Na Ismail Ngayonga, MAELEZO.
KAMPUNI
ya Reli Tanzania (TRL) inakusudia kuongeza mabehewa 4 kwa ajili ya
abiria wanaotumia huduma ya usafiri wa treni kutoka kituo cha Dar es
salaam hadi Pugu kufikia mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.
Ongezeko
hilo litafanya mabehewa kufikia 20 kutoka 16 yaliyopo sasa hali
itakayoongeza ufanisi wa utoaji wa huduma ya usafiri huo kwa abiria
wanaotumia usafiri huo.
Hayo
yamesemwa na Afisa Uhusiano wa TRL, Midladjy Maez ambaye alisema hatua
hiyo ni mkakati wa TRL wa kukabiliana na changamoto ya usafiri huo kwa
nyakati za asubuhi na jioni ambapo choombo hicho cha usafiri kimekuwa
kikikabiliwa na ongezeko kubwa la watumiaji.
Maez
alisema usafiri huo kwa sasa umekuwa ukitumiwa na idadi kubwa ya
wananchi hususani kwa nyakati za asubuhi na jioni na hivyo kusababisha
kuzidiwa na wasafiri ikilinganisha na uwezo wa chombo hicho.
“Nawaomba
abiria wote wafuate taratibu wakati wa kutumia usafiri wetu ikiwemo
kukata tiketi katika vituo vyetu, kwani iwapo itabainika abairia hana
tiketi na akaingia ndani ya treni basi adhabu kali zitachuliwa dhidi
yake ikiwemo kifungo cha miezi 3 hadi 6” alisema Maez.
Aidha
Maez aliwataka abiria kutumia lugha za kistaarabu kwa wafanykazi wa
treni pindi wanapobaini changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza
wakati wa kutumia vyombo hivyo badala ya kutumia lugha zisizo za
ustaarabu ambazo huwakwaza watumishi wa treni hiyo.
Akizungumzia
kuhusu mabadiliko ya matumizi ya kituo cha Kamata kilichopo katika eneo
la karikoo Jijini Dar es Salaam, Maez aliwataka abiria wanaotumia kituo
hicho kuhamia katika kituo kidogo kilichopo ndani ya ofisi za TRL Mtaa
wa Nkhurumah ambapo abiria wote watahudumiwa pasipo na usumbufu.
Akifafanua
zaidi Maez alisema ni wajibu wa abiria wote kufuata sheria, kanuni na
taratibu za matumizi ya chombo hicho ikiwemo kukata tiketi kwani
utaratibu huo hutumika ulimwenguni kote na si Tanzania pekee.
No comments:
Post a Comment