Pages

CONTACT

0757092504/0678321772

Tuesday, January 12, 2016

PROF. MUHONGO ATAKA TANESCO KUSHIRIKIANA NA WAZALISHAJI WADOGO

RA1
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akimsikiliza Mkurugezi Mkuu wa Kampuni ya Kufua umeme kwa kutumia mabaki ya miti aina ya Miwati na kampuni ya kuzalisha nguzo za umeme , TANWAT, Dkt. Singh Rajeer (wa nne kulia) wakati alipotembelea kampuni hiyo katia ziara yake ya kutembelea miradi ya umeme Mkoa wa Njombe. Wengine katika picha (wa pili kushoto) ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba, wa kwanza kulia ni Katibu Tawala, Mkoa wa Njombe, Jackson Saitabahu (wa kwanza kulia) na wa pili kulia ni Kamishna Msaidizi wa Madini, Kanda ya Ziwa Nyasa, Mhandisi Fred Mahobe.
RA2
Meneja wa Kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia maji katika Bwawa la Kihansi, Mhandisi Pakaya Sakaya (Wakwanza kulia)akimweleza jambo Wazriri wa Nishati na Madini, Profesa Sospter Muhongo (katikati), wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya umeme katika kituo cha kufua umeme cha Uwemba, nje kidogo ya mji wa Njombe. Kwa mujibu wa Mhandisi Pakaya, Bwawa hilo lina uwezo wa kuzalisha kilowati 843. Wa kwanza kushoto mbele ni ni Katibu Tawala, Mkoa wa Njombe, Jackson Saitabahu.
RA3
Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo akimsikiliza Sister Imaculata Mdoe wa Shirika la Wabenedictin Njombe ( kushoto kwake) wakati wa ziara ya Waziri katika bwawa la kufua umeme la Uwemba. Katika risala yake Sister Imaculata alimweleza waziri ombi la serikali kusaidia ujenzi wa bwawa linalomilikiwa na Shirika hilo katika eneo hilo ambalo litakuwa na uwezo wa kuzalisha kilowati 317 za umeme kwa kutumia maji na uwezo wa kuhudumia vijiji vinne.
RA4
Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba (katikati) akimweleza jambo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati wa ziara yake. Aidha, katika ombi lake kwa Waziri, Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa Shirika la Wabenedictin kusaidiwa ili waweze kutekeleza mradi wao wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji katika eneo la Uwemba nje kidogo ya mji wa Njombe, kutokana na umuhimu na mahitaji yake kwa jamii inayotarajiwa kunufaika na mradi huo.
RA5
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospter Muhongo na uongozi wa Mkoa wa Njombe, akiwemo pia Mbunge wa Njombe Mjini Edward Mwalongo wakifanya majumuisho ya ziara yao nje ya kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia maji katika bwawa la Uwemba mara baada ya kutembelea miradi kadhaa ya kufua umeme katika Mkoa huo.
RA6
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospter Muhongo akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika kampuni ya kufua umeme kwa kutumia mabaki ya miti aina ya Miwati na kampuni ya kuzalisha nguzo za umeme ya TANWAT. Wanaoshuhudia ni baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo na ujumbe uliongozana na waziri katika ziara hiyo.


Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kufanya majadiliano na Kampuni ya Kufua Umeme kwa kutumia mabaki ya miti ya Miwati ya TANWAT, ili kampuni hiyo iongeze kiwango cha uzalishaji umeme kutoka Megawati 2 zinazozalishwa sasa kufikia megawati 10.
 
Agizo hilo linafuatia ziara ya Waziri aliyoifanya katika kampuni hiyo ikiwa ni ziara yake ya kikazi kutembelea miradi ya umeme katika Mkoa wa Njombe, ambapo Meneja Mkuu wa Misitu wa kampuni hiyo, Antery Kiwale amemweleza , Prof Muhongo kuwa, kampuni hiyo ina uwezo wa kuzalisha megawati 2.5 na kutumia megawati 1.4 kwa matumizi ya kiwanda na kiasi cha megawati 0.6 kinauzwa kwa TANESCO.
 
Aidha, Prof. Muhongo amewataka TANESCO kubadilika kiutendaji ili kuongeza wigo wa uzalishaji umeme kwa kuwatumia wazalishaji wakubwa, kwa kati na wadogo ambao wote kwa pamoja watasaidia kuondoa tatizo la uhaba wa nishati hiyo muhimu ambayo inatajwa kuwa kichocheo kikuu cha ukuaji kiuchumi.
 
“Tunazunguka kukagua na kuangalia ni maeneo yapi yatatusaidia kuongeza kiasi cha uzalishaji umeme tunaouhitaji. Wazalishaji wadogo, wakubwa na wa kati wote watasaidia kufikia malengo yetu ya kuhakikisha tunakuwa na umeme mwingi na wa kutosha. Sote tunajua umeme ni ajira na umeme ni viwanda. Bila umeme hatuwezi kuwa na viwanda vya kutosha”,aliongeza Prof. Muhongo.
Katika hatua nyingine, Waziri Muhongo ameagiza TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kufanya majadiliano na TANWAT ambao pia ni wazalishaji wa nguzo za umeme , kufanya majadiliano na kampuni hiyo yenye uwezo wa kuzalisha nguzo 120,000 kwa mwaka, ili iuze nguzo hizo badala ya wakandarasi kuagiza nje ya nchi. 
 
“REA na TANESCO watakuja hapa kuangalia nguzo hizi na kufanya ukaguzi kama zinakidhi viwango vya TANESCO. Ikiwa zinakidhi vigezo, REA wawaelekeze Wakandarasi kununua nguzo za TANWAT badala ya kununua nguzo nje kama ilivyo sasa ambapo wananunua nchi za Kenya, Uganda, Zambia na Afrika Kusini”, amesisitiza Prof. Muhongo.
 
Akikagua mradi wa Kufua umeme wa Maji (Mini Hydro) uliopo Uwemba nje kidogo ya mji wa Njombe, Prof. Muhongo ameagiza TANESCO kuandaa orodha ya vyanzo vya umeme vinavyotokana na maji na vilivyo katika gridi na visivyo katika gridi na kujadiliana na wazalishaji ili kukubaliana nao namna ya kuuziana umeme.
“Uzalishaji umeme kwa kutumia maji ndiyo rahisi zaidi.

 TANESCO angalieni orodha hiyo na wao wawaeleze Mikataba yao muone na mkubaliane namna ya kuuziana umeme. Bila umeme wa mwingi na wa uhakika hatuwezi kuwa na viwanda vya kutosha,”ameongeza Prof.
Waziri Muhongo ameongeza kuwa, ni wajibu wa Serikali kuwasaidia na kufanya kazi na wazalishaji wadogo wa umeme ili wasaidie kuongeza kiwango cha uzalishaji umeme na hivyo kuutaka uongozai wa Mkoa wa Njombe kufuatilia kwa pamoja na TANESCO suala hilo na kulifanyia kazi kwa karibu.
Aidha, Prof.Muhongo amewaagiza TANESCO kuharakisha matengenezo ya mtambo ulioharibika katika kituo cha kufua umeme cha Uwemba ili kuongeza uzalishaji wa umeme wa uhakika.
Mbali na Mkoa wa Njombe katika ziara yake ya kutembelea miradi ya umeme, Prof Muhongo pia atatembelea Mikoa ya Ruvuma, Mbeya na iringa ambapo pia atakagua maeneo ya utafiti na uchimbaji wa Makaa ya Mawe.

No comments:

Post a Comment