Na Raymond Mushumbusi-MAELEZO
Serikali imejipanga kuipa nguvu Sera ya wazee
nchini kuwa Sheria itakayowasaidia wazee kujikwamua katika changamoto
mbalimbali zinazowakabili kwa sasa.
Mpango huo umetolewa leo na Waziri wa
Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
alipokuwa akizungumza na baadhi ya viongozi wa wazee wa mkoa wa Dar es
Salaam alipokutana nao leo ofisini kwake Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,wazee
na Watoto Mhe. amesema wazee wanakumbwa na changamoto nyingi katika
maisha yao ya kila siku nakusema kuwa azma ya Serikali ya awamu ya Tano
ni kuhakikisha wazee wanapata mahitaji yao muhimu ambayo ni huduma ya
afya,haki ya kuwezeshwa kiuchumi na uwakilishi katika vyombo vya
maamuzi.
“Mimi mwenyewe nalichukua jukumu hili la
kufanikisha kuandikwa kwa mswaada wa Sheria ya wazee nchini na kuipeleka
katika Bunge mwezi Septemba ili tuwe na Sheria itakayowezesha kuwabana
watu ambao watakaidi kutekeleza masuala yahusio wazee” Alisema Mhe.Ummy.
Naye mwenyekiti wa wazee wa mkoa wa Dar es
Salaam Mzee Hemed Mkali akiwasilisha mada katika kikao hicho amempongeza
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli
kwa kuwajali na kuwapa kipaumbele wazee kwa kuwapa wizara ambayo
itawasaidia kutatua changamoto zinazowakabili na wanaimani na Waziri
husika na watashirikiana naye ili kufanya wazee wa Tanzania waishi
katika maisha mazuri.
Aidha Waziri wa Afya,Maendeleo ya
Jamii,Jinsia,wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ameziagiza Halmashauri
zote nchini katika Hospitali zilizopo chini yao kuanzisha na kuboresha
madirisha kwa ajili ya wazee na kuongeza kuwa huduma kwa wazee ni bure
kuanzia kumwona Daktari, Vipimo mpaka madawa na kuhamasiha wazee kuungwa
kwenye Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF) ambao unatoa huduma za afya katika
maeneo mengi zaidi.
Kikao hiki cha wazee wa mkoa wa Dar es salaam
na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,wazee na Watoto dhumuni
kubwa ni kwa wazee ni kuomba kukutana na Mhe. Rais Dkt John Pombe
Magufuli kujadili mshtakabali wa maendeleo ya wazee nchini.
No comments:
Post a Comment