WAZIRI MKUU ANUSA UFISADI KIGOMA
* Ni ubadhirifu wa fedha za umma, atoa siku mbili kukamilisha uchunguzi
* Ataka apewe taarifa ya maandishi Januari Mosi, 2016
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ametoa siku mbili kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Eng. John
Ndunguru kukamilisha uchunguzi wake na kumpatia taarifa ya maandishi juu
ya tuhuma ubadhirifu wa fedha za umma unaohusisha uuzwaji wa jengo la
KIGODECO na viwanja 12 vya Manispaa
ya Kigoma/Ujiji ambao unadaiwa kukiuka taratibu.
ya Kigoma/Ujiji ambao unadaiwa kukiuka taratibu.
Ametoa agizo hilo leo mchana
(Jumatano, Desemba 30, 2015) kwenye ukumbi wa NSSF, mjini Kigoma wakati
akizungumza na viongozi na watendaji mbalimbali wa mkoa huo alipokuwa
akifanya majumuisho ya ziara yake ya siku mbili mkonai humo.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema
anazo taarifa kuwa jengo hilo liliuzwa kwa sh. milioni 370/- pamoja na
jengo jingine la MIBOS kwa sh. milioni 50/- licha ya kupewa barua na
Mkuu wa Mkoa huo kusitisha uuzwaji wa jengo pamoja viwanja hivyo, bado
liliuzwa.
“Katibu Tawala wa Mkoa kaa na
Mkurugenzi wa Manispaa, Mhandisi wa Manispaa na Mhasibu na unipatie
taarifa kwa maandishi ifikapo Jumamosi hii,” alisema Waziri Mkuu huku
akishangiliwa.
“Nataka kujua nani alifanya
tathmini ya jengo, ni kwa nini jengo liliuzwa kwa thamani hiyo, je ndiyo
thamani halisi ya jengo? Ni kwa nini RC alipozuia, utaratibu
uliendelea? Je, utaratibu wa uuzaji ulifuatwa? Ni kwa nini viwanja
viliuzwa chini ya thamani,? Katibu Tawala kaa na watu wako na uniletee
hiyo taarifa kwa maandishi. Tukigundua kuna mianyamianya tutachukua
hatua za kinidhamu,” alisema.
Viongozi walioagizwa kukutana na
Katibu Tawala wa Mkoa ni Mkurugenzi wa Manispaa, Eng. Boniface Nyambele;
Mhandisi wa Manispaa, Eng. Boniface William na Mhasibu wa Mapato wa
Manispaa, Ndg. Bawili Mkoko.
Kuhusu uuzwaji wa jengo na
viwanja, imebainika kuwa Mkuu wa Mkoa huo, Luteni Kanali (Mst), Issa
Machibya alizuia uuzaji huo kwa barua ya tarehe 16 Juni 2015 akitaka
viwanja hivyo vitumike kwa matumizi ya manispaa na mchakato huo
usitishwe hadi mwakani lakini agizo lake lilipuuzwa na jengo likauzwa
kwa sh. milioni 370 ambayo ni bei ya kiwanja pekee.
Tuhuma nyingine zinazopaswa
kuchunguzwa ni pamoja na matumizi ya sh. milioni 809 kwa ajili ya ujenzi
wa maabara. Kiasi hicho kilitolewa kutoka kwenye fedha za miradi ya
maendeleo (Capital Development Grants-CDG), Mradi wa Programu ya
Kuendeleza Sekta ya Kilimo na Mifugo (ASDP), Mradi wa Uendelezaji Miji
(Tanzania Strategic Cities Programme –TSCP) na Miradi ya Maendeleo ya
Elimu ya Sekondari (SEDP).
Inadaiwa kwamba Mkurugenzi huyo
kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wa idara ya mipango na fedha
walitumia ujenzi wa maabara kama kigezo cha kuchota fedha hizo bila
kutoa taarifa kwa wakuu wa idara husika ambao walikasimiwa fedha hizo.
Tuhuma nyingine ni manunuzi hewa
ya vipuri (spare parts) vyenye thamani ya sh. milioni 8 na manunuzi hewa
ya stationeries yenye thamani ya sh. milioni 4.6/-. Haya yanadaiwa
kufanywa Julai 25, mwaka huu na Mkurugenzi huyo akishirikiana na Mhasibu
Mkoko.
Waziri Mkuu amerejea jijini Dar es Salaam mchana huu.
No comments:
Post a Comment