kwa wananchi. Mpango huu ni wakupima, kupanga na kuwapatia hati wananchi waliojenga katika makazi yasio na mpangilio rasmi.

Akiwa mkoani morogoro Mhe. Waziri alitembelea baadhi ya makazi ya wananchi hao katika kata ya Bigwa na kujionea jinsi wananchi wanavyounga mkono juhudi za serikali katika kurasimisha makazi holela.Wananchi hao wa Bigwa kwa umoja wao walipima ardhi zao na kufuata utaratibu wa mipango miji kwa mujibu wa taratibu za serikali.

Aidha, Lukuvi alifanya ziara ya kushtukiza katika Masijara ya Ardhi ya Manispaa ya Morogoro, na kukuta idadi kubwa ya hati za wananchi zimekaa zaidi ya mwaka mzima bila ya kuwafikia wahusika. Alihoji juu ya suala hilo, na kutoa agizo kwa Mkurugenzi wa Manispaa hati hizo kuwafikia walengwa ndani ya mwezi mmoja.

Baada ya ziara hiyo Mheshimiwa Waziri aliongea na wananchi wa Morogoro katika ofisi za Manispaa ya Morogoro na kusikiliza kero zao mbalimbali za ardhi na kuzitatua papohapo. Katika mazungumzo yake aliwataka wananchi waunge mkono juhudi za serikali kurasimisha makazi yao ili waweze kuishi katika makazi salama yanayotambulika na pia waweze kufaidika na ardhi yao kama kupata mikopo Benki au katika mambo mengine ya maendeleo yao.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akimuhoji Afisa ardhi Manispaa ya Morogoro Bw. Abenance Kanomoga (wa kwanza kushoto), kwanini amekaa na hati za wananchi kwa zaidi ya mwaka mmoja bila kuwajulisha wahusika kuja kuzichukua.
 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akigawa hati kwa wakazi wa Bigwa mkoani Morogoro..

 Baadhi ya wananchi wa mkoani Morogoro wakimsikiliza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi.
1.       Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ajiongea na wananchi wa mkoani Morogoro.

No comments:

Post a Comment